Prime
Vurugu za Simba, Berkane adhabu hii hapa

Muktasari:
- Baada ya tukio kutokea taratibu zinazofuatwa ni pamoja na uchunguzi wa tukio, uwasilishaji wa ushahidi, na uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya CAF.
Zanzibar. Gumzo kubwa linaendelea kutawala mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kufuatia Simba kupoteza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco, lakini kilichotokea mara baada ya mchezo huo kwenye Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar ndicho kinachotikisa zaidi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya watu waliovaa jezi za Simba walinaswa kwa video wakiwa katika chumba cha kubadilishia nguo cha waamuzi, wakirekodi tukio na kurushiana maneno na mwamuzi aliyekuwa amechezesha fainali hiyo.
Video hiyo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku ikionekana wazi kuwa waamuzi nao walikuwa wakirekodi tukio hilo kwa simu zao.
Hali hiyo imeibua hofu kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka, huku ikielezwa kuwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linaweza kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika kwa mujibu wa kanuni zake.
Kwa mujibu wa Kanuni za Maadili na Nidhamu za CAF, kifungu cha 82 kinachoeleza kuhusu vitendo vya fujo, vitisho au hatari kwa usalama wa waamuzi, wachezaji au mashabiki, mtu yeyote atakayepatikana na hatia anaweza kuadhibiwa kwa faini au kufungiwa kushiriki shughuli za soka kwa kipindi maalumu.
Aidha, kifungu cha 123 nacho kinabainisha kuwa iwapo kiongozi, mchezaji au hata shabiki atahusika kwenye fujo ndani au nje ya uwanja, hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufungiwa au kutozwa faini.
Kwa sasa, kinachosubiriwa ni uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya CAF ambayo itapitia ushahidi wa video na taarifa kutoka kwa waamuzi kabla ya kutoa hukumu dhidi ya wahusika wa tukio hilo.
Wachambuzi wa masuala ya michezo wameonya kuwa matukio kama hayo yanaweza kuiumiza Simba si tu kwa adhabu za kifedha bali hata kwa sifa yake kimataifa, hasa baada ya kufikia hatua ya fainali katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Fainali hiyo ilimalizika kwa Berkane kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa mara ya tatu katika historia yake.