UEFA kubadili mfumo wa Ligi ya Mabingwa msimu ujao

Muktasari:
- Kuanzia msimu ujao timu iliyomaliza katika nafasi za juu kwenye hatua ya ligi itahakikishiwa kucheza mchezo wa pili nyumbani katika hatua zote za mtoano kuanzia 16 bora hadi nusu fainali.
Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) limepanga kufanya mabadiliko kwenye mfumo wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia msimu ujao, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha timu zilizofanya vizuri hatua ya makundi zinapata faida ya kucheza mechi za marudiano nyumbani kwenye hatua za mtoano.
Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Mashindano ya Klabu ya UEFA huku ikilenga kuondoa malalamiko yaliyotokea msimu huu baada ya Arsenal na Barcelona kutolewa katika hatua ya nusu fainali licha ya kumaliza nafasi za juu kwenye jedwali la Ligi ya Mabingwa.
Katika mfumo wa msimu wa 2024/25, ambao ni wa kwanza kwa mashindano hayo kushirikisha timu 36 katika hatua ya ligi, vilabu vinavyomaliza nafasi nane za juu hupewa faida ya kucheza mchezo wa marudiano nyumbani katika hatua ya 16 bora.
Hata hivyo, hatua ya robo fainali na nusu fainali zimekuwa zikiamuliwa kwenye droo, jambo lililopunguza uzito wa nafasi za juu kwenye msimamo.
Katika nusu fainali ya msimu huu, Paris Saint-Germain (PSG) iliyomaliza katika nafasi ya 15 na Inter Milan nafasi ya nne, zote zilipewa faida ya kucheza mechi za pili nyumbani, huku wapinzani wao Arsenal waliyomaliza nafasi ya tatu na Barcelona nafasi ya pili wakilazimika kucheza marudiano ugenini.
PSG ilipata ushindi wa jumla ya mabao 3-1 kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kutoka kushinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Arsenal huku Inter Milan pia ikipenya kucheza fainali baada ya kuifunga Barcelona katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Giuseppe Meazza.
Kimsingi, timu ya kwanza hadi ya nane ndiyo zitapewa faida ya kuanzia ugenini katika hatua za mtoano wakati zile zitakazomaliza kuanzia nafasi ya 9 hadi 24, zitacheza mechi ya pili ya mtoano nyumbani hadi nusu fainali.
Kwa mfano, Liverpool na Barcelona walimaliza nafasi ya kwanza na ya pili, hivyo kwa kanuni hiyo mpya, wangekuwa na faida ya kucheza marudiano nyumbani katika kila hatua waliyopitia.
Kwa mujibu wa mabadiliko mapya, kuanzia msimu ujao timu iliyomaliza katika nafasi za juu zaidi kwenye hatua ya ligi itahakikishiwa kucheza mchezo wa pili nyumbani katika hatua zote za mtoano kuanzia 16 bora hadi nusu fainali. Lengo ni kuongeza ushindani wa kumaliza nafasi za juu zaidi.
Mabadiliko hayo bado yanahitaji kupitishwa rasmi na Kamati ya Utendaji ya UEFA. Ingawa kanuni za msimu wa 2025/26 tayari zimeshapitishwa, mabadiliko hayo yanaweza kufanywa iwapo Kamati Tendaji itayapitisha. Kamati hiyo imepangwa kukaa Septemba kabla ya droo ya hatua ya ligi kupangwa Agosti 28 ili kutoa uamuzi wa mwisho.
Kulikuwa na mjadala pia kuhusu iwapo timu iliyomaliza nafasi za juu iwe na chaguo la kuchagua icheze wapi mchezo wa pili, nyumbani au ugenini, lakini pendekezo hilo halikuungwa mkono.
Badala yake, UEFA imeamua kuwa utaratibu wa timu iliyomaliza katika nafasi za juu kucheza mechi ya pili nyumbani utekelezwe moja kwa moja bila chaguo.
Mabadiliko haya pia yanatarajiwa kuhamishiwa kwenye mashindano mengine ya UEFA, ikiwemo Ligi ya Europa na Europa Conference League, ili kuwepo na uwiano sawa katika mashindano yote.
Hata hivyo, UEFA haijafanya mabadiliko yoyote mengine kwenye kanuni, ikiwemo uvumi wa kuondoa muda wa ziada kabla ya changamoto za mikwaju ya penalti na kuzuia timu kutoka nchi moja kukutana katika raundi ya mtoano.