Waangola wa Simba wampa presha Ahmed Ally
Muktasari:
- Simba ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Zimbabwe katika raundi ya pili.
Dar es Salaam. Homa ya mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Luanda ya Angola, Jumapili ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam inaonekana kuanza kupanda baada ya Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kukiri kuwa wana mtihani mgumu mbele yao
Akizungumza katika ziara ya hamasa kuelekea mechi hiyo, Ahmed amesema Petro Atletico sio timu ya kubeza hivyo Wanasimba waipe sapoti timu yao ili iweze kupata ushindi.
"Tuendelee kuhamasishana ili Wanasimba wengi waje uwanjani Jumapili hii kutokana na umuhimu wa mchezo huu. Mpinzani wetu ni mkubwa kwelikweli na silaha yetu ni mashabiki, na tunajua nguvu yenu mkiujaza Uwanja wa Mkapa.
"Mkishakuja kwa wingi uwanjani tunamfanya vibaya Atlético Petróleos de Luanda na hilo halina mjadala.
“Kila Mwanasimba ni muhimu kununua tiketi na kuja uwanjani. Kama kuna mtu hajawahi kuja uwanjani basi huu ndio uwe mtoko wao wa kwanza. Jumapili Novemba 23 tuje uwanjani lakini tuhakikishe tumevaa jezi za msimu huu," amesema Ahmed Ally.
Ahmed amesema kuwa mchango wa mashabiki una nafasi kubwa ya kusaidia kuongeza hamasa kwa wachezaji na hivyo timu kufanya vizuri.
“Hamasa imezinduliwa rasmi hapa Zingiziwa. Nitumie nafasi hii kuwakaribisha uwanjani Jumapili, pamoja na ugumu wa mchezo huu lakini niwahakikishie kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu tutaondoka na ushindi.”
“Kuitakia mema Simba yako ni kuja uwanjani Jumapili kuishangilia timu yetu. Nunua tiketi ili uje kujumuika na Wanasimba wenzako, asibaki mtu nyumbani. Twendeni uwanjani kumpelekea moto Atlético Petróleos de Luanda.”
“Kila atakayekuja uwanjani Jumapili aje amevaa jezi nyekundu, na nyekundu ya msimu huu. Hiyo ndio itakuwa sare yetu ya siku hiyo," amesema Ahmed Alilyy