Yanga yaiua USM Alger ikikosa ubingwa CAF

Muktasari:

  • Ndoto za Yanga kutwaa Kombe la Shirikisho zimefifishwa na mabao ya ugenini licha ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika fainali ya pili dhidi ya USM Alger.

Dar es Salaam. Yanga imeandika historia nyingine usiku huu kwa kushinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini ikalikosa taji la kwanza la CAF kutokana na faida ya bao la ugenini kuwabeba Waalgeria.

Wenyeji ilitwaa taji hilo la kwanza kwao baada ya awali kushinda ugenini 2-1 na matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2, lakini kanuni ya bao la ugenini ikawapata taji hilo kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algers na Yanga iliupiga mwingi tofauti na ilivyocheza jijini Dar.

Kocha Nasreddine Nabi aliwatumia mabeki watano, ikiwamo Dickson Job kama kiungo namba sita na kuwabana wenyeji na kufanikiwa kupata bao hilo pekee dakika ya saba tu likiwekwa kimiyani kwa penalti na beki Djuma Shaban baada ya Kennedy Musonda kuchezwa madhambi.

Ushindi huo hata hivyo haukuisaidia Yanga kubeba taji, lakini ilishuhudiwa straika wa timu hiyo Fiston Mayele akibeba tuzo ya mfungaji Bora wa michuano hiyo kwa kufunga mabao saba na kuasisti mara tatu.

Yanga imekuwa timu ya pili ya Tanzania kufika hatua ya fainali ya michuano ya CAF baada ya Simba kufanya hivyo mwaka 1993 kwenye fainali za Kombe la CAF ambalo lilikuja kuungwanisha na Kombe la Washindi mwaka 2004 na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kumaliza kama mshindi wa pili kumeifanya Yanga kuvuna kitita cha Sh2.3 bilioni, huku USM Alger ikizoa Sh4.7 bilioni za ubingwa.

Katika mechi hii ya fainali ambayo ilishuhudiwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, Yanga itajilaumu kwa kushindwa kupata ushindi mnono kutokana na kutengeneza nafasi nyingi na kutawala mchezo huo kulinganisha na wenyeji waliopoteza penalti dakika ya 59 baada ya kipa Djigui Diarra kudaka mkwaju wa nahodha wa USM Alger, Zineddine Belaid.

Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea nchini usiku huu kwa ndege iliyotolewa na serikali kuwapeleka Algeria, ambapo itafika Dar es Salaam alfajiri kujiandaa na mechi mbili za kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons zitakazochezwa Juni 6 na Juni 9 kisha kwenda Tanga kwenye fainali ya ASFC ikitarajiwa kuvaana na Azam FC, mechi itakayopigwa Juni 12 Uwanja wa Mkwakwani.

Kikosi cha Yanga; Diarra, Djuma/Moloko, Lomalisa/Farid, Bacca, Mwamnyeto, Job, Kisinda/Morrison, Sure Boy, Mayele, Mudathir/Mzize na Musonda/Aziz KI.

Kikosi cha USM Alger; Benbot, Radouani, Loucif, Alilet, Belaid, Chita, Bousseliou/Belkacemi, Merbah/ Meziane, Mahious, Merili na Orebonye