Tshabalala rasmi atua Yanga, vita iko hapa
Muktasari:
- Tshabalala kwa sasa yupo katika kikosi cha timu ya Taifa ambacho kinashiriki Fainali za CHAN 2024 na alifunga bao katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Burkina.
Dar es Salaam. Hatimaye yametimia, baada ya Yanga kumtambulisha rasmi beki wa kushoto Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kama mchezaji wao mpya leo Jumatano, Agosti 6, 2025.
Iliripotiwa mapema kuwa baada ya Tshabalala kutangaza kuachana na Simba, beki huyo alishasaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga na usiku wa leo klabu hiyo imethibitisha rasmi.
Ni mkataba ambao utashuhudia Tshabalala akipokea kiasi cha zaidi ya Sh400 milioni kama fungu la usajili na pia atalipwa mshahara wa zaidi ya Sh20 milioni kwa mwezi na waajiri wake hao wapya.
Tshabalala anajiunga na Yanga baada ya kuitumikia Simba kwa miaka 11 tangu alipojiunga nayo 2014 akitokea Kagera Sugar.
Katika miaka yake 11 ambayo ameitumikia Simba, ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu, mataji matatu ya Kombe la Shirikisho la CRDB, mataji matano ya Ngao ya Jamii, matatu ya Mapinduzi na moja la Muungano.
Mafanikio ya juu zaidi katika soka la Afrika ambayo Tshabalala ameyapata ni kufika hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika katika msimu wa 2024/2025 ingawa pia timu hiyo imewahi kuishia hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika mara sita tofauti.
Beki huyo wa kushoto kuanzia 2017 hadi 2024 alikuwa nahodha msaidizi wa Simba na baada ya hapo alikuwa nahodha mkuu hadi alipoachana na timu hiyo.
Mbali na Simba na Kagera Sugar, Tshabalala pia amewahi kuitumikia Azam FC hasa kikosi chao cha vijana ambacho kilimuibua kutoka mtaani kwake Magomeni Kagera.
Ndani ya Yanga, Tshabalala anakabiliwa na ushindani wa namba kutoka kwa mabeki Chadrack Boka na Clement Kibabage ambao msimu uliopita walikuwa wakicheza kwa kupishana kwenye nafasi hiyo.
Ukiondoa Kibabage na Boka, wachezaji wengine wa Yanga ambao wanamudu kucheza nafasi ya beki wa kushoto ni Kibwana Shomari na Israel Mwenda.
Tshabalala anakuwa mchezaji nane kujiunga na Yanga katika dirisha hili la usajili akiungana na Offen Chikola, Abdulnassir Casemiro, Andy Boyeli, Lassine Kouma, Moussa Balla Conte, Celestin Ecua na Abubakar Ninju.