Mzize, Mayele kiboko ya Waarabu Tuzo za CAF
"Habari za jioni mabibi na mabwana, jina langu ni Asamoah Gyan, nipo na Manucho. Tupo hapa kutangaza Tuzo ya Bao Bora la Mwaka 2025. Na mshindi ni Clement Mzize."
Hayo yalikuwa maneno ya wanasoka wa zamani Afrika, Asamoah Gyan, mshambuliaji raia wa Ghana aliyewahi kutamba na klabu kadhaa Ulaya ikiwamo Sunderland na Mateus Alberto Contreiras Gonçalves maarufu Manucho, mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Angola na Manchester United wakati wakimtangaza mshambuliaji wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Clement Mzize kuwa ndiye mshindi wa Tuzo ya Bao Bora la Mwaka la CAF 2025, katika hafla iliyofanyika Novemba 19, 2025, Rabat nchini Morocco.
Mzize ametwaa tuzo hiyo kutokana na bao alilofunga msimu wa 2024-2025 katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Januari 4, 2025.
Bao hilo la Mzize, lilikuwa la kusawazisha dakika ya 30, baada ya TP Mazembe kutanguliwa dakika ya 16 kwa mkwaju wa penalti. Siku hiyo Mzize alipachika mabao mawili, lingine likifungwa na Aziz Ki.
Mzize kabla ya kufunga bao hilo, alipokea pasi kutoka kwa Chadrack Boka, mbele kidogo mwa mstari unaogawa uwanja, akiwa umbali mrefu akitokea upande wa kushoto kuelekea goli la kusini, akaingia ndani kidogo kisha akaachia shuti kali na mpira kujaa nyavuni.
Katika kinyang'anyiro hicho, Mzize alikuwa akishindana na wenzake 12 lakini kura zilizopigwa na mashabiki, zimempa ushindi huo.
Katika mchakato wa kulisaka bao bora, CAF ilitangaza wachezaji 13 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo ambapo mashabiki wakapewa nafasi ya kuchagua mshindi.
Orodha hiyo iliandaliwa na Kamati Maalum ya Ufundi ya CAF ambapo kura zilianza kupigwa Novemba 6, 2025 na kufungwa Novemba 12, 2025.
Kwa mujibu wa CAF, kura za mashabiki zinachangia asilimia 100 ya matokeo ya mwisho, tuzo hiyo ndiyo pekee inayotegemea kura za mashabiki.
Mzize ameibuka mshindi mbele ya Abdellah Ouazane (Morocco vs Tanzania-AFCONU17), Anas Roshdy (Misri vs Afrika Kusini -AFCONU17), Asharaf Tapsoba (Burkina Faso vs Cameroon-AFCONU17), Barbra Banda (Zambia vs Morocco-WAFCON2024).
Wengine ni Calvin Fely (Madagascar vs Morocco-CHAN2024), Ghizlane Chebbak (Morocco vs Nigeria-WAFCON2024), Ibrahim Adel (Pyramids vs ES Tunis-Ligi ya Mabingwa), Jean-Claude Girumugisha (Al Hilal SC vs MC Alger-Ligi ya Mabingwa).
Pia kuna Ndabayithethwa Ndlondlo (Afrika Kusini vs Uganda-CHAN2024), Oussama Lamlioui (Morocco vs Madagascar-CHAN2024), Refiloe Jane (Afrika Kusini vs Mali-WAFCON2024) na Soufiane Bayazid (Algeria vs Uganda-CHAN2024).
Baada ya kushinda tuzo hiyo, Mzize amesema: "Habari za wakati huu, kwa majina naitwa Clement Mzize, ninawashukuru sana CAF kwa kunipa tuzo hii, naamini ni chachu kwangu, imeniongezea thamani na kitu kikubwa katika maisha yangu ya soka.
"Ninawashukuru pia wachezaji wenzangu kwa kupambana kuweza kupata tuzo hii, naamini hii ni ya kwetu wote. Ninawashukuru sana benchi la ufundi. Ninawashukuru sana viongozi. Ninawashukuru sana mashabiki kwa kunipigia kura na kupata tuzo hii ya goli bora la msimu. Mwenyezi Mungu awabariki sana. Nashukuru."
Wakati Mzize akibeba tuzo hiyo, Morocco imeandika historia mpya katika soka la Afrika baada ya nyota wake wawili, Achraf Hakimi na Ghizlane Chebbak, kutwaa tuzo za juu kabisa za CAF.
Hakimi, beki wa Paris Saint-Germain, ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa upande wa wanaume baada ya mwaka 2025 kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup, Ligue 1, Coupe de France na kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu la FIFA 2025.
Mmorocco huyo pia ameliongoza taifa hilo kufuzu Kombe la Dunia 2026, na kuwa beki wa kwanza kushinda tuzo hiyo tangu Bwanga Tshimen mwaka 1973.
Hakimi amewashinda Mohamed Salah wa Misri na klabu ya Liverpool na mshindi wa tuzo hiyo mwaka 2023, Mnigeria, Victor Osimhen anayecheza Galatasaray.
Kwa upande wa wanawake, Ghizlane Chebbak ameng’ara kwa kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika, ikiwa mara ya kwanza kwa mwanasoka wa kike kutoka Morocco. Chebbak alimaliza WAFCON ya 2025 kama mfungaji bora na kuipa Morocco nafasi ya pili kabla ya kujiunga na Al-Hilal ya Saudi Arabia.
