Yanga yageuka mbogo ikimjibu Mtendaji Bodi ya Ligi

Muktasari:
- Mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu baina ya Yanga na Simba imepangwa kuchezwa Juni 15, 2025.
Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Almas Kasongo kusema yaliyozungumzwa katika kikao kati yake na Yanga, klabu hiyo imeibuka na kukanusha yaliyosemwa na Kasongo.
Kasongo alisema kuwa Yanga imetoa masharti manne ambayo inataka yafanyiwe kazi ili icheze dhidi ya Simba ambayo ni kuvunjwa kwa kamati ya uendeshaji wa ligi, Bodi ya Ligi kuwa huru, Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu kujiuzulu na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kujiuzulu.
Ofisa Habari wa Yanga Ally Kamwe amesema klabu yao Iko ‘serious’ kwenye msimamo wao wa kutocheza mchezo dhidi ya Simba akisema Bodi ya Ligi Tanzania imepotosha juu ya matakwa yao manne.
Akizungumza jioni hii makao makuu ya Yanga Kamwe amesema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Almas Kasongo ameshindwa kufafanua vizuri matakwa yao manne kwamba yapo matakwa ya muda mfupi na muda mrefu.
Kamwe amesema matakwa ya muda mfupi ni pamoja na kuvunjwa kwa Kamati ya usimamizi ya Ligi kwa kile ilichodai imeshindwa kusimamia kwa weledi usimamizi wa Ligi kwa msimu wa 2024/25
Amesema takwa la pili la muda mfupi ambalo linakwenda sambamba ni kujiuzulu kwa Kasongo alipotosha Bodi wakati wa kuahirishwa kwa mchezo namba 184 uliopangwa kufanyika Machi 8,2025.
"Jambo lingine la muda mfupi ni kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, wote mnajua kumekuwa na vilio vingi juu ya maamuzi ya waamuzi, waamuzi wanafanya makosa na bado wanapewa mechi za kuamua,"amesema Kamwe.
"Kama hamfahamu hii Kamati ya waamuzi ipo chini ya Katibu Mkuu wa TFF kwa kuwa matatizo yamekuwa mengi Yanga tunasema na yeye atupishe,” amesema Kamwe.
Aidha Kamwe amesema takwa la kuunda Bodi huru ndio jambo la muda mrefu ambalo wamewaachia TFF na Bodi kulifanyia kazi ambapo endapo halitafanyiwa kazi kwa uzito wanaweza wasishiriki Ligi msimu ujao