Mayele aipa wakati mgumu Mamelodi

Muktasari:
- Mayele amefunga mabao matano akishika nafsi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora msimu huu akilingana na Emam Ashour wa Al Ahly anayeshika nafasi ya kwanza.
Pretoria, Afrika Kusini. Mshambuliaji wa Kimataifa wa DR Congo anayekipiga kwenye Klabu ya Pyramids ya Misri, Fiston Mayele amezidi kuwapa wakati mgumu wapinzani wao katika kuelekea mchezo wa kwanza wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo huo utakaofanyika kesho jumamosi, Mei 24 kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria Afrika Kusini, beki wa Mamelodi, Mosa Lebusa amekiri kuwa mshambuliaji wa Pyramids, Fiston Mayele ni mchezaji mzuri lakini timu yao haijafanya maandalizi ya kumkaba Mcongo huyo pekee bali timu nzima:
"Mayele ni mchezaji mzuri sana, lakini sisi hatuangalii mchezaji mmoja tu, tunaiangalia timu yote kwa ujumla.
"Kwa upande wetu, tunataka tu kuwazuia Pyramids wasikaribie eneo letu la hatari na kuhakikisha tunapunguza nafasi zao za kufunga mabao.
"Tunajua kuwa karibu na eneo la hatari, Mayele ni hatari sana, na hilo ndilo jambo tunaloliangalia. Tunatumai tutafaulu na kuhakikisha tunapata faida," amesema Lebusa, beki wa Sundowns.

Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Pyramids imefunga jumla ya mabao 22 ambapo kati ya hayo Mayele amefunga mabao matano akionekana kuwa tishio zaidi katika safu ya ushambuliaji ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na kocha, Krunoslav Jurčić, raia wa Croatia.
Baada ya mchezo wa kesho kutakuwa na mwingine wa marudiano ambao umepangwa kuchezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa 30 June huko Misri.