Tuzo nyingine kubwa zilionyesha utawala wa Morocco katika hafla hiyo, ambapo kipa Yassine Bounou alitwaa Tuzo ya Kipa Bora wa Afrika kwa wanaume, huku chipukizi Othmane Maamma akipewa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi baada ya kuisaidia Morocco kushinda Kombe la Dunia la Vijana U-20 mwaka 2025. Doha El Madani naye alitetea taji la Mchezaji Bora Chipukizi kwa wanawake.
Timu ya taifa ya vijana ya Morocco (U-20) imetajwa Timu Bora ya Mwaka Wanaume, baada ya ubingwa wa dunia, wakati Nigeria (Super Falcons) ikitwaa Tuzo ya Timu Bora ya Mwaka Wanawake.
Katika tuzo za klabu, Pyramids ya Misri imenyakua Tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka kwa wanaume baada ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza, huku mshambuliaji wao Fiston Mayele akitunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Klabu.
Katika upande wa marefa, Omar Abdulkadir wa Somalia ametwaa Tuzo ya Refa Bora wa Mwaka kwa wanaume, huku Shamirah Nabadda wa Uganda akitwaa tuzo kwa upande wa wanawake.
REKODI NA MAAJABU YA BAO LA MZIZE
Kitendo cha Mzize kushinda Tuzo ya Bao Bora la Mwaka CAF, imemfanya kuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo. Pia ni Mtanzania wa pili kutunukiwa tuzo na CAF katika sherehe zake za kila mwaka baada ya Mbwana Samatta kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika Mwaka 2015 anayecheza ligi ya ndani alipokuwa akiitumikia TP Mazembe ya DR Congo.
Pia Mzize anakuwa mchezaji wa pili anayecheza Ligi Kuu Bara kutunukiwa Tuzo ya Bao Bora la CAF baada ya Pape Ousmane Sakho kufanya hivyo mwaka 2022 akiwa na Simba.
Si unakumbuka Sakho bao lake lile la kubinuka 'acrobatic' dhidi ya ASEC Mimosa pale Benjamin Mkapa ndilo lilimpa tuzo mwaka 2022. Basi Mzize naye kupitia uwanja huohuo na goli la upande uleule aliofunga Sakho, limempa tuzo. Haya ni maajabu.
USHINDI ULIOMBEBA MAYELE
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa DR Congo, ametoa mchango wa hali ya juu kwa klabu ya Pyramids iliyotwaa mataji matatu makubwa ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika, CAF Super Cup na Kombe la FIFA la African-Asian-Pacific.
Mbali na mchango wake wa kubeba mataji hayo, nyota huyo wa zamani wa Yanga, amemaliza msimu wa 2024-2025 akiwa mfungaji kinara kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga mabao sita yaliyokuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha Pyramids kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Pia Mayele alifunga mabao matatu yaliyoiwezesha Pyramids kutwaa ubingwa wa Kombe la FIFA la African-Asian-Pacific katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Al Ahli ya Saudi Arabia, Septemba 25, 2025.
Oktoba 18, 2025, Mayele akafunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 ilioupata Pyramids mbele ya RS Berkane na kubeba taji la CAF Super Cup.
Mayele amemshinda mchezaji mwenzake wa Pyramids, Mohamed Chibi raia wa Morocco ambaye ni beki wa kulia. Mwingine ni mshambuliaji wa RS Berkane na timu ya taifa ya Morocco, Oussama Lamlioui ambaye alifunga mabao matano yaliyoisaidia RS Berkane kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024-2025. Pia alikuwa na mchango wa kuisaidia RS Berkane kushinda taji lao la kwanza la Botola Pro 2024-2025.
Lamlioui pia aliiwezesha Morocco kutwaa taji la CHAN 2024, akiibuka pia mfungaji bora wa mashindano hayo akipachika mabao sita.
ORODHA YA WASHINDI
1.Mchezaji Bora – Wanaume: Achraf Hakimi (Morocco/PSG)
2.Mchezaji Bora – Wanawake: Ghizlane Chebbak (Morocco/Al-Hilal)
3.Kipa Bora – Wanaume: Yassine Bounou (Morocco/Al-Hilal)
4.Kipa Bora – Wanawake: Chiamaka Nnadozie (Nigeria/Brighton)
5.Mchezaji Bora wa Klabu – Wanaume: Fiston Mayele (DR Congo/Pyramids)
6.Chipukizi Bora – Wanaume: Othmane Maamma (Morocco/Watford)
7.Chipukizi Bora – Wanawake: Doha El Madani (Morocco/AS FAR)
8.Kocha Bora – Wanaume: Bubista (Cape Verde)
9.Timu Bora ya Mwaka – Wanaume: Morocco U-20
10.Timu Bora ya Mwaka – Wanawake: Nigeria
11.Klabu Bora – Wanaume: Pyramids (Misri)
12.Bao Bora la Mwaka: Clement Mzize (Yanga)
13.Refa Bora – Wanaume: Omar Abdulkadir (Somalia)
14.Msaidizi Bora wa Refa – Wanaume: Liban Abdoulrazack (Djibouti)
15.Refa Bora – Wanawake: Shamirah Nabadda (Uganda)
16.Msaidizi Bora wa Refa – Wanawake: Tabara Mbodji (Sene