Yanga, Simba kesho mziki uko hapa
Muktasari:
- Wababe wa Kariakoo kesho watashuka dimbani katika fainali ya Ngao ya Jamii ambapo kila mmoja anataka kuweka heshima.
Kesho Jumanne Septemba 16, 2025, utachezwa mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa msimu wa mashindano yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa msimu wa 2025-2026.
Tofauti na msimu uliopita ambapo Ngao ya Jamii ilishirikisha timu nne za Yanga, Azam, Simba na Coastal Union, safari hii ni timu mbili pekee, Yanga dhidi ya Simba.
Msimu uliopita timu hizo nne zilicheza kwa mtindo wa mtoano, ilianza nusu fainali Azam ikaifunga Coastal Union mabao 5-2, kisha Yanga ikaichapa Simba bao 1-0.
Simba ikaja kuifunga Coastal Union 1-0 katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu, huku fainali Yanga ikishinda kwa mabao 4-1 dhidi ya Azam na kubeba Ngao ya Jamii.
TFF limeeleza kuwa ratiba ya msimu huu imebana kutokana na mambo mbalimbali ya kimataifa na kitaifa. Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Fainali za CHAN 2024, mashindano ambayo yalianza Agosti 2, 2025 na kukamilika Agosti 30, 2025. Aidha, mwanzoni mwa mwezi Septemba, Taifa Stars imecheza michezo miwili muhimu ya mchujo wa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Congo na Niger.
Kwa kuzingatia mazingira haya, TFF limeona ni muhimu kupunguza idadi ya michezo ya Ngao ya Jamii ili kutoathiri ratiba ya klabu na timu ya taifa. Baada ya mchezo huo, klabu za Tanzania zitakabiliwa na mechi za awali za mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Simba na Yanga zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Azam na Singida Black Stars zikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Taarifa ya TFF iliyotolewa Agosti 20, 2025 na Ofisa Habari, Cliford Ndimbo, imefafanua hivi: "Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwataarifu wadau na mashabiki wa soka kuwa mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) itakayozindua msimu mpya wa mashindano itachezwa tarehe 16 Septemba 2025 jijini Dar es Salaam, ikiwakutanisha Yanga na Simba.
"Kwa mujibu wa marekebisho ya kanuni yaliyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake cha hivi karibuni, mfumo wa mashindano ya Ngao ya Jamii umebadilika. Endapo ratiba za mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) zitaingiliana na ratiba za ndani, Ngao ya Jamii itachezwa kwa mchezo mmoja tu wa fainali, badala ya mfumo wa awali uliokuwa na mechi tatu (nusu fainali mbili na fainali).
"Mabadiliko haya yamezingatia ukweli kwamba Tanzania ni mwenyeji wa Fainali za CHAN 2025, zinazochezwa kuanzia tarehe 2 Agosti hadi 30 Agosti 2025. Aidha, mwanzoni mwa Septemba, timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashiriki michezo miwili ya mchujo wa Kombe la Dunia. Baada ya Ngao ya Jamii, klabu zetu zitakuwa na majukumu ya kushiriki mechi za raundi ya awali ya mashindano ya CAF."
Ikumbukwe kwamba, mashindano ya Ngao ya Jamii yalianzishwa mwaka 2001, ikianza kwa mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga. Katika mchezo huo wa kwanza, Yanga iliibuka na ushindi kwa kuifunga Simba 2-1. Mabao ya Yanga yalifungwa na Edibily Lunyamila na Ally Yussuph ‘Tigana’, huku bao pekee la Simba likifungwa na Steven Mapunda ‘Garincha’.
Mashindano haya kuna kipindi hayakufanyika, ilikuwa mwaka 2004, 2006, 2007 na 2008. Yakarejea mwaka 2009 na tangu wakati huo, yameendelea kuwa kipimo cha kuashiria mwanzo wa msimu mpya, yakihusisha klabu ambazo zimefanya vizuri katika msimu uliopita.
Awali ilikuwa bingwa wa ligi anacheza na mshindi wa pili, lakini baadae na hadi sasa imekuwa bingwa wa ligi anacheza dhidi ya bingwa wa Kombe la FA. Ikitokea timu imeshinda mataji yote hayo, basi inacheza dhidi ya timu iliyomaliza nafasi ya pili ligi kuu.
Kwa mfumo wa timu nne, zinazoshiriki ni zile zenye tiketi ya kushiriki michuano ya CAF ambazo hupatikana kutokana na zilizomaliza nafasi tatu za juu kwenye msimamo na moja bingwa wa Kombe la FA kukamilisha idadi ya timu nne, lakini ikitokea bingwa wa ligi ndiye bingwa wa FA, basi timu zote nne za juu kwenye msimamo ndizo zitashiriki.
