Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba unyama mwingi ikitinga makundi CAFCL

EWAAA...ndivyo walivyosikika mashabiki wa soka walioujaza Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, baada ya Simba kulazimishwa sare nyumbani na Power Dynamos ya Zambia na kukata tiketi ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiifuata Yanga iliyotangulia mapema.

Sare hiyo imeinufaisha Simba kufuzu hatua hiyo kwa kutumia kanuni ya faida ya bao la ugenini baada ya awali kutoka sare ya 2-2 ugenini wiki mbili zilizopita zilipokutana kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, mjini Ndola kwa matokeo ya jumla kuwa sare ya 3-3 na kufanya iwe mara ya sita kwa timu hiyo kucheza hatua hiyo kwa michuano ya CAF.

Mbali na kufuzu hatua hiyo, Simba pia imejihakikishia kukunja Dola 700,000 (zaidi ya Sh 1.8 Bilioni) ikiungana na wababe wengine waliofuzu mapema wikiendi iliyopita.

Simba yenye rekodi tamu kwenye michuano ya CAF, ilifuzu mara ya kwanza makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, kisha ikarudia 2018-2019, 2020-2021 na 2022-2023 mbali na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2020-2021. Pia hii ni mara nne mfululizo kwa Simba kutinga makundi zikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa na moja ya Shirikisho.

Kufuzu kwa Simba pia kumeifanya Tanzania kuandika historia kwa mara ya kwanza kupenyeza timu mbili kwa mpigo kucheza hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa baada ya Yanga juzi usiku kuing'oa Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0.

Licha ya Simba kufuzu, lakini mashabiki wa timu hiyo hawakuwa na furaha kutokana na timu hiyo kushindwa kuonyesha soka tamu, kwani wageni walionekana kuwa bora zaidi kwa dakika zote 90 za pambano hilo, huku mabao yote yakifungwa na Wazambia.


Bao makosa ya viungo

Simba ilishtukizwa kwa bao la kuongoza la Dynamos lililofungwa dakika ya 16, huku lawama zikiwa kwa  viungo Clatous Chama, Fabrice Ngoma na Mzamiru Yassin walioshindwa kutoa mchango wao kwa angalau kumsumbua mfungaji Andy Boyeli aliyeumiliki mpira na kuzunguka kabla ya kuachia shuti na kufunga.


Mfumo waibeba Dynamos

Simba ilianza na mfumo wa 4-3-3 huku wapinzani wao Dynamos wakianza na mfumo wa 3-5-2 ambao uliwafanya Simba kuonekana wachache katikati ya uwanja na kushindwa kupenya kirahisi ngome ya wageni.


Bocco ambeba Robertinho

Simba ilifanya mabadiliko ya kwanza mwanzo wa kipindi cha pili akitoka Jean Baleke nafasi yake ikichukuliwa na nahodha wao Mkuu John Bocco na dakika kumi baadaye tangu aingie alipoteza nafasi ya wazi shuti lake lilitoka nje kidogo akipokea pasi ya kiungo Clatous Chama.

Baada ya kupoteza nafasi hiyo mashabiki wa Simba walianza kumrushia chupa za maji wakichukizwa na hatua hiyo ya kupoteza nafasi hiyo.

Hata hivyo, Bocco alionekana kuziokota na kuzisogeza nje kidogo huku Chama akijaribu kuwatuliza mashabiki hao lakini Bocco ndiye aliyeiokoa Simba dakika ya 68 baada ya krosi yake kusababisha beki wa Dynamos Kondwani Chiboni kujifunga wakati akijaribu kuiokoa.

Baada ya kuingia kwa bao hilo Bocco alilazimika kuwanyamazisha kwa kuwaonyeshea ishara ya kufunga midomo mashabiki waliojaza uwanjani ambao awali walionekana kutofurahia kuingizwa kwake kumpokea Jean Baleke.


Mzamiru na Kanoute

Kiungo Mzamiru Yassin ni kama ndiye aliyemuingiza mwenzake Sadio Kanoute uwanjani ambapo mara baada ya Simba kupata bao aliwafuata makocha wake na kuwashauri aingie Kanoute.

Hata hivyo, Kocha Robertinho alimtaka kusubiri, lakini mara baada ya bao hilo Dynamos wakianza kuishambulia kwa kasi Simba na Mzamiru aliinuka tena na kuwataja makocha kumuingiza Kanoute huku kocha wake akimfokea na kumtaka atulie.

Mara baada ya muda ushauri huo ulikubalika kwa Mzamiru na aliposikia Kanoute anaitwa aliinuka haraka na kumtaka kuharakisha kuvaa ili aingie.

Kuingia kwa Kanoute kulizima nguvu ya Dyanamos ambao walikuwa wanatengeneza mashambulizi makali kwenda kwa wenyeji wao.


Boyeli Vita na Che Malone, Kennedy

Mshambuliaji Boyeli alikuwa na kazi kubwa ya kutengeneza utulivu wa mashambulizi akitumia nguvu zake lakini vita ilikuwa ni kupambana na mabeki wawili wa Simba Che Malone Fondoh na Kennedy Juma.

Che Malone alionekana kuwa kiongozi mkuu kwa kuwatuliza wenzake ndani ya ukuta wa Simba lakini akiwa pia na akili ya kupanda juu kupandisha mashambulizi.


Wazambia ngazi ya Simba makundi

Simba imeitumia klabu ya kutoka Zambia kwa mara mbili kwenda makundi wakitangulia kuwang'oa Nkana Red Devils Desemba 23, 2018, lakini jana tena wakaitumia Dynamos kwenye safari kama Ile ya kutinga makundi

Simba: Ayoub, Kapombe, Tshabalala, Kennedy, Che Malone, Mzamiru/Onana, Ngoma, Chama, Baleke/Bocco, Saido na Kibu/Kanoute

Dynamos: Mwanza, Chiboni, Makwaza, Mutale, Katebe, Soko,Tembo, Zulu, Muwowo, Makubuli na Boyeli/Ngwenya.