Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzize ashinda tuzo ya Bao Bora la mwaka la CAF

Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ameshinda tuzo ya Mfungaji wa Bao Bora la Mwaka 2025 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mzize ametangazwa Mshindi wa kipengele hicho katika hafla ya utoaji tuzo hizo inayoendelea Rabat, Morocco leo Jumatano, Novemba 19, 2025.

Bao hilo ni lile alilofunga dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/2025 uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Januari 4, 2025. Katika mchezo huo, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mzize ameibuka mshindi mbele ya Abdellah Ouazane, Anas Roshdy, Asharaf Tapsoba, Barbra Banda, Calvin Fely, Ghizlane Chebbak, Ibrahim Adel, Jean Claude, Ndabayithethwa Ndlonolo, Refiloe Jane, Oussama Lamlioui na Soufiane Bayazid.

Hii ni mara ya pili tuzo hiyo inakuja kwenye Ligi ya Tanzania kwani mara ya mwisho alishinda Pape Osmane Sakho akiwa na Wekundu wa Msimbazi, Simba mwaka 2022.

New Content Item (1)

Mayele Mchezaji Bora wa ndani wa CAF 2025

Mshambuliaji wa Pyramids FC, Fiston Mayele ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ndani ya Afrika ya CAF 2025.

Mayele ameshinda tuzo hiyo mbele ya Oussama Lamlioui wa RS Berkane ya Morocco na Mohamed Chibi wa Pyramids FC.

Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa DR Congo aliibuka Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu wa 2024/2025 akifunga mabao sita.

New Content Item (1)

Pyramids Klabu Bora Afrika 2025

Pyramids ya Misri imeshinda tuzo ya CAF ya Klabu Bora Afrika 2025.

Timu hiyo imeshinda mbele ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na RS Berkane ya Morocco.

Katika mwaka huu, timu hiyo imechukua Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la FIFA la Mabara na Taji la CAF Super Cup.

New Content Item (1)

Morocco yatamba tuzo za CAF 2025 vijana

Timu ya Taifa ya Vijana ya Morocco chini ya Umri wa miaka 20, imeshinda Tuzo ya Timu Bora ya Soka ya Kiume ya CAF 2025.

Morocco U20, ilitwaa taji la Kombe la Dunia la Vijana chini ya Umri huo mwezi uliopita ikiichapa Argentina kwa mabao 2-0 katika Fainali.

Mchezaji wa timu hiyo, Othmane Maama ameibuka Mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora Mdogo wa Kiume huku Doha El Madani akishinda Tuzo ya Mchezaji Bora Mdogo wa Kike.

Kwa upande mwingine, Timu ya Taifa ya Wanawake ya Nigeria, imeshinda Tuzo ya Timu Bora ya Taifa ya Wanawake ya CAF 2025.

New Content Item (1)

Rais Samia atunukiwa tuzo CAF

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Tuzo ya Maalum na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kutambua mchango wake katika mchezo wa soka.

Tuzo hiyo imekabidhiwa leo Jumatano, Novemba 19, 2025 jijini Rabat, Morocco ilikofanyika hafla ya Tuzo za CAF 2025.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa serikali, Gerson Msigwa ndio amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Samia.

New Content Item (1)

Hakimi Mchezaji Bora Afrika 2025

Beki wa Morocco anayeitumikia PSG ya Ufaransa, Achraf Hakimi, ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Afrika wa CAF 2025.

Katika hafla za utoaji wa tuzo hizo leo, Rabat, Morocco, Hakimi ametangazwa mshindi akiwapiku Mohamed Salah wa Liverpool na Misri pamoja na Victor Osimhen wa Nigeria na Galatasaray.

Katika mwaka huu, Hakimi ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu Ufaransa, Kombe la Ufaransa na ameiongoza Morocco kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Kwa upande wa Wanawake, Mchezaji Bora Afrika 2025 ni Ghizlane Chebbak wa Morocco na Klabu ya Al Hilal.