Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usiku wa Ulaya na vita ya kufuzu Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

  • Droo ya hatua ya mchujo itafanyika Ijumaa, Januari 30, ikihusisha timu zitakazomaliza nafasi ya tisa hadi ya 24. Michezo ya mchujo itafanyika Februari, kabla ya hatua ya 16 bora kuanza rasmi.

Mzunguko wa nane na wa mwisho wa hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya unatarajiwa kutoa burudani ya kipekee, huku timu 17 zikipambana kuwania nafasi chache zilizosalia za kufuzu hatua ya mtoano.

Hadi kufikia sasa, timu 15 tayari zimefuzu, huku Arsenal na Bayern Munich zikiwa pekee zilizo na uhakika wa kutinga hatua ya 16 bora.

Baadhi ya wachezaji wa Barcelona wakishangilia ushindi wa 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania 'La Liga' dhidi ya Oviedo uliopigwa Jumapili, Januari 25, 2026. Picha na Mtandao


Barcelona vs Copenhagen

Barcelona wanaendeleza rekodi ya kufunga mabao karibu kila mechi, wakiwa hawajamaliza mechi bila bao katika michezo 42 ya Ulaya. Copenhagen, licha ya kuwa na historia mbaya dhidi ya timu za Hispania, wamekuwa imara katika mechi tatu zilizopita ambapo wameshinda mbili na kutoa sare mara moja huku wakishika nafasi ya 26 kwenye msimamo wa ligi kwa pointi nane.

Kwa upande wa Barcelona, wao wanahitaji ushindi ili waweze kujihakikishia nafasi ya kupenya katika hatua ya 16 bora bila kucheza mechi za mchujo, kwani inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 13 sawa na Chelsea iliyopo nafasi ya nane, Newcastle na PSG ambazo zimezidiana kwa tofauti ya mabao.

Kiungo wa Chelsea, Moisés Caicedo (wa kwanza mbele) akishangilia bao alilofunga katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Januari 21, 2026 dhidi ya Pafos. Picha na Mtandao


Napoli vs Chelsea

Napoli wana rekodi nzuri nyumbani dhidi ya timu za England. Chelsea, licha ya rekodi mbaya nchini Italia, wamekuwa na mwendelezo mzuri barani Ulaya na hawajawahi kucheza mechi bila kufungana katika michezo 55 ya mwisho. Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Diego Maradona, utakuwa mkali na wa aina yake kwani Chelsea itakuwa inapambana kubakia kwenye nafasi nane za juu huku Napoli nao wakiwa wanahitaji ushindi kuhakikisha wanabaki kwenye hatua za mchujo wa kutinga 16 bora.

Mshambuliaji wa Newcastle, Harvey Barnes akishangilia moja ya bao katika ushindi wa 3-0 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSV. Picha na Mtandao


PSG vs Newcastle

Hii itakuwa ni vita ya kubakia nafasi nane za juu kwenye msimamo wa ligi ambapo PSG inashika nafasi ya sita kwa pointi 13 sawa na Newcastle iliyopo nafasi ya saba huku zikitofautiana mabao ya kufungwa na kufunga. PSG wamekuwa wakifunga mabao mengi kwenye Uwanja wa nyumbani wakiwa wameshapachika mabao 20 hadi sasa. Kwa upande wa Newcastle wanamtegemea Anthony Gordon, ambaye amekuwa mfungaji wao bora msimu huu barani Ulaya akiwa tayari ameshapachika mabao sita nyuma ya Harry Kane mwenye saba na Kylian Mbappé anayeongoza akiwa na mabao 11.

