Yacouba...Alitumia mamilioni kutibu goti

Muktasari:
- Kwa mujibu wa mchezaji huyo, aliwasiliana na klabu yake kuwajulisha juu ya mahitaji ya matibabu yake lakini akaona ni kama wanamchelewesha
“Ilikuwa kwenye mchezo wa timu yangu Tabora United dhidi ya KMC, nakumbuka nilimpiga chenga beki nikiwa nataka kwenda kufunga nikateleza vibaya mguu wangu wa kushoto ukageuka, nikasikia maumivu makali eneo la goti, nikaona labda ni kitu kidogo. Nikajaribu kuinuka lakini maumivu yakawa makali zaidi.”

Haya ni maneno ya kiungo mshambuliaji wa Tabora United, Yacouba Songne akielezea safari ya majeraha yake ilivyoanza, kufuatia kuumia vibaya goti lake la mguu wa kushoto.
Yacouba ambae ni raia wa Burkina Fasso aliyewahi kuitumikia Yanga na iliyokuwa Ihefu kabla ya kuuzwa na sasa kuitwa Fountain Gate FC, yupo nje ya uwanja akiuguza goti lake ikiwa ni majeraha ya pili makubwa kuwahi kupata tangu atue nchini, akiwa kwenye klabu mbili tofauti.
Yacouba yuko nje ya uwanja na sio nje ya uwanja pekee lakini yupo nchini Morocco, akipambana kupona majeraha yake hayo, akiwa tayari ameshafanyiwa upasuaji wa goti hilo baada ya kutangulia kupambana kupona hapa nchini lakini ikashindikana.

Hatua za awali
Mchezaji huyo anasema alianza kupambania afya yake akiwa hapa nchini, “Klabu yangu na mimi tulishirikiana vizuri kutafuta matibabu sahihi lakini baada ya muda kama mwezi hivi, nikaanza kuona mwanga wa kupona sawasawa maumivu yakaanza kupungua, nikahisi nakaribia kurudi uwanjani.
“Nikaanza hata mazoezi, lakini mapema tu maumivu yale yakarudi vilevile kama mwanzoni na daktari akanishauri nitafute tiba zaidi ya kufanyiwa upasuaji ili nipone sawasawa,” anasimulia.
Yacouba anasema alipoambiwa suala hilo limuumiza sana, kwake aliona kama ‘mkosi’ kwa kuwa alikutana na matatizo kama hayo wakati akiwa Yanga, lakini sasa akiwa Tabora pia ilijirudia ingawa ni miguu tofauti.
“Waliniambia naweza kutibiwa hapa nchini, lakini nilipata wasiwasi nikikumbuka wakati nikiwa Yanga waliona niende nje kutibiwa vipi sasa. Nikafanya mawasiliano na ndugu zangu na marafiki wakanishauri ni bora niende Morocco ambako nitapata matibabu bora zaidi.”

Atimka nchini
Kwa mujibu wa mchezaji huyo, aliwasiliana na klabu yake kuwajulisha juu ya mahitaji ya matibabu yake lakini akaona ni kama wanamchelewesha.
Alifanya uamuzi mgumu na kwenda Morocco haraka kwa gharama zake ili kuokoa kipaji chake, aliwasiliana kila kitu na daktari bingwa wa magoti na kujipanga kwa kila kitu.
“Nilikuwa nasumbuliwa na ‘anterior cruciate ligament’ ilikuwa imekatika kwenye mguu wangu wa kushoto, jitihada zangu za awali zote hazikuweza kusaidia ndio nikaamua kusafiri kuja Morocco kupata matibabu ili nirudi kwenye kazi yangu kwa kuwa bado nina nguvu ya kucheza zaidi,” anasema.

Imejirudia
Yacouba anasema tatizo hilo ni kama limejirudia kwani akiwa Yanga alipata tatizo kama hilo.
Anasema wakati huo, aliumia akiwa mazoezini, “Bahati nzuri nawashukuru viongozi wa Yanga kuanzia Rais wao na wote walisimamia nikapata matibabu sahihi, walinipeleka Tunisia nikapatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji na kurudi hapa Tanzania kwa gharama zao.
“Nilikuwa napata huduma zote zilizostahili, nawashukuru sana madaktari wa wakati huo kuanzia dokta Youssef (Ammar) najua Yanga ilitumia gharama kubwa, lakini jambo zuri kwangu niliweza kurudi uwanjani kwa wakati na nikaendelea na majukumu yangu kama kawaida ingawa baadaye waliniacha kwenye timu.”

Gharama si mchezo
Yacouba anasema aliamua kuzingatia maisha yake bila kujali gharama, kama angesema asichukue maamuzi magumu kwa kusubiri Tabora wamtibu, anadhani ingekuwa tatizo kubwa sana kwake.
Kwenda Morocco kuna gharama kubwa, kwa haraka mpaka sasa ameshatumia kiasi cha Dola za Marekani 12000 (Sh32.2 milioni) kwenye maeneo mbalimbali.
Mchezaji huyo anasema kufanyiwa upasuaji pekee alitumia dola 2600 (Sh7 milioni) lakini kuna gharama za tiketi ya ndege dola 3000 (Sh8 milioni).
“Kujiuguza nako kuna gharama yake, nimetumia dola 1700 (Sh4.5 milioni) pia kuna gharama ya yule daktari anayekuja kukufuatilia kila siku ni gharama kubwa, lakini nilimuomba nimlipe kwa dola 1000 (Sh2.6 milioni) hizo namlipa kila baada ya wiki mbili.
“Na nipo huku kwa mwezi wa pili sasa, bado kuna gharama ya usafiri natumia teksi kwenda na kurudi ni dola 20 (Sh54000) piga hiyo hesabu kwa kila ninapokwenda, ndani ya miezi miwili hapo bado haujalipia sehemu unayokaa wala hujala chakula, kwahiyo ni gharama kubwa lakini unaamua kuchukua maamuzi magumu ili upone sawasawa.”

Yacouba anasema anamshkuru Mungu kwasasa maendeleo yake ni mazuri na kila kitu kipo sawa. Na kwamba anafarijika kuona anapata uhakika kwamba atarudi uwanjani kwa haraka.
“Hata madaktari wameniambia hawakutarajia kama mambo yatakuwa sawa kama ambavyo ipo sasa, nahitajika kubaki hapa kwa wiki chache baada ya hapo nitarudi nyumbani Burkina Fasso na baadaye nitarudi Tanzania.
“Nawashukuru sana madaktari wote ambao walipambana na mimi kuanzia Tanzania nikianza na Dokta Gilbate (Kigadye) na wasaidizi wake wote, walijitahidi sana kuhakikisha nakuwa sawa…
“Najua walitaka niendelee na matibabu pale Tanzania lakini niliona bora nije huku kwa uhakika mkubwa zaidi, bila kujali gharama kubwa ambazo nazipitia kitu muhimu hapa ni kupata uihakika wa kupona sawasawa.”
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa Taasisi ya Gates Foundation