Prime
MZEE WA FACT: Isamuhyo Uwanja wa tano kuwakutanisha Watani wa Jadi Dar
Muonekano wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambao utatumika katika mchezo wa Ligi Kuu utakaowakutanisha Watani wa Jadi, Simba na Yanga, Mei 3, 2026. Picha na Mtandao
Mei 3, 2026, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo utakuwa wa tano jijini Dar es Salaam kuandaa mechi ya Watani wa Jadi.
Nimetumia jina la WATANI WA JADI kwa sababu ndio jina rasmi la mchezo huu kwa miaka mingi sio Kariakoo Dabi.
Na ndio maana nimeliandika jina hilo kwa herufi kubwa, kuonyesha msisitizo. Ni kuishusha thamani mechi hii kwa kuitangaza kwa kutumia neno Dabi hili ni neno jepesi ambalo tafsiri yake ni ndogo tu mechi baina ya timu mbili zinazotoka eneo moja la kijiografia.
Bila kujali historia zao, ushindani wao wala utamaduni wao ni kutoka eneo moja tu, basi! Lakini hebu tuachane na hilo, turudi kwenye hoja ya msingi. Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo unaomilikiwa na klabu ya JKT Tanzania utakuwa wa tano katika ardhi ya Dar es Salaam kushuhudia Watani wa Jadi wakipepetana.
UWANJA WA KWANZA
Historia ya Watani wa Jadi inarudi nyuma hadi 1936 pale klabu ya kwanza ya Waafrika watupu, New Young Sports Club, iliposhuka daraja kwenye ligi ya Dar es Salaam kutoka la kwanza hadi la pili.
Baadhi ya wachezaji na wanachama walilalamika kwamba uongozi wa klabu yao ulifuja pesa za klabu na kushindwa kuisimamia vizuri hadi ikashuka daraja.
Watu hao wakakutana kwenye mtaa wa Stanley ambao sasa ni Aggrey, pale Kariakoo. Wakakubaliana wajitenge na kuanzisha klabu yao, wakaiita Stanley FC, kwa kuchukua jina la mtaa wao.
Wale waliobaki, wakapinga kushindwa kuisimamia timu, wao walilalamikia uonevu wa waamuzi ambao walikuwa wazungu, kuionea timu yao. New Young ndio ilikuwa timu pekee ya wazawa, zingine zote zilikuwa za wageni wazungu, waarabu, wahindi.
Baada ya wenzao kujitenga, na wao wakabadili jina kutoka New Young SC na kuwa Young Africans SC. Utengano huu ndio ulioleta upinzani...kwa sababu kila upande ulitaka kumuonesha mwanzake kwamba wao wako vizuri. Wakati huo kulikuwa na madaraja mawili tu ya ligi, la kwanza na la pili.
Timu mpya zote zilianzia daraja la pili ndiko walikoanzia Stanley FC. Na ndiko walikopaswa kuwepo Young Africans kwa kuwa walishuka kutoka daraja la kwanza. Lakini hata hivyo, walikataa kushiriki ligi hiyo kwa kile walichosema waamuzi walikuwa wanawaonea.
Wakaanzisha harakati za kuwa na ligi ya Waafrika watupu, na kujitoa kwenye ligi ya wazungu. Wakagoma kushiriki ligi hadi 1938 walipokubali baada ya mabadiliko mengi ya mfumo wa ligi na uongozi wa chama cha soka na Bodi ya Ligi.
Kwa mara ya kwanza timu hizi zilikutana 1939. Mwaka huo ndio Stanley FC ilibadili jina na kuwa Sunderland FC, baada ya kuungana na Arab Sports Club. Mechi hii ilifanyika kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja ambao sasa ni Kidongo Chekundu. Wakati huo ule ndio ulikuwa uwanja mkubwa wa mpira mjini Dar es Salaam.
UWANJA WA PILI
Mwaka 1942 mpira ukahamia Uwanja wa Ilala, ambao sasa ni Karume. Hapo zikafanyika mechi za Watani wa Jadi kwa awamu mbili. Awamu ya ligi ya Dar es Salaam iliyoanza 1929 na awamu ya ligi ya taifa, iliyoanza 1965.
Mechi ya mwisho ya ligi ya Dar es Salaam ilifanyika 1964, ambapo Simba wakati huo iliitwa Sunderland ilishinda 4-3 huku Khamis Kilomoni wa Simba akifunga mabao matatu (hat trick).
