Simbu mzigoni Boston Marathon leo

Muktasari:
- "Nyota huyo kwa sasa yupo katika shepu nzuri ya ukimbiaji huku akitambia muda wake mzuri wa saa 2:04:38 ambao alipata katika mbio za Valencia Marathon mwaka jana".
Arusha. Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania,Alphonce Simbu amesema amejiandaa kushinda mbio za Boston Marathon zitakazofanyika leo Jumatatu nchini Marekani.
Mbio hizo zitaanza majira ya saa 11 jioni ambapo Simbu mwenye medali kadhaa ikiwemo medali ya Shaba ya mashindano ya Dunia ambayo yalifanyika London Uingereza mwaka 2017 pamoja na medali ya fedha ya Jumuiya ya Madola ambayo alipata mwaka 20222 Birmigham Uingereza.
Huku akiingia nane bora marathoni za Olimpiki mara mbili mfululizo mwaka 2016 akishika nafasi ya tano huko Rio De jeneiro Brazil kwa muda wa 2:11:15 na 2020 Tokyo Japan akimaliza wa saba kwa muda wa 2:11:35.
Atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wababe tisa wa riadha duniani akiwemo Sisay Lema wa Ethiopia ambaye anatetea medali yake ya Dhahabu aliyoshinda katika mbio za mwaka jana akitumia muda wa saa 2:06:17.
Pia akitambia rekodi binafsi ya kutumia muda wa saa 2:01:48 katika mbio za Valencia Marathon 2023 ambayo ilimfanya ashike nafasi ya nne katika chati ya wanariadha waliotumia muda mfupi zaidi kumaliza mbio ndefu.
Mwamba mwingine ambaye anatazamiwa kumtoa jasho ni mshindi mara mbili wa mbio hizo Evance Chebet ambaye mwaka jana alimaliza wa tatu pamoja na mshindi wa mbio za Chicago Marathon,John Korir.
Nyota huyo kutoka timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (Jwtz) mwenye cheo Cha Sajenti atakutana pia na kigingi cha bingwa wa Dunia 2024 Victor Kiplangat pamoja na washindi namba mbili na tatu mbio za Berlin Marathon 2024,Cybrian Kotut na Haymanot Alew.
Simbu kwa sasa yupo katika shepu nzuri ya ukimbiaji huku akitambia muda mzuri wa saa 2:04:38 ambayo alipata katika mbio za Valencia Marathon mwaka jana amesema kutokana na maandalizi ambayo amefanya anaamini kesho atalipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa kuongoza na kuwashinda wababe wa mbio hizo kwa dunia.
“Natambua kutakuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wengine ndio maana nimefanya maandalizi ya kutosha ambayo yatanifanya kushinda"amesema Simbu.
Ameongeza kutokana na uzoefu alionao katika mbio kubwa za Dunia ambazo ameshiriki hana shaka hata kidogo kuhusu uwezo wake wa kufanya kweli na kutumiza malengo yake ambayo ni kushinda.
Kocha wa timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (Jwtz),Antony Mwingereza amesema matumaini kwa Simbu kufanya vizuri leo ni makubwa kutokana na maandalizi ambayo walifanya lakini pia shepu ambayo nyota huyo anayo kwa sasa.
"Sina wasiwasi hata kidogo na uwezo wa Simbu ,tulifanya maandalizi ya kutosha kikubwa tu Watanzania wamuombee leo afanya kweli", ameongeza Mwingereza.
Kapteni Christopher Masanga ni meneja wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi Tanzania (Jwtz),amemtaka mwanariadha huyo kuoengeza jitihada ambayo itamfanya kufanikisha malengo ambayo ni kushinda Boston Marathon kesho.
Ameweka wazi kuwa hamasa ni kubwa kwa mwanariadha huyo kuanzia kwenye maandalizi ambayo yatamfanya kwenda kupambana na kurudi na ushindi nchini.
Mshindi wa kwanza mbio za Boston Marathon atavuna kitita cha Dola 150,000 mshindi wa pili Dola 75,000 wa tatu 40,000 huku wanne akivuna 25,000.