Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba wamlaani refa kwa vigoma bandarini

Muktasari:

  • RS Berkane imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa kuifunga Simba mabao 3-1 katika mechi mbili za fainali.

Mashabiki wa Simba wamemtaja refa Beida Dahane kutoka Mauritania kuwa ndio sababu ya timu yao kutoka sare ya bao 1-1 na RS Berkane katika mechi ya pili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika jana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Matokeo hayo yameifanya RS Berkans itwae ubingwa kwa ushindi wa mabao 3-1 ikinufaika na ushindi wa mabao 2-0 ilioupata katika mechi ya kwanza ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco, Mei 17, 2025.

Muda mfupi baada ya kuwasili katika Bandari ya Dar es Salaam leo wakitokea Zanzibar, kikundi cha mashabiki hao wa Simba kimekuwa kikiimbia nyimbo za kumlaumu refa Dahane kuwa ndiye amesababisha timu yao kupoteza jana.

“Nani katuua Simba, refa huyo. Nani katuua Simba refa huyo,” mashabiki hao wanaimba wakiongozwa na kikundi chao cha ngoma.

Mashabiki hao waliimba pia,”mchawi ndugu refa ametumwa. Mchawi ndugu refa ametumwa.”

Baada ya shangwe hizo za kama dakika 10, mashabiki hao wamepumzika kwa muda wakingojea msafara wa wachezaji ambao utaingia na boti ya saa 6:30 mchana.

Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kuingia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2024 baada ya kuunganishwa kwa mashindano ya Kombe la Washindi Afrika na Kombe la CAF.

Lakini kwa mashindano ya klabu Afrika, hiyo ni mara ya pili kwa Simba kutinga hatua ya fainali baada ya kufanya hivyo mara ya kwanza mwaka 1993 katika Kombe la CAF.

Mwaka huo 1993, Simba ilipoteza katika fainali dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 2-0 ambayo ilifungwa katika mechi ya marudiano Dar es Salaam baada ya mechi ya kwanza ugenini kumalizika kwa sare tasa.

Kwa RS Berkane huo ni ubingwa wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufanikiwa kutwaa msimu wa 2019/2020 na msimu wa 2021/2022.

RS Berkane kwa kutwaa ubingwa imepata kitita cha Dola 2 milioni (Sh5.4 bilioni) na Simba kwa kumaliza katika nafasi ya pili inapata kiasi cha Dola 1 milioni (Sh2.7 bilioni).