Baadhi ya wachezaji wa Dortmund wakishangilia ushindi wa mabao 2-0 walioupata Jumapili, Januari 25, 2026 katika mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ dhidi ya Union Berlin. Picha na Mtandao


Borussia Dortmund vs Inter Milan

Dortmund wanatafuta ushindi wao wa 100 katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wakiwa na rekodi bora nyumbani, watawakabili Inter walio katika wakati mgumu baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo, jambo ambalo halijawahi kutokea kwao hapo awali. Timu zote mbili zinanafasi ya kupenya katika nafasi nane za juu iwapo mmoja wao ataibuka na ushindi. Inter yenye pointi 12 katika nafasi ya 14 inaweza kufikisha pointi 15 wakati Dortimund yenye pointi 11 nayo inaweza kufikisha 14 iwapo itaondoka na ushindi. Hata hivyo, hatma ya timu hizo kupenya katika nafasi nane za juu itategemeana na timu zilizopo juu yao iwapo kama zitafanya vibaya katika mechi zao za mwisho.

Mshambuliaji wa Madrid, Kylian Mbappé, akiwa na wachezaji wengine wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 2-0 walioupata kwenye mchezo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ Jumamosi, Januari 24, 2026 dhidi ya Villarreal. Picha na Mtandao


Benfica vs Real Madrid

Real Madrid wanaingia wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya timu za Ureno. Kylian Mbappé tayari ameweka rekodi ya mabao katika hatua ya ligi akiwa ameshapachika 11 katika mechi sita alizocheza hadi sasa. Kwa upande wa Benfica ni kama tayari wameumaliza mwendo msimu huu wakiwa na jumla ya pointi sita walizokusanya katika mechi saba ambazo wameshinda mbili na kupoteza tano.

Baadhi ya wachezaji wa Tottenham wakishangilia moja ya bao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika Januari 20, 2026. Spurs ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Dortmund. Picha na Mtandao


Frankfurt vs Tottenham

Tottenham wanaingia wakiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Frankfurt, wakiwatoa katika michuano ya Europa League msimu uliopita. Spurs wamekuwa imara katika safu yao ya ulinzi, wakizuia nyavu zao kutikiswa mara nne katika mechi tano zilizopita, huku Frankfurt wakikosa ushindi katika michezo sita mfululizo. Katika mchezo huu Frankfurt itaingia kukamilisha ratiba huku Spurs ikitafuta ushindi wa kuhakikisha inamaliza nafasi nane za juu.

Kiungo wa Liverpool, Dominik Szoboszlai (katikati), Milos Kerkez (kulia) na Ryan Gravenberch (kushoto) wakishangilia moja ya bao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille iliyomalizika kwa Majogoo wa Anfield kuibuka na ushindi wa 0-3. Picha na Mtandao


Liverpool vs Qarabağ

Liverpool wamekuwa wakitisha Anfield, licha ya kupoteza mara ya mwisho nyumbani. Qarabağ wana uwezo wa kushambulia na wamekuwa wakifunga mabao mengi, lakini historia iko dhidi yao wanapokutana na timu za England. Katika mchezo huu Majogoo wa Anfield wanahitaji ushindi kuhakikisha wanabakia nafasi nane za juu wakiwa tayari wameshakusanya pointi 15 katika nafasi ya nne.

Baadhi ya wachezaji wa Juventus wakishangilia ushindi wa mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Italia ‘Seria A’ dhidi ya Napol iliyopigwa Jumapili, Januari 25, 2026. Picha na Mtandao


Monaco vs Juventus

Juventus wanaingia wakiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Monaco, baada ya kuwatoa mara zote walipokutana katika hatua ya mtoano. Hata hivyo, Monaco wana rekodi nzuri nyumbani na hawajafungwa bao katika mechi zao mbili za mwisho za nyumbani za Ligi ya Mabingwa. Katika mchezo huu macho yatakuwa kwa Paul Pogba anayekutana na klabu yake ya zamani.

