Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raphael Kinda anayesaka Sh2 milioni kujitibu

Masahibu ya majeraha kama haya yamewakumba wachezaji wengi, ambapo yupo pia kinda mwenye kipaji kikubwa ndani ya Singida Black Stars, Helman Raphael  ambaye anapambana na majeraha makubwa ya kuchanika nyama za paja.

Raphael ambaye kabla ya kujiunga na Singida alikuwa akiwania na klabu mbalimbali kutokana na kipaji chake, ameshindwa kuwa na maisha mazuri ndani ya Singida kutokana na changamoto hizo za majeraha.

Kwa mujibu wa kinda huyo, kiasi cha Sh2 milioni tu kimekwamisha kupona kwake kwa wakati akipambana zaidi ya miezi saba sasa.

Raphael (19) anasema, “Nina takribani miezi wa saba sasa, kuna daktari nilimfuata jijini Dar es Salaam, akaniambia kadiri nilivyokuwa naendelea kucheza ndivyo nilivyokuwa nikiongeza ukubwa wa jeraha bila mimi kujua.

“Nilichokuwa nakilinda ni nafasi yangu katika timu, ndio maana nilikuwa naendelea kucheza ijapokuwa nina majeraha. Hata kama nina maumivu nitayaficha tu ilimradi nafasi yangu isiondoke.


Ilivyoanza

Kwa mujibu wa Raphael, hilo ni tatizo ambalo lilianza tu. Daktari akamwambia inasababishwa na kunyoosha kabla hajaanza mazoezi.

Anasema kwa hali ya uwanja ambao walikuwa wanautumia ndio ukasababisha zaidi majeraha hayo. Anasimulia kuwa chanzo alikuwa anawania mpira juu, uliposhuka tu kwa kuwa viungo vilikuwa havijakunjuka sawasawa, akasikia maumivu makali baada ya kushukia kwenye shimo uwanjani.

Raphael anasema hapohapo akajua labda ni nyonga imeshtua kidogo, lakini anakiri kwamba haikuwa hivyo.

“Nikawa napata matibabu madogo madogo, napata nafuu lakini baada ya muda hali ile inarudi vilevile tena wakati mwingine yanakuwa makali zaidi.

“Nikapewa ushauri kwamba nitafute matibabu zaidi ndio nikaanza kuhangaika huku na kule, kuna wakati nikashindwa kabisa kucheza nikajikuta nalia mwenyewe tu nikijiuliza nini kimenikumba mapema hivi lakini nakosa majibu sahihi,”anasema Raphael.

Akielezea maisha ya majeraha, anasema kabla hajakutana na daktari maisha yalikuwa ni magumu, “Siwezi nikadanganya kwa sababu unaweza ukapata matibabu leo, kesho ukasitisha kwa ukosefu wa fedha.

“Baadaye ukija kupata hela mbeleni ndio uanze tena matibabu, ambayo inazidi kuongeza jeraha tofauti na mwanzo.”


Tatizo

“Nilikuja kugundua tatizo baada ya kumfuata Daktari na kumuelezea hali ninayoipitia,akaniambia ni shida ya ‘Ligaments za nyonga’.

“Huwa likianza unapata maumivu yanayokuja na kuondoka ila unavyozidi kucheza ndivyo linavyozidi kuwa kubwa, ila sasa naendelea vizuri na kuna aina tatu za huduma natakiwa kupata, nimeanza ya kwanza.”


Umbali

“Napata matibabu hata nikiwa mbali muda mwingine, kwani nawasiliana na daktari  kwa njia ya simu na ananipa maelekezo ya dawa za kutumia.

“Nikipata likizo nitazidi kumuona zaidi na shida ni pesa kwani uwezo wangu wa kulipia matibabu ni mdogo lakini pia nalinda nafasi yangu ili kocha asinisahau.

“Nipo naangalia wenzangu kwa sababu sichezi wala sifanyi mazoezi mpaka nitakapo kuwa sawa kabisa.


Kuhusu gharama

“Gharama za matibabu ni kubwa kidogo kuanzia milioni moja na nusu mpaka mbili na matibabu yako ya aina tatu kama nilivyokuambia hapo awali.

“Inamaana mpaka zije ziishe huwezi kusema ni gharama ndogo,  ambayo inaweza ikatumika kiukweli inahitaji pesa nyingi na kwa maisha yangu mimi, kupata matibabu mpaka mwisho ni ngumu.

“Kwa hiyo itabidi tena nitulie au nipate mtu wa kunipa msaada, ili nipone tena na nirejee katika mazoezi yangu kama kawaida, kuna muda nawaza kama nitapoteza kipaji changu cha mpira, kwani bado nina malengo mengi na umri wangu ni mdogo.


Timu za vijana malipo yake

“Mimi nipo timu ya vijana kama mnavyofahamu maisha ya timu za vijana bado hayako kwenye mfumo mzuri wa malipo wala kusaini mikataba mikubwa, kwa hiyo kuna posho tu ndogondogo ndio tunazopata lakini sio malipo makubwa, kama ningekuwa timu ya wakubwa ningekuwa nimeshapona mpaka sasa kwa kuwa tatizo langu linatibika.


Habari hii imeandikwa kwa msaada wa Taasisi ya Gates Foundation.