Partey mbioni kuondoka Arsenal

Muktasari:
- Partey alijiunga na Arsenal kwa dau la Pauni milioni 45 (Sh155 bilioni) akitokea Atlético Madrid.
London, England. Kiungo mkabaji raia wa Ghana, Thomas Partey, anaripotiwa kuwa mbioni kuondoka Arsenal msimu huu wa joto baada ya mazungumzo ya kuongezewa mkataba wake kusimama kabisa, hali inayotafsiriwa kuwa mwisho wa safari yake ndani ya klabu hiyo ya Ligi Kuu England.
Kwa mujibu wa taarifa ya ESPN, mkataba wa Partey umemaliza jana, lakini pande zote hazijafikia muafaka juu ya kuendelea naye, licha ya juhudi zilizofanywa.

Partey alijiunga na Arsenal kwa dau la Pauni milioni 45 (Sh155 bilioni) akitokea Atlético Madrid katika dakika za mwisho za dirisha la usajili Oktoba 2020. Tangu wakati huo, ameichezea Arsenal mara 167, akifunga mabao tisa.

Ingawa alipitia kipindi kigumu cha majeruhi msimu wa 2023/24, Partey alirejea kwa kasi na kuwa mhimili muhimu kwenye safu ya kiungo cha kocha Mikel Arteta, akiisaidia timu kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu iliopita.
Hata hivyo, akiwa Arsenal hajafanikiwa kutwaa kombe lolote kubwa, isipokuwa Ngao ya Jamii mwaka 2023 dhidi ya Manchester City kwa njia ya mikwaju ya penalti.

Kwa sasa, Arsenal inatajwa kuwa katika hatua za mwisho za kufanikisha usajili wa kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi, kwa dau la Pauni milioni 51 (Sh175 bilioni), ambaye anaonekana kama mbadala wa Partey.
Akizungumzia hatma yake, Partey alieleza kuwa uamuzi wa wapi ataelekea utategemea zaidi ustawi wa familia yake:
"Nafikiri jambo la kwanza ni wapi unahisi furaha na nyumbani. Mwisho wa siku, huu ni mchezo ambao umecheza kwa muda mrefu, lakini pia familia inahitaji maisha bora. Hatuzidi kuwa vijana na kwa sasa kuna mambo mengi ya kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi."

Pia alieleza kuwa yeye ni shabiki wa Arsenal na hawezi kufanya maamuzi binafsi:
"Mimi ni shabiki wa Arsenal, siwezi kuamua lolote peke yangu. Nawaachia mawakala wangu na klabu. Mimi ninachotaka ni kufurahia mpira."
Katika msimu uliomalizika, Partey hakucheza mechi tatu tu za EPL, akifunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao. Alipoulizwa kama huo ulikuwa msimu bora zaidi kwake, amesema:
“Naamini kwa wale wanaoangalia upatikanaji wa mchezaji, wangesema ndiyo. Kila wakati ninapopata nafasi ya kucheza, huwa ninatoa uwezo wangu wote.”

Kocha Mikel Arteta pia amewahi kusisitiza umuhimu wa Partey kikosini:
“Kwa upande wa uthabiti, huu umekuwa msimu bora kwake. Upatikanaji wake umeongeza uimara kikosini, na ni mchezaji muhimu sana kwetu. Ndio, natamani aendelee kuwepo.”
Hata hivyo, dalili zote zinaonesha kuwa Partey anaelekea kuondoka Emirates, ikiwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayoendelea chini ya uongozi mpya wa safu ya benchi la ufundi. Endapo dili la Zubimendi litakamilika, basi safari ya Partey London Kaskazini huenda ikafikia tamati rasmi.