Ile stori ya Abdallah Kibaden kuwa mchezaji pekee kufunga mabao matatu, ni katika ligi ya taifa iliyoanza 1965. Ni bahati mbaya sana kwamba historia ya ligi yetu kabla ya 1965, imefutwa.
Awamu ya pili ni ya ligi ya taifa iliyoanza 1965 WATANI WA JADI walikutana katika mechi iliyoshindwa kumalizika. Mechi hii mbayo ndio hutajwa kama ya kwanza, ilifanyika Juni 7, 1965 lakini ilivunjika huku Yanga wakiongoza 1-0 kwa bao la Mawanzo Shomvi.
UWANJA WA TATU
Mwaka 1968 mechi za Watani Jadi zilihamishwa kutoka Uwanja wa Ilala hadi Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru). Mechi ya kwanza ilifanyika Juni Mosi, 1968 na Yanga ilishinda 5-0.
Japo mechi zingine za ligi ziliendelea kuchezwa Ilala, ni mechi ya Watani wa Jadi tu ndio ilihamia Uwanja wa Taifa.
UWANJA WA NNE
Miaka ya 2000 serikali ilijenga uwanja mpya wa taifa, na ule uliokuwa wa taifa ukaitwa Uwanja wa Uhuru. Uwanja mpya wa taifa ambao sasa ni Uwanja wa Mkapa, ulianza kutumika kwa mechi za Watani wa Jadi mwaka 2008.
Mchezo huo uliofanyika Oktoba 26, 2008, ulishuhudia Yanga wakishinda 1-0 kwa bao la Ben Mwalala. Huu ulikuwa ushindi wa kwanza wa Yanga dhidi ya Simba kwa miaka minane.
Baada ya viwanja vyote hivyo, sasa ni zamu ya Meja Jenerali Isamuhyo.
VIWANJA VYA NJE YA DAR ES SALAAM
1. DODOMA
Yanga 3-1 Simba 1959
Hii ilikuwa mechi ya kirafiki na ya kwanza kabisa kwa Watani wa Jadi kucheza nje ya Dar es Salaam. Yanga 1-0 Simba 1997
Ligi Kuu ya Muungano
2. MWANZA
Mechi za Watani wa Jadi zimefanyika mara sita mjini Mwanza.
Yanga 2-1 Simba 1974
Ligi ya taifa
Maarufu kama Nyamagana Thriller kwa sababu ilifanyika Uwanja wa Nyamagana. Ilifanyika Agosti 10, 1974 na kuandika historia kama mechi ya kwanza ya ligi kufanyika nje ya Dar es Salaam.
Yanga 2-0 Simba 1996
Fainali Kombe la Tusker
Yanga 3-0 Simba 2003
Fainali Kombe la AICC
Simba 2-0 Yanga 2005
Fainali Kombe la Tusker
Yanga 1-0 Simba 2010
Ligi Kuu
Yanga 1-0 Simba 2022
Kombe la Shirikisho la Azam Sports
3. ZANZIBAR
WATANI WA JADI wamekutana mara 7 kwenye uwanja wa Amaan Zanzibar
Yanga 2-0 Simba 1975
Fainali 'Kagame Cup'
Simba 1-1 Yanga (penati 6-5) 1992
Fainali 'Kagame Cup'
Yanga 0-1 Simba 1992
Fainali Ligi ya Muungano
Simba 2-0 Yanga 2011
Fainali Mapinduzi Cup
Simba 0-0 Yanga (penalti 4-2) 2017
Nusu fainali Mapinduzi Cup
Simba 0-0 Yanga (penalti 3-4) 2021
Fainali Mapinduzi Cup
Simba 0-0 Yanga 2026
Ligi Kuu
4. ARUSHA
Mechi ya safari hii ilitajwa kwamba ingefanyika Arusha kabla haijatangazwa kufanyika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kama ingefanyika Arusha, ingekuwa kwa mara ya tatu.
Yanga 4-4 Simba 1996, Ligi Kuu
Yanga 2-1 Simba, Fainali mkondo wa kwanza Kombe la FAT 2000
5. MBEYA
Yanga 1-1 Simba 1997, Ligi ya Muungano
6. KIGOMA 2021, Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports
7. TANGA, Yanga 0-0 Simba (penalti 1-3) 2023