Raja Casablanca yamtambulisha rasmi Fadlu Davids, Simba yamuaga
Muktasari:
Fadlu Davids alikuwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca wakati timu hiyo ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco, 2023/2024.
Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Fadlu Davids kuiaga Simba, Raja Casblanca ya Morocco imemtangaza rasmi kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo.
Kupitia taarifa yake kwa umma ambayo imeitoa leo, Septemba 22, 2025, Raja Casablanca imesema kuwa Fadlu Davids anajiunga nao kuchukua nafasi ya Lassad Chabbi aliyetimuliwa.
"Raja Club Athletic imetangaza kumteua Fadlu Davids kuwa Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza. Davids alikuwa mchezaji muhimu katika msimu wa kihistoria wa 2023-2024 ambao tulitwaa ubingwa wa taifa "Botola Pro," ambao timu ilishinda bila kupoteza mechi, na Kombe la Throne akicheza jukumu muhimu kama Kocha Msaidizi.
"Kuteuliwa kwa Fadlu Davids kukiongoza kikosi cha kwanza cha Raja kulitokana na ujuzi wake wa awali wa klabu, ambao unamfanya kuwa mtu bora wa kuimarisha mshikamano wa kundi na kuiongoza Raja Club Athletic kufikia malengo yake ya kimichezo na kitaasisi.
"Uamuzi huu unakuja kama sehemu ya mwendelezo wa mradi mpya wa Raja Club Athletic, ambao unalenga kujenga muundo thabiti na mzuri wenye maono yenye mwelekeo wa siku zijazo.
"Klabu inathibitisha kuegemea kwake kwa usaidizi usio na mashaka wa mashabiki wake waaminifu kuunga mkono timu katika awamu hii mpya," imefafanua taarifa ya Raja Casablanca.
Fadlu anarejea Raja Casablanca baada ya kuitumikia Simba kwa muda wa siku 444, tangu alipojiunga nayo Julai mwaka jana.
Taarifa za Davids kuondoka Simba zilipamba moto baada ya timu hiyo jana kurejea nchini ikitokea Botswana kupitia Afrika Kusini ambapo Kocha huyo na wasaidizi wake hawakuwepo.
Baadaye ilifahamika kwamba Davids amesafiri kwenda Morocco kumalizana na Raja Casablanca na leo aliiaga rasmi klabu hiyo, jambo ambalo lilidhihirisha kuwa anaoondoka.
Kufuatia utambulisho wa Fadlu Davids ndani ya Raja Casablanca, Simba nayo imetoa taarifa rasmi ya kumuaga Kocha huyo Raia wa Afrika Kusini.
“Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha Mku Fadlu Davids baada ya kuhudumu na timu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Makubaliano haya ni matakwa binafsi ya kocha Fadlu kwa uongozi wa klabu.
“Klabu ya Simba inamshukuru Kocha Fadlu kwa kuiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kumalizia nafasi ya pili kwenye Ligi kuu ya NBC.
Uongozi wa klabu unamtakia kheri na baraka kocha Fadlu katika maisha yake ya soka nje Simba,” imefafanua taarifa hiyo ya Simba.