Tshabalala awapoza Simba kipigo cha Yanga
Muktasari:
- Mara ya mwisho kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ni msimu wa 2020/2021.
Muda mfupi baada ya Simba kupoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Yanga na kukosa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, beki na nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema matokeo hayo hayapaswi kuwakatisha tamaa.
Tshabalala amesema kuwa wanapaswa kujipanga zaidi ili wafanye vizuri siku za usoni huku akiwashukuru wadau mbalimbali wa timu hiyo.
“Kwanza, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu wa rehema kwa kutuwezesha kuanza ligi na kumaliza salama. Pili, uongozi chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji na makamu wake Murtaza Mangungu, benchi la ufundi, menejimenti, wanachama na mashabiki wote kwa kuwa bega kwa bega nasi mpaka mwisho wa msimu.
“Kwa mashabiki wetu, sijui nitumie maneno gani kuelezea shukrani zangu za dhati kwenu kwa mapenzi yenu makubwa kwetu.
“Hakika tuna deni la kulipa kwenu. I would never compare na kitu chochote kwenye suala la kutupa nguvu na kutupigania ndani na nje ya uwanja iwe kwenye jua kali au kwenye mua mlikuwepo.
“Katika kila nyakati ngumu hamkukata tamaa, hamkutuacha. Mwenyezi
Mungu awabariki sana. You are The True Heroes. Mwisho wa msimu mmoja ndio maandalizi ya msimu
mwingine. Inshaallah next season tutafanya vizuri zaidi,” amesema Tshabalala.
Simba ilikuwa inahitajika kupata ushindi dhidi ya Yanga leo Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ili itwae ubingwa lakini hilo halikutimia baada ya kufungwa na Yanga kwa mabao 2-0.
Mabao ya Pacome Zouzoua na Clement Mzize yameifanya Yanga imalize ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 82 ambazo zimeiwezesha kutwaa ubingwa.
Simba imemaliza msimu ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 78.