Pyramids mabingwa Afrika, Mayele akiibuka mfungaji bora

Muktasari:
- Timu nne za Misri zimechukua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara 18 tofauti, kinara ikiwa ni Al Ahly iliyotwaa ubingwa mara 12.
Pyramids FC ya Misri imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya leo kupata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Matokeo hayo ya leo, yameifanya Pyramids FC kupata ushindi wa jumla wa mabao 3-2 katika mechi mbili za fainali za mashindano hayo msimu huu kufuatia sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Afrika Kusini Mei 24, 2025, jambo ambalo limeihakikishia kuondoka na Kombe na kitita cha Dola 4 milioni (Sh10.8 bilioni).
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Juni 30, Cairo Misri, mabao ya ushindi ya Pyramids FC yalifungwa na Fiston Mayele na Ahmed Samy huku bao la kufutia machozi la Mamelodi Sundowns likipachikwa na Iqraam Rayners.
Katika mchezo huo, Pyramids FC ilifanya mabadiliko ya kuwapumzisha Ramadan Sonhi, Mohamed Chibi, Ibrahim Blati Toure ambao nafasi zao zilichukuliwa na Ibrahim Adel, Ahmed Tawfik na Ali Gabr.
Mamelodi Sundowns iliwatoa Aubley Modiba, Tashreek Matthews, Jayden Adams, Mosa Lebusa na Iqraam Rayners ambao nafasi zao zilichukuliwa na Divine Lunga, Peter Shalulile, Arthur Sales, Thapelo Morena na Lebo Mothiba.
Refa wa mchezo huo alikuwa ni Mohamed Artan kutoka Somalia ambaye alitoa kadi tano za njano, mbili kwa wachezaji wa kila upande na moja kwa kocha wa Pyramids FC, Krunoslav Jurcic.
Wachezaji walioonyeshwa kadi za njano ni Ahmed Atef na Mohamed Chibi wa Pyramids FC na kwa upande sa Mamelodi Sundowns ni Aubley Modiba na Teboho Mokoena.
Kwa Pyramids FC kutwaa taji hilo, Misri inazidi kuboresha rekodi yake ya kuwa nchi ambayo klabu zake zimetwaa mara nyingi taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo zimefanya hivyo mara 18 ikifuatiwa na Morocco iliyofanya hivyo mara saba.
Pyramids FC inakuwa timu ya nne ya Misri kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikifuata nyayo za Al Ahly, Zamalek na Ismaily ambazo zimewahi kufanya hivyo hapo nyuma.
Mamelodi Sundowns ineshindwa kuandika rekodi mpya ya kuwa timu pekee ya Afrika Kusini iliyotwaa mara nyingi ubingwa wa mashindano hayo na badala yake imeendelea kuwa sambamba na Orlando Pirates zikiongoza kutwaa ubingwa huo kila moja ikiwa na taji moja.
Hata hivyo Mamelodi Sundowns inaondoka na kifuta jasho cha Dola 2 milioni (Sh5.4 bilioni) kwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo.
Habari njema zaidi kwa Pyramids FC ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele kumaliza akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo baada ya kupachika mabao sita.
Ikumbukwe kuwa Mayele katika msimu wa 2022/2023 aliibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akipachika mabao saba.