Simbu, Geay: Vita ya medali na miamba mitano

Dar es Salaam. Kuna matumaini makubwa ambayo Watanzania wanayo kwa wakimbiaji wa mbio ndefu, Alphonce Simbu na Gabriel Geay kuwa wanaweza kumaliza ukame wa miaka 44 wa Tanzania kushiriki michezo ya Olimpiki bila kupata medali.
Tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza Tanzania imetwaa medali mbili tu ambazo zote ilizipata katika michezo ya mashindano hayo iliyofanyika mwaka 1980 huko Moscow,Urusi.
Medali hizo zote zilikuwa za fedha,ambapo moja ilitwaliwa na mwanariadha Suleiman Nyambui,aliyeshika nafasi ya pili katika mbio za mita 5000 na nyingine ilichukuliwa na Filbert Bayi katika mbio za mita 3000.
Mara baada ya hapo,Tanzania imekuwa ikipeleka wanamichezo wake katika mashindano hayo lakini wameshindwa kurudi na medali.
Matumaini ya Watanzania kwa Simbu na Geay yanakuja kutokana rekodi nzuri na mafanikio ambayo wamewahi kuyapata katika mbio tofauti hapo nyuma.
Simbu ana medali moja ya Shaba ya mashindano ya Dunia ambayo yalifanyika London, England mwaka 2017 akitumia muda wa 02:09:51 na medali ya fedha ya michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022 huko Birmingham, England.
Geay ndiye bingwa wa marathoni Tanzania kwa upande wa wanaume akiwa na rekodi ya masaa 2:03:00 rekodi ambayo aliiweka katika mbio za Valencia marathon zilizofanyika Hispania,Desemba 4,2022 akimaliza wa pili.
Hata hivyo wawili hao wanapaswa kufanya kazi ya ziada katika Olimpiki mbele ya wanariadha watano ambao nao wana rekodi na historia nzuri katika mashindano hayo na mbio tofauti na ufuatao ni wasifu mfupi wa wakimbiaji hao.
Eliud Kipchoge
Mkenya huyo katika michezo ya mwaka huu anasaka rekodi ya kushinda medali ya dhahabu kwenye Olmpiki katika mbio za marathoni baada ya kutawala katika michezo ya mwaka 2020 na ile ya 2016.
Ushindi wa medali ya dhahabu kwenye mbio za Marathoni utamfanya aweke rekodi ya kuwa mshindi aliyepata ushindi mara nyingi zaidi katika Olimpiki na kuwaacha Abebe Bikila wa Ethiopia na Waldemar Cierpinski wa Ujerumani ambao nao kila mmoja alishinda medali ya dhahabu kwenye marathoni Olimpiki mara mbili.
Benson Kipruto
Anashikilia rekodi ya kuwa mkimbiaji aliyekimbia marathoni kwa haraka zaidi mwaka huu akitumia muda wa 2:02:16, tukio alilolifanya katika mbio za Tokyo Marathon ambazo aliibuka mshindi.
Mwaka jana alipata medali ya shaba katika mbio za Chicago Marathon na alipata medali ya fedha katika mbio za Boston Marathon.
Kenenisa Bekele
Katika umri wa miaka 42, Bekele ni tishio jingine kwa Simbu na Geay kwenye mbio za marathoni katika Olimpiki mwaka huu huko Ufaransa.
Ana medali tatu za dhahabu katika Olimpiki lakini hakuzipata katika mbio za marathoni ambapo mbili alivuna katika mbio za mita 10,000 na moja katikambio za mita 5,000.
Victor Kiplangat
Victor Kiplagat ni mkimbiaji mwingine ambaye Simbu na Geay wanapaswa kumdhibiti katika mbio za marathoni kwenye michezo ya Olimpiki mwaka huu licha ya umri wake mdogo wa miaka 24.
Raia huyo wa Uganda ni mshindi wa mashindano ya dunia mwaka jana yaliyofanyika Budapest, Hungary lakini pia mwaka 2022 alishinda medali ya dhahabu katika michezo ya Jumuiya ya Madola.
Sisay Lemma
Mshindi wa medali ya dhahabu katika mbio za Boston Marathon mwaka huu akitumia muda wa 2:06:17 lakini pia mwaka 2021 alishinda London Marathon akitumia muda wa 2:04:01.
Muda bora zaidi ambao aliwahi kukimbia ni 2:03:36 aliposhika nafasi ya tatu katika mbio za Berlin Marathon mwaka 2019.