Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yaitumia salamu Simba ikiichapa Pamba Jiji

Muktasari:

  •  Katika mechi mbili dhidi ya Pamba Jiji FC msimu huu, Yanga imefunga mabao saba ambapo manne iliyapata katika mechi ya mzunguko wa kwanza na matatu imeyapata katika mzunguko wa pili.

Dar es Salaam. Yanga imejiweka katika hali nzuri kuelekea katika mechi ya watani wa jadi dhidi ya Simba, Machi 8, 2025 baada ya leo Februari 28, 2025 kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji FC katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mabao mawili ya Stephane Aziz Ki na moja la Chadrack Boka yameipa Yanga pointi tatu muhimu katika mechi hiyo ambayo yameifanya ifikishe pointi 58 ambazo zimezidi kuihakikishia kuwepo kileleni mwa msimamo wa ligi.

Boka ndiye aliyeanza kuipa Yanga uhakika wa ushindi katika mchezo huo baada ya kufunga bao kwa Mpira wa faulo ambao ulipita juu ya ukuta wa Pamba Jiji na kujaa wavuni.

Faulo ilipatikana baada ya Zabona Mayombya kumchezea ndivyo sivyo Mudathir Yahya. Bao hilo lilidumu hadi filimbi ya mapumziko ilipopulizwa na refa Nassoro Mwinchui.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya kumtoa Khalid Aucho na kumuingiza Stephane Aziz Ki.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa Yanga kwani Ki amefunga bao la pili katika dakika ya 75 akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi wa Maxi Nzengeli na akafunga lingine katika dakika ya 77 akimalizia kwa shuti la mguu wa kushoto pasi ya Duke Abuya.

Matokeo hayo yameifanya Yanga ifikishe mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza ambapo imepata ushindi mara kumi na kutoka sare moja tangu ilipopoteza mbele ya Tabora United kwa mabao 3-1, Novemba 7, mwaka jana.

Tukio ambalo limevutia wengi katika mchezo huo lilikuwa ni la kuingia kwa winga wa Yanga aliyesajiliwa katika dirisha dogo la usajili Jonathan Ikangalombo ambaye alichukua nafasi ya Clement Mzize katika dakika ya 69.

Umati wa mashabiki wa Yanga waliojitokeza katika Uwanja wa CCM Kirumba walishangilia kwa nguvu mabadiliko hayo ya kuingia kwa Ikangalombo ambaye jana ilikuwa mechi yake ya kwanza kuitumikia timu hiyo.

 Matokeo ya leo yameifanya Pamba Jiji kubakia katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi zake 22.

 Kipa Djigui Diarra kwa kutoruhusu bao leo, amefikisha mchezo wa 11 bila kuruhusu bao na hivyo kuwa katika nafasi ya pili katika chati ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao huku kinara akiwa ni Moussa Camara wa Simba ambaye amefanya hivyo katika mechi 15.