Senegal yapinga uamuzi wa CAF, kwenda CAS
Baadhi ya wachezaji wa Senegal na Morocco wakilumbana baada ya maamuzi ya refa, Jean-Jacques Ndala, kuamuru mkwaju wa penalti kwenda langoni mwa Senegal baada ya Brahim Diaz kufanyiwa faulo na Malick Diouf katika mechi ya Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Januari 18, 2026.
Muktasari:
- Senegal imeelezea kutoridhishwa kwake na uamuzi huo, ikiutaja kuwa wa kiholela, usiokubalika, huku ikidai kuwa unadhoofisha taswira ya soka la Afrika kimataifa.
Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limepinga vikali uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) uliotolewa Machi 17, 2026, kuhusu shauri lililotokana na mechi ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya Senegal na Morocco.
CAF imebaini kuwa mwenendo wa timu ya Senegal ulikiuka vifungu vya 82 na 84 vya kanuni za AFCON, hatua iliyosababisha kutangazwa kwa Senegal kupoteza mechi hiyo kwa njia ya mezani kwa mabao 3-0 dhidi ya Morocco.
Kifungu cha 82 kinasema, ikiwa timu kwa sababu yoyote ile inakataa kucheza au inaacha uwanja kabla ya mwisho wa mechi bila idhini ya mwamuzi, itachukuliwa kuwa imeshindwa na itatupwa kwenye mashindano yote.
Kifungu cha 84, kinakamilisha kifungu cha 82 kwa kusema, timu inayokiuka kifungu cha 82 itatupwa kabisa kwenye mashindano na itapoteza mechi kwa mabao 3–0.
Hata hivyo, Senegal imeelezea kutoridhishwa kwake na uamuzi huo, ikiutaja kuwa wa kiholela, usiokubalika, huku ikidai kuwa unadhoofisha taswira ya soka la Afrika kimataifa.
Shirikisho hilo limeweka wazi dhamira yake ya kupinga uamuzi huo kwa nguvu zote, likilenga kulinda maslahi ya soka la Senegal na kuhakikisha haki inapatikana.
Katika hatua nyingine, FSF imetangaza kuwa itakata rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) iliyoko Lausanne, Uswisi, kwa lengo la kutafuta haki ya mwisho katika sakata hilo.
Wakati huo huo, FSF imeahidi kuendelea kuheshimu misingi ya haki na uadilifu katika mchezo wa soka, huku ikiahidi kuufahamisha umma kuhusu maendeleo yote ya kesi hiyo yenye mvuto mkubwa barani Afrika.