Baadhi ya wachezaji wa Atletico Madrid wakishangilia ushindi wa 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ uliopigwa Jumapili, Januari 25, 2026 dhidi ya Mallorca. Picha na Mtandao


Atlético Madrid vs Bodø/Glimt

Atlético wana rekodi nzuri dhidi ya timu za Norway, huku wakishinda mechi zote sita walizocheza. Bodø/Glimt nao wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao ambapo wameshapachika mabao 12 hadi sasa huku wakiwa wametoka kuandika historia baada ya kuifunga Man City wiki iliyopita. Kwa upande wa Atletico wanapambania kukwea katika nafasi nane za juu huku Bodø/Glimt wakipambania nafasi ya kucheza mechi za mchujo ambayo inaonekana kuwa ngumu kwao.

Mshambuliaji wa Man City, Antoine Semenyo (Kushoto), mwingine ni Omar Marmoush wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 2-0 walioupata Jumamosi, Januari 24, 2026 katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Wolves. Picha na Mtandao


Manchester City vs Galatasaray

City wanatafuta kuepuka kupoteza mechi mbili mfululizo nyumbani, jambo ambalo halijatokea kwa muda mrefu. Vijana wa Guardiola wanahitaji ushindi ili kujaribu kupenya katika nafasi nane za juu huku wakiziombea mabaya Sporting, Barcelona, Chelsea, Newcastle na PSG ambazo zinatofauti nzuri ya mabao dhidi yao.

Beki wa Ajax, Aaron Bouwman akijaribu kumtoka mchezaji wa Volendam katika mchezo wa Ligi Kuu Uhoranzi ‘Eredivisie’ uliopigwa Jumamosi, Januari 24, 2026. Picha na Mtandao


Ajax vs Olympiacos

Ajax na Olympiacos zinaingia uwanjani zikiwa na rekodi inayolingana, kila moja ikishinda mechi mbili kati ya sita walizokutana kwenye michuano ya Ulaya. Ajax ina rekodi nzuri dhidi ya timu za Ugiriki, lakini imekuwa ikianza mechi zake kwa kuruhusu bao la kwanza. Olympiacos nao wanatafuta ushindi wa pili mfululizo ugenini, jambo ambalo hawajawahi kulifanya mara nyingi kwenye mashindano haya. Ajax imekusanya jumla ya pointi sita ikishika nafasi ya 32 wakati Olympiacos wakiwa nafasi ya 24 kwa jumla ya pointi nane.

Baadhi ya wachezaji wa Arsenal wakiteta jambo baada ya kichapo cha mabao 2-3 dhidi ya Man United katika mechi ya Ligi Kuu England 'EPL' iliyopigwa Jumapili, Januari 25, 2025. Picha na Mtandao


Arsenal vs Kairat Almaty

Arsenal wamekuwa moto wa kuotea mbali. Wameshinda mechi zote saba walizocheza hadi sasa na hawajawahi kufungwa katika mechi tano zilizopita. Kikosi hicho cha London kimekuwa kikifunga mabao matatu au zaidi mara kwa mara, huku Kairat Almaty wakihangaika bila ushindi katika michezo yao 10 ya mwisho ya mashindano ya Ulaya. Timu zote zitakuwa hazina deni kwani Kairat Almaty tayari imeshaaga mashindano wakati Arsenal imeshafuzu hatua ya 16 bora. Hata hivyo, kikosi cha Mikel Arteta kitahakikisha kinalinda rekodi yake na kuweka historia ya kushinda mechi saba za hatua ya ligi.

Baadhi ya wachezaji wa Bayern wakishangilia bao walilopata katika mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ uliomalizika kwa kufungwa mabao 1-2 dhidi ya Augsburg, Januari 24, 2026. Picha na Mtandao.


PSV Eindhoven Vs Bayern München

Bayern München wanaingia katika mchezo huu wakiwa na rekodi bora dhidi ya PSV Eindhoven, baada ya kushinda mechi sita kati ya nane walizokutana kwenye mashindano ya UEFA. Katika michezo yao ya karibuni kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2016/17, Bayern walionyesha ubabe kwa ushindi wa mabao 4-1 nyumbani na 2-1 ugenini nchini Uholanzi.

Baadhi ya wachezaji wa PSV wakishangilia moja ya bao katika sare ya 2-2 walioipata Jumamosi, Januari 24, 2026 katika Ligi Kuu Uhoranzi ‘Eredivisie’ dhidi ya NAC. Picha na Mtandao

Kwa upande wa PSV, hali si shwari. Wameshindwa kupata ushindi katika mechi zao tano za mwisho dhidi ya timu za Ujerumani, huku wakishinda michezo miwili tu kati ya tisa ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa kwa ujumla. Hali hiyo inaongeza presha kwao wanapokutana na miamba hiyo ya Ujerumani.

Bayern, licha ya kupoteza 3-0 dhidi ya Feyenoord katika mechi yao ya mwisho dhidi ya timu ya Uholanzi msimu uliopita, bado wana rekodi imara wakikabiliana na vilabu vya nchi hiyo, wakipoteza mechi tatu kati ya 19. Kwa sasa, wamekuwa imara katika hatua ya ligi, wakishinda mechi 10 kati ya 12 walizocheza.

Baadhi ya wachezaji wa Athletic Club wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 2-3 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atalanta. Picha na Mtandao


Athletic Club vs Sporting CP

Athletic Club wana nguvu kubwa nyumbani, wakishinda mechi saba kati ya 10 za mwisho Ulaya. Sporting CP kwa upande wao hawajawahi kushinda ugenini dhidi ya timu za Hispania. Gorka Guruzeta wa Athletic Club na Luis Suárez wa Sporting CP wanatarajiwa kuwa silaha muhimu kwa timu zao kutokana na mchango mkubwa walioutoa hadi sasa. Sporting CP ipo kwenye nafasi nzuri ya kuendelea na mashindano wakati Athletic Club watakuwa wanapambana kuhakikisha wanabaki kucheza mechi za mtoano.

Washambuliaji wa Villarreal wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 3-1 walioupata dhidi ya Alaves katika Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’. Picha na Mtandao


Leverkusen vs Villarreal

Villarreal hawajawahi kufungwa na Leverkusen katika mechi zao nne zilizopita, lakini wanakuja wakiwa na rekodi mbaya ya michezo 10 bila ushindi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hadi sasa Manyambizi hao wa njano kutokea Hispania hawajapata ushindi wowote, wakipoteza mechi sita na kutoa sare mara moja huku wakishika nafasi ya 35 kwenye msimamo wa ligi sawa na Kairat Almaty ambayo inabuluza mkia kwa tofauti ya mabao. Leverkusen, licha ya kuwa na rekodi nzuri nyumbani, hawajashinda mechi nne mfululizo kabla ya pambano hili.

Mshambuliaji mpya wa Olympique de Marseille ya Ufaransa ambaye ametua kwa mkopo kutokea Arsenal, Ethan Nwaneri akimtoka beki wa Lens katika mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa ‘League One’ uliomalizika kwa Marseille kupata ushindi wa mabao 3-1 Jumamosi, Januari 24, 2026. Picha na Mtandao


Club Brugge vs Marseille

Brugge wana rekodi nzuri wanapocheza nyumbani dhidi ya timu za Ufaransa. Marseille kwa upande wao hawajapoteza dhidi ya timu za Ubelgiji katika mechi saba zilizopita na wanatafuta ushindi wa pili mfululizo ugenini. Katika mchezo huu timu zote mbili zitakuwa zikitafuta ushindi kuhakikisha zinapata nafasi ya kucheza hatua ya mchujo wa kuingia 16 bora. Brugge wapo kwenye hali ngumu ya kucheza mtoano, imekusanya jumla ya pointi saba tu katika mechi saba ilizocheza wakati wapinzani wao Marseille wakiwa na pointi tisa katika nafasi ya 19.

Droo ya hatua ya mchujo itafanyika Ijumaa, Januari 30, ikihusisha timu zitakazomaliza nafasi ya tisa hadi ya 24. Michezo ya mchujo itafanyika Februari, kabla ya hatua ya 16 bora kuanza rasmi.