Prime
Yanga, AS FAR hakuna aliye salama Zanzibar
Muktasari:
- Msimu uliopita, Yanga iliishia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikikusanya pointi nane wakati huo AS FAR ikiishia katika hatua ya Robo Fainali ambapo ilitolewa na Pyramids FC.
Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga kesho kuanzia saa 10:00 jioni wanarusha karata yao ya kwanza ya hatua ya makundi katika mashindano hayo dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambao unatumika na Yanga kwa mechi zake za nyumbani za mashindano hayo.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika mashindano ya Klabu Afrika ingawa ipo historia ya timu za Tanzania na Morocco kukutana katika mashindano tofauti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Wakati saa zikizidi kusogea kukaribia mchezo huo, kuna rekodi mbili za ufungaji ambazo hapana shaka zinaziweka safu za ulinzi za timu zote mbili katika presha kuelekea mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu.
Rekodi ya kwanza ni ya wastani mkubwa wa mabao katika mechi tano zilizopita za mashindano ya Klabu Afrika ambazo zimechezwa uwanjani hapo na rekodi ya pili ni makali ya ufungaji ya kila timu katika mechi ambayo imecheza hivi karibuni.
Ukianzia ya kwanza, katika mechi tano zilizopita za Mashindano ya Klabu Afrika, zilizochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, idadi ya mabao 15 yamefungwa ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa mchezo.
Mechi hizo zote tano, zilishuhudia nyavu zikitikiswa na hakuna mechi ambayo ilimalizika kwa sare tasa jambo lililofanya wastani wa mabao kwa mechi yawe matatu.
Rekodi ya pili ni ya ufumaniaji nyavu ambao timu hizo mbili zimeonyesha kwenye mechi zao 10 zilizopita ambazo zimecheza hivi karibuni.
Yanga katika mechi 10 zilizopita za mashindano tofauti na kirafiki, imepachika idadi ya mabao 20 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa mchezo.
AS FAR Rabat nayo katika mechi 10 zilizopita za mashindano tofauti, imefumania nyavu kama Yanga ambapo ina mabao 20 sawa na wastani wa mabao mawili kwa mechi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kuwa timu yake imejiandaa vyema kukabiliana na FAR Rabat.
"Kwa kesho ni mechi ya kwanza kwenye kundi. Kila mmoja anakiri kwamba ni kundi la kifo. FAR Rabat ni timu imara na timu ambayo imefanya vizuri katika misimu miwili iliyopita. Tunataka kuendelea na nyakati nzuri na tunaamini kesho kwa uwepo wa sapoti ya mashabiki wetu na kazi ya pamoja kama timu, tutafanya vizuri," amesema Goncalves.