Vigogo kuvaana Ligi ya Mabingwa Ulaya
Monaco, Ufaransa. Droo ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imepangwa na sasa vigogo wakubwa wamepangwa kukutana wenyewe huku mechi kati ya Arsenal na Bayern Munich, Man City dhidi ya Real Madrid zikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki.
PSG ambao walikuwa mabingwa watetezi watalazimika kupambana ili kutetea ubingwa wao kutokana na vigogo ambao wamepangwa kukutana nao kwenye michuano hiyo ya hatua ya ligi inayotarajiwa kuanza kupigwa Septemba 16-19 kwa mchezo wa kwanza.
Hata hivyo, hatua ya ligi ya michuano hiyo itakamilika Januari 28 ambapo vigogo watakaoingia hatua inayofuata watakuwa wameshafahamika.
Liverpool yapewa Madrid
Liverpool imepangwa na vigogo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya ligi baada ya kupangiwa Real Madrid pamoja na Atletico Madrid.
Msimu uliopita timu zote zilishindwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na sasa zimepangwa pamoja ambapo Liverpool itawalazimu kwenda nchini Hispania kuvaana na mabingwa hao wa kihistoria.
Hata hivyo, itawalazimu Liverpool kurudi tena nchini Hispania kwa kuwa imepangwa pia kuvaana na Atletico Madrid moja ya timu ambayo imekuwa haitabiriki kwenye michuano hii.
Timu nyingine ambazo zitavaana na Liverpool ni Inter Milan ambayo itakwenda Anfield, Eintracht Frankfurt, PSV Eindhoven, Marseille, Qarabag na
Galatasaray.
Mfumo wa michuano hii hatua ya ligi ni mchezo mmoja, hivyo baada ya mechi ya Madrid na Liverpool kutakuwa hakuna mchezo mwingine wa marudio labda kama watakutana kwenye hatua nyingine.
Bayern wataivaa Arsenal
Klabu ya Bayern Munich italazimika kwenda nchini England mara moja pamoja kwamba kwenye ligi yake kuna timu mbili kutoka nchini humo.
Bayern watavaana na Chelsea wakiwa nyumbani, lakini watalazimika kwenda Emirates kuivaa Arsenal, ambapo timu nyingine ambazo itavaana nazo ni Mabingwa watetezi PSG ambao Club Burgge, Sporting CP, PSV, Union SG pamoja na Pafos, mechi nne watacheza nyumbani na nne ugenini.
Man City mambo magumu
wakiwa hawakufanya vizuri msimu uliopita Man City kwenye mechi zao nane watavaana na vigogo Real Madrid ikiwa ni mara ya tano wanakutana kwenye michuano ya Uefa tangu mwaka 2022.
Man City watakwenda Hispania kuwafuata Madrid, lakini watabaki nyumbani kuvaana na
Borussia Dortmund, watawasubiri Bayer Leverkusen na kwenda Hispania kuwavaa Villarreal.
Timu nyingine ambazo zitavaana na Man City ni Napoli mabingwa watetezi wa Italia, Bodo/Glimt Galatasaray na Monaco.
Chelsea kuivaa Barca na Bayern
Klabu ya Chelsea ambao ni mabingwa wa Klabu Bingwa ya Dunia imepewa timu kigogo ambapo itavaana na Barcelona nyumbani, itasafiri kwenda Ujerumani kuvaana na Bayern Munich ikiwa ndiyo michezo inayoonekana kuwa kigogo zaidi kwao.
Mbali na mechi hizo, pia Chelsea itavaana na Benfica nyumbani, Atalanta ugenini, Ajax nyumbani na itasafiri kwenda Italia kupambana na Napoli kabla hajamaliza mechi zake dhidi ya Pafos nyumbani na Qarabag ugenini.
Arsenal uso kwa uso na Bayern
Arsenal imekuwa na bahati mbaya kila inapokutana na Bayern Munich na sasa imepangwa tena kuvaana nayo ambapo itawasubiri kwenye Uwanja wa Emirates na huu utakuwa mchezo wao wa 15 wanakutana kwenye michuano hiyo.
Mbali ya Bayern, Arsenal ambayo msimu uliopita ilitolewa hatua ya nusu fainali itavaana pia na Inter Milan ambayo ilifika fainali msimu uliopita na kupoteza kwa PSG, lakini pia itakuwa nyumbani kuisubiri Atletico Madrid.
Timu nyingine ambazo zitavaana na Arsenal ni Club Brugge, Olympiacos, Slavia Prague timu ngeni ya Kairat Almaty pamoja na Athletic Bilbao.
Spurs kuwafuata mabingwa
Pamoja na kuanza vyema kwenye Ligi Kuu England, Tottenham Hotspur kwenye michezo yake itawalazimu kuwafuata mabingwa watetezi PSG nchini Ufaransa, lakini pia wakitakiwa kubaki nyumbani kuvaana na vigogo Borussia Dortmund.
Timu nyingine ambazo zitavaana na Spurs kwenye mtindo wa ligi ni Villarreal, Eintracht Frankfurt, Slavia Prague, Bodo Glimt, Copenhagen, pamoja na Monaco ya Ufaransa.
Newcastle uso kwa uso na Barcelona
wakati kukiwa na michezo kadhaa ya kuvutia kwenye michuano hii ya msimu huu, mechi nyingine ambayo mashabiki wanaisubiri kwa hamu ni ile ya Barcelona ambao watalazimika kusafiri kwenye England kuvaana na Newcastle United ambayo haipewi nafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa msimu huu.
Mechi nyingine za Newcastle ni dhidi ya PSG, Benfica, Bayern Leverkusen, PSV, Marseille, Athletic Club na Union SG.