Tanzania yatamba ASFC, Futsal Afrika

Muktasari:
- Bingwa wa mashindano ya soka kwa shule Afrika anapata kiasi cha Dola 300,000, mshindi wa pili akipata Dola 200,000 na mshindi wa tatu anapata Dola 150,000.
Timu ya Tanzania imechukua ubingwa wa mashindano ya soka ya shule Afrika (ASFC) baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Senegal jana katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ghana.
Taji hilo ni la pili mfululizo kwa Tanzania na linaifanya iongoze kwa kulitwaa mara nyingi kwani hakuna nchi nyingine iliyowahi kufanya hivyo tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2023.
Tanzania haikuondoka na taji hilo pekee bali pia imepata tuzo nyingine mbili ambazo ni za timu yenye nidhamu na kipa bora.
Tuzo ya kipa bora imeenda kwa Rajabu Manyerezi wakati mchezji bora wa mashindano ni Souleymane Commissaire Faye wa Senegal na wafungaji bora ni John Andor na Ingatus Cyril Acquah Hagan wa wenyeji Ghana.
Kwa upande wa wanawake, wenyeji Ghana wameibuka mabingwa baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Uganda.
Wakati Tanzania ikitamba katika mashindano ya shule Afrika wanaume, timu ya taifa ya wanawake ya mchezo wa Futsal imeingia hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Senegal katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Moulay Abdallah Sports Hall.

Mabao ya Tanzania katika mechi hiyo yamefungwa na Donisia Minja, Stumai Abdallah na Anastazia Katunzi.
Ushindi huo umeifanya Tanzania kuongoza kundi C na hivyo imekata moja kwa moja tiketi ya kucheza nusu fainali ya mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika.