Rio ataja wawili kuiokoa Man United
Muktasari:
- Red Devils imepitia miaka 12 ya tabu tangu kuondoka Ferguson mwaka 2013, ikisajili wachezaji lukuki pamoja na kuajiri makocha sita lakini imeshindwa kabisa kurudisha enzi zao.
MANCHESTER, ENGLAND: Lejendi wa Manchester United, Rio Ferdinand ametaja wachezaji wawili ambao anadhani wangeweza kuwaokoa Manchester United kutoka kwenye kipindi kigumu baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka.
Red Devils imepitia miaka 12 ya tabu tangu kuondoka Ferguson mwaka 2013, ikisajili wachezaji lukuki pamoja na kuajiri makocha sita lakini imeshindwa kabisa kurudisha enzi zao.
Katika misimu miwili ya hivi karibuni mashetani hawa wekundu wanaonekana katika hali mbaya zaidi waliyowahi kuwa nayo baada ya kuondoka kwa Sir Alex.
Ferdinand, aliyecheza mechi 455 akiwa na Man United anaamini klabu yake hiyo ya zamani ingekuwa katika nafasi tofauti kwa sasa kama ingesajili nyota wawili waliokuwa na uwezekano wa kuwapata.
Akizungumza na Michael Owen kwenye podcast ya Rio Ferdinand Presents, beki huyo wa zamani wa England alisema:
“Hilo ndilo kosa kubwa zaidi nadhani wamelifanya katika miaka 10 iliyopita. Nadhani kama wangeenda na kulipa kiasi ambacho Spurs wanataka, wangeweza kumpata Harry Kane. Nina uhakika kabisa, nitasema hili na ninaamini, kama Man United ingeenda na kumchukua Declan Rice na Harry Kane kwa wakati ule, ingekuwa katika nafasi nzuri kwa sasa.”
Mbali ya kuamini wachezaji hao wawili wangesababisha kitu, Owen na Rio wanaamini mazingira pia ni sehemu mojawapo ya matatizo ya timu yao wakiwa na maana ya timu inakosa wachezaji wakongwe ambao ni viongozi.
“Pia kuna utamaduni wa kujitoa kwa kila kitu kwa ajili ya timu ili ishinde, ambao unatengenezwa hauji tu. Man United lazima wafikie hatua ya kuunda hali hiyo. Kocha lazima azalishe mazingira hayo ili wachezaji wafuate.”
Man United ikiongozwa na wachezaji wake wapya Bryan Mbuemo, Matheus Cunha na Benjamin Sesko ilianza kampeni yao msimu huu kwa kichapo cha bao 1-0 mbele ya Arsenal, kisha ikatoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Arsenal, kisha ikaenda kutolewa Carabao Cup kwa changamoto ya mikwaju ya penalti kutoka kwa timu ya madaraja ya chini, Grimsby Town.
Hata hivyo, baada ya mwanzo huo mgumu, Man United ilionekana kurudi katika mstari baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Burnley.