Ilianza hivyo mwaka 2023 wakati Simba inabeba Ngao ya Jamii, timu zilizoshiriki ni Yanga, Azam, Singida Fountain Gate na Simba. Mwaka 2024 ni Yanga, Azam, Simba na Coastal Union.
Wakati tunakwenda kushuhudia Ngao ya Jamii ikipigwa hapo kesho, rekodi zinaonyesha Simba na Yanga zimekutana mara tisa katika fainali ya Ngao ya Jamii, achana na ile ya mwaka jana zilipokutana hatua ya nusu fainali.
Katika fainali 20 za Ngao ya Jamii zilizochezwa kwa ujumla tangu 2001, wakongwe hao wamekutana mara tisa, Simba ikishinda tano na Yanga nne. Safari hii ngoja tuone nani atakuwa mbabe. Simba itaongeza wigo wa ushindi, au Yanga itaweka mzani sawa? Nyasi za Uwanja wa Benjamin Mkapa, zitaamua.
Mbali na hilo, Yanga inafukuzia mafanikio ya Simba katika Ngao ya Jamii tangu kuanzishwa kwake.
Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa na mafanikio katika mashindano ya Ngao ya Jamii, ikiwa imechukua taji hilo mara kumi, ikionyesha uwezo wake mkubwa na ushindani katika soka la Tanzania. Ushindi wake wa kwanza ulikuja mwaka 2002 ilipoifunga Yanga 4-1, na ushindi wake wa hivi karibuni ulikuwa mwaka 2023 iliposhinda dhidi ya Yanga kwa penalti 3-1 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.
Yanga katika kufukuzia mafanikio hayo, imeshinda Ngao ya Jamii mara nane. Ushindi wake wa kwanza ulikuwa mwaka 2001 ilipoifunga Simba 2-1. Ushindi wake wa hivi karibuni ulikuwa mwaka 2024 iliposhinda dhidi ya Azam kwa mabao 4-1.
Katika fainali hizo 20 za Ngao ya Jamii zilizopita, Simba imecheza 14, ikishinda 10 dhidi ya Yanga (5), Azam (2), Mtibwa Sugar (2) na Namungo (1). Pia imepoteza nne zote ni dhidi ya Yanga.
Kwa upande wa Yanga, imecheza fainali 15 za Ngao ya Jamii, imeshinda nane dhidi ya Simba (4) na Azam (4), huku ikipoteza saba dhidi ya Simba (5), Mtibwa Sugar (1) na Azam (1).
Mtibwa, Azam nao wamo
Kama inavyoonekana kwenye orodha ya washindi, Simba na Yanga ndiyo klabu zinazotawala katika mashindano haya. Ushindani wao umeleta burudani kubwa kwa mashabiki na kuimarisha soka la Tanzania.
Kwa upande mwingine, klabu ya Azam na Mtibwa Sugar nazo zimeweza kuonyesha ushindani kwa kushinda mara moja kila moja.
Mtibwa na Azam wakati zinabeba Ngao ya Jamii, zote ziliifunga Yanga. Ilianza Mtibwa mwaka 2009 iliposhinda 1-0, kisha Azam mwaka 2016 kwa penalti 4-1.
WASHINDI NGAO YA JAMII
2001 Yanga 2-1 Simba
2002 Simba 4-1 Yanga
2003 Simba 1-0 Mtibwa
2004 HAIKUFANYIKA
2005 Simba 2-0 Yanga
2006 HAIKUFANYIKA
2007 HAIKUFANYIKA
2008 HAIKUFANYIKA
2009 Mtibwa 1-0 Yanga
2010 Yanga 0-0 Simba (Penalti 3-1)
2011 Simba 2-0 Yanga
2012 Simba 3-2 Azam
2013 Yanga 1-0 Azam
2014 Yanga 3-0 Azam
2015 Yanga 0-0 Azam (Penalti 8-7)
2016 Azam 2-2 Yanga (Penalti 4-1)
2017 Simba 0-0 Yanga (Penalti 5-4)
2018 Simba 2-1 Mtibwa
2019 Simba 4-2 Azam
2020 Simba 2-0 Namungo
2021 Yanga 1-0 Simba
2022 Yanga 2-1 Simba
2023 Simba 0-0 Yanga (Penalti 3-1)
2024 Yanga 4-1 Azam