TFF yatakiwa kujenga vituo vya michezo kila mkoa

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Husna Sekiboko
Muktasari:
- Kamati ya Kudumu ya Bunge Elimu ,Utamaduni Sanaa na Michezo imefanya ziara ya siku moja katika kiwanja kikubwa cha michezo kilichopo Mnyanjani Jijini Tanga kinachojengwa na TFF
Tanga. Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeiomba Serikali ijenge vituo vya michezo kila mkoa.
Pia kamati hiyo, imelipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufuatia uwekezaji wa ujenzi wa mradi wa vituo viwili vya michezo vilivyopo Mnyanjani Tanga na Kigamboni jijini Dar es salaam.
Miradi hiyo inayotekelezwa hapa nchini ilianza mwaka 2020 na kukabidhiwa Februari 2023 baada ya awamu ya kwanza kukamilika ukihusisha ujenzi wa nyumba za kulala na jengo la utawala.
Mara baada ya kukamilika TFF imedhamiria kuwekeza katika soka la vijana wa kike na wa kiume wenye umri kati ya miaka 4-23, vijana wa kike watakaopatikana katika mikoa nchini wataweka kambi wilayani Kigamboni Dar es Salaam huku wakiume wakiwa Mnyanjani jijini Tanga.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo jana Septemba 9, 2023 akiwa pamoja na wajumbe wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko ameipongeza serikali kwa mapinduzi makubwa inayoyafanya kupitia sekta ya michezo hususan katika mradi huo.
Sekiboko ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Tanga alilisisitiza TFF kuendelea kuimarisha mahusiano baina yao na Wizara ya Michezo ili kusimamia na kufanikisha maono na mipango ya Serikali ya kuleta maendeleo kwenye sekta ya Michezo.
"Kwa niaba ya kamati hii nimpongeze sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa nguvu kubwa anayoitumia katika kuwezesha sekta ya michezo,
Tumeshuhudia katika michauano ya vilabu mbalimbali lakini hata katika timu zetu za Taifa amewekeza fedha nyingi na ameonyesha nia ya dhati ya kutaka kuendelea michezo nchini ". amesema Sekiboko.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' amesema wizara itaendelea kuhakikisha michezo yote hapa nchini inapewa kipaumbele na kupitia vituo hivyo.
"Tunaona umuhimu wa kufanya mambo makubwa namna hii kwa sababu tunaamini vituo hivi maendeo makubwa ya mpira wa miguu hapa nchini,
Moja ya mipango ambayo tunayo kwa sasa hivi Kama Serikali ni kujenga kituo kikubwa cha michezo ambacho kitasaidia kufundishia walimu wanaokuja kufundishia michezo huku mashuleni na vyuoni,"amesema Mwana FA.