Kalenda FIFA presha kwa Klabu
Muktasari:
- Stars ilikuwa icheze dhidi ya Algeria, Novemba 18 baada ya mechi dhidi ya Kuwaita lakini TFF ikaiondoa mechi hiyo.
Dar es Salaam. Mechi za kimataifa za kirafiki za timu za taifa zilizo chini ya kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) zinaweka mtegoni maandalizi ya klabu nne za Tanzania zinazoshiriki hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika msimu huu.
Klabu hizo nne ambazo ni Yanga na Simba zilizopo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC na Singida Black Stars zilizopo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Uwepo wa mechi zilizo kwenye kalenda ya FIFA kuanzia jana Novemba 12 hadi wiki ijayo Novemba 18, utazilazimisha klabu hizo kufanya maandalizi ya mechi zao za mwanzo za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika zikiwa na idadi isiyotosheleza ya wachezaji lakini hata kutopata mapumziko ya kutosha ya wachezaji kabla ya mechi hizo.
Ni tofauti ya siku tatu tu kutoka kumalizika kwa kalenda ya FIFA na mechi za kwanza za hatua ya makundi ya mashindano hayo ya klabu.
Dalili zinaonyesha kwamba wachezaji walio katika timu za taifa tofauti watajikuta wakifanya mazoezi ya pamoja na wengine waliobakia vikosini kwa muda usiozidi siku tano kutegemeana na ratiba ya mechi za mchezaji husika kwa timu yake ya taifa.
Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Novemba 21, 2025 Simba itaikaribisha Petro de Luanda ya Angola kisha Yanga ikikifuata Novemba 22 kwa kuwa mwenyeji wa AS FAR Rabat ya Morocco.
Azam wao wataanzia ugenini wakiwafuata Union Maniema ya DR Congo mchezo ulipangwa kuchezwa Novemba 23 wakati wenzao Singida nao wakiwa wageni wa CR Belouizdad ya Algeria Novemba 22.
Yanga ndio inaonekana kuwa na presha kubwa katika maandalizi yake kwa vile ina wachezaji 10 waliotwa katika timu mbalimbali za taifa.
Kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza dhidi ya Kuwait, Novemba 15 huko Misri, Yanga ina wachezaji watano ambao ni Bakari Mwamnyeto,Mohammed Hussein ‘Tshabalala, Mudathir Yahya,Ibrahim Abdula ‘Bacca’ na Dickson Job wakati wengine ni Moussa Bala Conte (Guinea),Lassine Kouma (CHAD),Prince Dube(Zimbabwe),Duke Abuya (Kenya) na kipa Djigui Diarra (Mali).
Nafuu inaonekana kuwa kwa wachezaji wa Taifa Stars ambao angalau watawahi kurudi nchini kwa vile timu hiyo itacheza mchezo mmoja tu ingawa timu nyingine za taifa nyingi zitakuwa na michezo miwili.
Afisa Habari wa Yanga Ally Kamwe ameliambia gazeti hili kuwa presha kubwa ipo kwa wachezaji hao wakati wa maandalizi ambapo tayari klabu yao imefanya mawasiliano na mataifa ya wachezaji hao kuangalia uwezekano wa kuruhusiwa kurudi nchini baada ya mechi za kwanza za timu zao za taifa kwa vile wengi ndio wanaunda kikosi cha kwanza.
“Tuko kwenye wakati mgumu lakini Yanga tuna mahusiano mazuri na mataifa ambayo wachezaji wetu wanakwenda kuyatumikia. Kawaida kwenye kalenda kama hii ya FIFA kunakuwa na mechi mbili lakini uongozi wetu umefanya mawasiliano ili wawaruhusu baada ya mechi ya kwanza.
“Kuomba ni hatua moja lakini bado hawajatujibu,. Tunaamini watatuelewa na kuwaruhusu kwa kuwa hizi ni mechi za kirafiki sio zile muhimu zaidi ambazo zinakuwa za kuwania kufuzu mashindano mbalimbali ya kimataifa,” alisema Kamwe.
Simba wao ina achezaji saba waliokwenda kujiunga na timu ya taifa wakiwemo watano wa Stars ambao ni Yakoub Suleiman, Shomari Kapombe, Wilson Nangu,Suleiman Mwalimu, Morrice Abraham na Naby Camara wa Guinea pia akiwepo Steven Mukwala wa Uganda.
Azam ina wachezaji wanne kwenye kikosi cha Stars ambao Zuberi Foba, Pascal Msindo, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Iddi Selemani.
Singida Black Stars ina wachezaji wawili pekee waliokwenda kujiunga na Stars ambao ni kipa Hussein Masalanga na kiungo Habib Idd na kipa Amas Obasogie aliye katika kikosi cha Nigeria lakini pia makocha wao Miguel Gamondi na msaidizi wake wa kwanza Mussa Ndaw wako na Stars iliyokwenda Misri kucheza dhidi ya Kuwait.
“Singida tuna wachezaji wawili tu ambao tutawakosa hivi karibuni ni Masalanga na Habib. Labda watu wengine muhimu ni makocha wetu Gamondi na wasaidizi wake ambao wamejiunga na Stars,” alisema ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza.
Presha ingekuwa kubwa kwa klabu hizo iwapo Taifa Stars ingecheza mechi mbili za kirafiki huko Misri lakini kwa lengo la kuzipa klabu zake fursa ya angalau kuwa na wachezaji wao kwa siku tano, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliamua Taifa Stars icheze mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Kuwait.
Stars ilikuwa icheze dhidi ya Algeria, Novemba 18 baada ya mechi dhidi ya Kuwaita lakini TFF ikaiondoa mechi hiyo.