Simba yamnasa mrithi Tshabalala, apewa mitatu
Muktasari:
- Tshabalala ameitumikia Simba kwa miaka 11 lakini kwa sasa ameachana nayo baada ya mkataba wake kumalizika.
Dar es Salaam. Simba imemtambulisha rasmi beki wa kushoto Anthony Mligo kama mchezaji wake mpya akitokea Namungo FC aliyoitumikia msimu uliopita.
Mligo anajiunga na Simba kama mchezaji anayetegemewa kuziba nafasi iliyoachwa na Mohamed Hussein na Valentine Nouma.
“Karibu Simba SC, Anthony Mligo,” imeandika Simba katika kurasa zake za mitandao ya kijamii ikimkaribisha beki huyo.
Mligo amesajiliwa kutokana na mapendekezo ya Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ambaye alimhitaji kama mchezaji mzawa wa kucheza nafasi hiyo baada ya kushindwa kumbakisha Tshabalala.
Mapema jana, Mligo aliaga rasmi Namungo FC, kitendo ambacho kilitafsiriwa kama hatua muhimu katika kukamilisha usajili wake ndani ya Simba.
“Kwanza kabisa natoa shukrani zangu za dhati kwa wachezaji wenzangu kwa ushirikiano mzuri ndani pamoja na nje ya Uwanja tulikuwa pamoja na kupambana kwa HALI na MALI katika kila nyakati furaha na huzuni tulivuka pamoja tukiwa IMARA!!
“Napenda kulishukuru benchi la ufundi/ Viongozi wa team Mashabiki na wapenzi wa NAMUNGO FC kwa kuwa pamoja ndani ya mwaka mmoja tukiipambania nembo ya team pamoja na malengo ya team iliyojiwekea katika msimu mzima.
“Inaniwia ugumu kuiaga familia niliyoishi nayo vizuri kwa upendo na amani wakati wote, Lakini sina jinsi kwenda kupata changamoto sehemu nyingine naamini tutakutana wakati mwingine.
“Nawatakia kila lenye kheri katika msimu ujao 2025-2026, SOUTHERN KILLERS,” ameandika Mligo.
Mligo anakuwa mchezaji wa tatu mzawa kusajiliwa na Simba katika dirisha linaloendelea la usajili akifuata baada ya Morice Abraham na Daud Semfuko