Stars yaichapa Mauritania ikinusa robo fainali CHAN
Muktasari:
- Kundi B la mashindano ya CHAN 2024 linaundwa na Tanzania, Mauritania, Burkina Faso, Madagascar na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ imeendelea kugawa dozi kwenye michuano ya CHAN baada ya leo usiku kuitandika Mauritania bao 1-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Bao la Kapombe dakika ya 88 lilitosha kuipa Taifa Stars ushindi huo ambao umeifanya izidi kujichimbia kileleni mwa kundi B ikifikisha pointi sita.
Kapombe alifunga bao hilo kwa shuti kali la mguu wa kushoto akimalizia pasi ya Iddi Seleman ‘Nado’.
Kipindi cha kwanza Mauritania walionyesha upinzani mkubwa wakifunga mianya ya viungo wa Stars kupitisha mipira hasa kwa Fei Toto na Mudathir aliyeibuka mchezaji bora wa mechi.
Mwanzoni mwa dakika 45 za kipindi cha pili kocha Hemed Suleiman 'Morocco' alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili alimtoa Yusuph Kagoma baada ya kupewa kadi ya njano na kumuingiza Ahmed Pipino lakini pia alimuingiza Nassor Saadun na kumtoa Abdul Suleiman 'Sopu'.
Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na manufaa kwani Kagoma alionekana kutoka mchezoni akiwa mzito kufanya maamuzi na kwa upande wa Saadun baada ya kuingia alishambulia kwa Kasi.
Hata hivyo baada ya kucheza kwa dakika chache, Pipino alishindwa kuendelea baada ya kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Shekhan Khamis dakika ya 72.
Kwa kupata ushindi huo, Taifa Stars imeandika rekodi ya kupata ushindi katika mechi nyingi zaidi kwenye hatua ya makundi na kukusanya pointi nyingi katika Fainali za Chan.
Mwaka 2009 ilimaliza hatua ya makundi ikiwa na pointi nne na iliposhiriki fainali za mwaka 2020 pia ilimaliza ikiwa na pointi nne.
Ushindi huo dhidi ya Mauritania unaifanya sasa Taifa Stars ihitaji pointi mbili tu katika mechi zake mbili ilizobakiza dhidi ya Madagascar na Afrika ya Kati ili itinge robo fainali ya mashindano hayo.
Kikosi cha Stars kilichoanza, Yakoub Suleiman, Ibrahim Hamad, Dickson Job, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Idd Seleman, Feisal Salum, Abdul Suleiman 'Sopu', Yusuph Kagoma, Mudathir Yahya na Clement Mzize.
kikosi cha Mauritania kilichoanza, Abderrahmane Sarr, Mohamed Ramdane, Demine Saleck, El Mami Tetah, Alassane Diop, Nouh Mohamed, Soukrana M'haimid, El Hacen, Hamady N'diaye, Ahmed Ahmed na Mohamed Said.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa leo, Burkina Faso iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.