Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi ya Simba tishio kwa Waangola

Muktasari:

  • Simba na Petro Luanda zimepangwa katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ambalo pia linaundwa na timu za Esperance na Stade Malien.

Ni rasmi mchezo wa kwanza wa Simba kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu utachezwa Jumamosi, Novemba 22, 2025 kuanzia saa 1:00 usiku kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mchezo huo umepangwa kufanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambao Simba ndio klabu pekee ya Tanzania inaoutumia kwa mechi zake za nyumbani za mashindano hayo.

Ikumbukwe wawakilishi wengine wa Tanzania katika hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika, Yanga, Azam FC na Singida Black Stars wamepanga kutumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kitendo cha CAF kupanga mechi hiyo ya kwanza ya Simba ya hatua ya makundi kuchezwa kuanzia saa 1:00 usiku hapana shaka kinapaswa kupokelewa kwa nyuso za furaha na mashabiki wa Simba kwani inakumbushia rekodi tamu ambayo timu hiyo inayo kwa mechi za usiku za mashindano ya Klabu Afrika.

Historia inaonyesha mechi za usiku hasa za saa moja katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, zimekuwa na bahati kubwa kwa Simba kutokana na kupata ushindi mara nyingi zaidi kuliko kupoteza.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, Simba imecheza idadi ya mechi saba za usiku za mashindanio ya Klabu Afrika kwa miaka ya hivi karibuni katika uwanja huo ambapo imepata ushindi mara tano na kupoteza miwili tu.

Bahati ya Simba usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilianzia katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Msimu wa 2021/2022, Simba ikapata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya USGN ya Niger, katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu wa 2022/2023, Simba ilicheza mechi zote tatu za nyumbani za hatua ya makundi usiku kuanzia saa 1:00 usiku ambapo moja ilifungwa mabao 3-0 na Raja Casablanca ya Morocco na mbili ikashinda ambazo ni dhidi ya Vipers ua Uganda kwa bao 1-0 na dhidi ya Horoya ya Guinea ikapata ushindi wa mabao 7-0.

Katika msimu wa 2023/2024, Simba ilipangwa kucheza na Al Ahly kuanzia saa 1:00 usiku kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikapoteza kwa bao 1-0.

Kabla ya hapo, Simba katika msimu huohuo, iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy katika mchezo wa hatua ya makundi.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa wanajipanga kuhakikisha wanaanza vyema hatua ya makundi kwa kupata ushindi dhidi ya Petro Luanda.

"Macho yetu yote sasa ni mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi ya ligi mabingwa Afrika. Tumebakiwa na wiki moja pekee ya kufanya maandalizi ya ndani na nje ya Uwanja.

"Maandalizi ya Nje Uwanja ni pamoja kununua Tiketi, mapema kuanzia wiki Ijayo Jumatatu Insha Allah tiketi zitaanza kuuzwa na ombi letu ni Wana Simba wengi zaidi kuja Uwanjani siku ya mechi

"Tunataka kuutendea haki Uwanja wa Benjamini Mkapa," amesema Ahmed Ally.