Pamba kuichorea Yanga msitari wa dabi

Muktasari:
- Timu hizo zinatarajiwa kukutana leo ikiwa ni kati ya mechi mbili za Ligi Kuu zinazopigwa leo Ijumaa, huku mshabiki wakitarajia kushuhudia pambano la kiufundi zaidi, Pamba ikitaka kulipa kisasi na kulinda heshima ikiwa nyumbani, lakini Yanga ikitaka kuendeleza ilipoishia kabla ya kukabiliana na Mnyama.
Dar es Salaam. Ligi Kuu Bara inaendelea tena leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja mbalimbali lakini macho yataelekezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati wenyeji Pamba Jiji FC watakapowakaribisha mabingwa watetezi Yanga saa 10:15 jioni, ikiwa ni mechi ya mwisho kabla Yanga haijajiandaa na mchezo wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.
Pamba inaingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2, mechi ya mwisho dhidi ya Singida Black Stars, huku kwa upande wa wapinzani wao Yanga, ikiwa na ari nzuri baada ya kuishushia kichapo cha fedheha Mashujaa mabao 5-0.
Timu zote zimekuwa na mwenendo mzuri katika michezo yao mitano ya mwisho ambapo Pamba imeshinda mitatu kati ya hiyo, ikitoka sare mmoja na kupoteza mmoja.
Kwa upande wa Yanga katika michezo yake mitano ya Ligi Kuu Bara iliyopita, imeshinda minne na kutoka sare mmoja, ambapo moja ya safu inayotishia wapinzani ni eneo la ushambuliaji lililofunga mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.
Yanga itaendelea kuwategemea washambuliaji nyota wa timu, Prince Dube na Clement Mzize ambao hadi sasa ndio vinara wa ufungaji baada ya kila mmoja wao kufunga mabao 10.
Dube ndiye nyota aliyechangia mabao mengi ya kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara hadi sasa kwani kati ya 55, yaliyofungwa na timu nzima, amehusika kwenye 17, baada ya kufunga 10 na kuchangia upatikanaji wa mengine saba kwa maana ya ‘Assisti’.
Kwa upande wa Pamba, itaendelea kutegemea ubora wa mshambuliaji nyota wa timu hiyo raia wa Kenya, Mathew Momanyi Tegisi ambaye hadi sasa amehusika katika mabao matano ya kikosi hicho, baada ya kufunga matatu na kuchangia mawili ‘Assisti’.
Momanyi ni kama ameendeleza pale alipoishia wakati akiwa na Shabana FC, kwani kabla ya kujiunga na Pamba alikuwa amefunga mabao matano kwao Kenya.
Hata hivyo, Pamba ina kazi ya kulipiza kisasi baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex kuchapwa mabao 4-0.
Mchezo huu ni wa raundi ya 22, ambapo kwa upande wa Yanga inayoongoza na pointi 55, imeshinda 18, sare mmoja na kuchapwa miwili, huku kwa upande wa Pamba Jiji, ikishinda mitano tu, sare saba na kupoteza tisa, ikiwa nafasi ya 12 na pointi 22.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema.
“Tunacheza na timu nzuri na yenye wachezaji bora hadi sasa, ni mchezo mgumu kama ilivyokuwa mingine iliyopita.”
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema licha ya ushindi mnono wa mabao 5-0, dhidi ya Mashujaa, ila wamesahau na kuweka nguvu kwenye mechi hii.