Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal yakamilisha dili la kumsajili kiungo wa Brentford

Muktasari:

  • Nørgaard, mwenye umri wa miaka 31, atasajiliwa rasmi baada ya kufanyiwa vipimo vya afya, huku makubaliano binafsi kati yake na Arsenal yakitarajiwa kukamilika bila vikwazo.

London, England. Klabu ya Arsenal imekamilisha makubaliano ya kumsajili nahodha wa Brentford na kiungo mkabaji wa kimataifa wa Denmark, Christian Nørgaard kwa dau la pauni milioni 10 sawa na Sh37 bilioni za Kitanzania, ambalo linaweza kuongezeka hadi kufikia pauni milioni 15 sawa na Sh55 bilioni kutokana na nyongeza mbalimbali.

Usajili huu unakuja baada ya klabu hiyo ya London Kaskazini kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na Thomas Partey, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu. Ingawa kuna uwezekano mdogo wa mazungumzo ya dakika za mwisho, hatua ya Arsenal kumalizana na Nørgaard ni ishara ya wazi kuwa hawataki kuwekwa mateka na madai ya mishahara mikubwa.

Taarifa zinasema kuwa Nørgaard, mwenye umri wa miaka 31, atasajiliwa rasmi baada ya kufanyiwa vipimo vya afya, huku makubaliano binafsi kati yake na Arsenal yakitarajiwa kukamilika bila vikwazo. Hii ni ndoto inayotimia kwa kiungo huyo ambaye ameiongoza Brentford kwa mafanikio makubwa tangu alipowasili mwaka 2019.

Nørgaard alikuwa amesaini mkataba mpya wa miaka miwili na Brentford mwezi Machi mwaka huu, akiamua kubaki kutokana na kutaka kuendeleza maisha ya kifamilia jijini London licha ya kuwa kwenye rada ya klabu kubwa ya Ureno, Benfica. Hata hivyo, fursa ya kujiunga na Arsenal klabu yenye nafasi ya kupigania mataji na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya imekuwa kivutio kikubwa kwake.

Kocha Mikel Arteta amekuwa akihitaji kuongeza uzoefu katika eneo la kiungo, hasa baada ya kuondoka kwa Jorginho, ambaye tayari amejiunga na Flamengo ya Brazil. Nørgaard anatarajiwa kushirikiana na Declan Rice na mchezaji mpya anayetarajiwa kuwasili, Martin Zubimendi kutoka Real Sociedad ambaye dau lake linaelezwa kufikia pauni milioni 55 katika eneo la katikati la uwanja.

Kwa upande mwingine, kuondoka kwa Nørgaard ni pigo jingine kwa Brentford, ambao tayari wamepoteza kocha wao mkuu Thomas Frank pamoja na sehemu ya benchi lake la ufundi waliokwenda Tottenham Hotspur. Aidha, mshambuliaji Bryan Mbeumo yuko mbioni kujiunga na Manchester United kwa dau la pauni 60 milioni  sawa na Sh220 bilioni, ingawa Frank alitaka kumchukua kwenda Spurs.

Frank pia alikuwa na nia ya kumrejesha Nørgaard, aliyewahi kucheza chini yake katika kikosi cha vijana cha Denmark na pia Brøndby, lakini Arsenal wamekamilisha mpango huo kwa haraka na kwa bei wanayoona kuwa ni ya haki kwa mchezaji mwenye uzoefu mkubwa wa EPL na anayefaa katika mfumo wa Arteta.

Mkurugenzi mpya wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta kwa kushirikiana na Arteta, wameweka wazi dhamira ya kufanya biashara kubwa msimu huu wa joto, huku wakiwa na matarajio makubwa ya kuboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu wa 2025/26.