Rais Samia awamwagia maua Tanzania Futsal

Muktasari:
- Fainali za AFCON za Futsal kwa wanawake zinafanyika kwa mara ya kwanza ambazo zitatoa timu mbili za kwenda Kombe la Dunia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya taifa ya wanawake ya Futsal kwa kuingia hatua ya fainali katika fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea Morocco.
Mbali na kuingia fainali, timu hiyo imejihakikishia kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Phillipines baadaye mwaka huu.
Rais Samia Samia amesema kuwa mafanikio hayo ni heshima kwa Tanzania.
“Hongereni wanangu Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mchezo wa Futsal kwa kufuzu kuingia fainali ya mashindano hayo kwa Bara la Afrika, na wakati huo huo kufuzu kucheza Mashindano ya Kombe la Dunia la Futsal kwa Wanawake 2025 ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), yatakayofanyika huko Manila, Ufilipino baadaye mwaka huu.
“Nimefurahishwa na juhudi na nidhamu yenu katika mashindano haya. Ushindi wenu ni heshima kwa nchi yetu, na hamasa zaidi kwa watoto wa kike kushiriki katika michezo, si tu kwa burudani lakini pia kama ajira. Ninawapenda na ninawatakia kila la kheri,” amesema Rais Samia.

Timu ya taifa ya wanawake ya Futsal imefuzu kuingia fainali kwenye AFCON baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Cameroon.
Mabao yaliyoipa ushindi timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ya Futsal yamefungwa na Anastazia Katunzi, Violeth Nicholas na Aisha Mnunka.