Prime
MZEE WA FACT: Ugumu wa ligi msimu huu uko hapa
Ligi kuu ya NBC msimu huu wa 2025/26 imeamirika na kuwa na ushindani mkubwa zaidi kuliko msimu uliopita na hata msimu mingi ya nyuma.
Hii ni kwa mujibu wa takwimu za matokeo ya uwanjani, hasa za timu mbili kubwa za Yanga na Simba ambazo zimetawala mpira wa Tanzania kwa miaka na mikaka, miongo na milongo!
Timu nyingi za chini zimefanikiwa kuchukua alama nyingi zaidi kwa vigogo hawa tofauti na msimu uliopita, na misimu mingine mingi ya nyuma.
Hadi tukiwa katika raundi ya 18, kabla ya ligi kusimama kupisha hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB, hakuna timu ambayo haijadondosha angalau alama 10.
Hii ni tofauti kabisa na msimu uliopita wa 2024/25.
Vigogo Yanga na Simba walikuwa na matokeo bora zaidi hadi mwisho wa msimu, kulinganisha na msimu huu hadi sasa.
1. MABINGWA YANGA SC
Walimaliza ligi wakiwa na alama 82 kati ya alama 90 ambazo wangeweza kuzipata endapo wangeshinda mechi zote.
Maana yake ni kwamba waliangusha alama nane tu msimu mzima...pata picha!
Walipoteza mechi mbili, na kupata sare moja.
Yanga 0-1 Azam FC
Yanga 1-3 Tabora United
JKT Tanzania 0-0 Yanga SC
Japo msimu huu hadi sasa raundi ya 18 hawajapoteza mchezo wowote, lakini wameshadondosha alama 10 baada ya kupata sare 5.
Mbeya City 0-0 Yanga
TRA United 0-0 Yanga
Azam FC 0-0 Yanga
Mtibwa Sugar 1-1 Yanga
Yanga 0-0 Simba
Bado kuna mechi 12 yawezekana wakadondosha alama zingine nyingi zaidi huko mbele.
2. MAKAMU BINGWA SIMBA SC
Walimaliza ligi wakiwa na alama 78 kati ya 90 ambazo wangeweza kuzipata endapo wangeshinda mechi zote 30 za msimu. Mana yake waliangusha alama 12 tu msimu mzima.
Simba 0-1 Yanga
Yanga 2-0 Simba
Simba 2-2 Azam FC
Simba 2-2 Coastal Union
Fountain Gate 1-1 Simba
Msimu huu hadi sasa wamedondosha alama 15 baada ya kupoteza mechi moja na kupata sare sita.
Simba 1-1 Mtibwa Sugar
Yanga 0-0 Simba
Dodoma Jiji 0-0 Simba
Azam FC 0-0 Simba
Pamba 1-1 Simba
TRA United 0-0 Simba
Simba 0-2 Azam FC
Bado kuna mechi 13 yawezekana wakadondosha alama nyingine nyingi zaidi huko mbele.
NI UBORA WA LIGI
Kitendo cha Yanga na Simba ambazo ni kilelezo cha mpira wetu kudondosha alama nyingi ni kiashiria cha kuimarika kwa timu zingine ambazo msimu uliopita na hata nyuma zaidi zilikuwa mteremko wa vigogo hawa.
Timu hizo msimu huu zimeimarika na kuwa bora kiasi cha kusimama imara na kubishana na vigogo.
Hata mechi ambazo vigogo hawa wameshinda, hazikuwa nyepesi kwao...walipata ushindani mkali sana uwanjani na hata kushangilia sana baada ya filimbi ya mwisho.
Huu ndio ubora wa ligi...timu yoyote inaweza kuangusha alama wakati wowote.
Hakuna timu yenye uhakika wa kushinda mechi yoyote....wakati wowote chochote kinaweza kutokea.
Sare tatu mfululizo za Yanga, dhidi ya Azam FC, dhidi ya TRA United na baadaye dhidi ya Mtibwa, zikawalazimu kuimarisha benchi la ufundi kwa kumuongeza Abdihamid Moallin kama kocha msaidizi.
Lakini hata kabla ya hapo, walilalamikia ratiba, sio tu kwa mechi kubanana, bali kupangiwa Azam na TRA United kwa mfuatano.
Hii peke yake ilikuwa ishara kwamba macho yaliwabadilika na kuwa mekundu kutokana na ugumu wa ligi.
Simba imefikia wakati wanalalamikia mechi ya Azam FC kuhamishwa kutoka Mkapa hadi Chamazi.
Haya yote ni kwa sababu ya matokeo magumu yanayotokana na ubora wa ligi.
Vigogo waliozoea kushinda kiurahisi, sasa wanapata upinzani mgumu hadi akili zinavurugika.
PONGEZI KWA WADAU
I. MAMLAKA
Sifa za kwanza ziende kwa mamlaka za soka, TFF na Bodi ya Ligi. Ubora wa ligi yoyote hutokana na misingi imara ya usimamizi wa ligi yenyewe na mpira kwa ujumla.
Mamlaka zetu hapa nchini, TFF na Bodi ya Ligi, zimejitahidi sana kuifikisha ligi yetu hapa. Miongoni mwa hatua bora walizochukua hadi kuwa hivi sheria ya kusimamia mabenchi ya ufundi.
Ili uwe kocha wa ligi kuu lazima uwe na vigezo vya kufundisha hatua ya makundi ya mashindano ya CAF. Na vigezo vya kufundisha hatua ya makundi ya mashindano ya CAF ni kuwa na leseni A ya CAF, au Pro License ya mabara mengine.
Maana yake makocha wanaofunisha Tanzania ni wa daraja la juu sana. Makocha hawa wamesaidia kuinua uwezo wa wachezaji hivyo ligi kuwa bora kama ilivyo.
II. WADHAMINI
Wadhamini wa haki za matangazo, Azam TV wametoa mchango mkubwa sana kuifikisha hapa ligi yetu.
Pesa ambazo wanatoa kwa vilabu vyetu, zimesaidia sana kupunguza baadhi ya changamoto na kuzifanya timu zimudu angalau kidogo gharama za uendeshaji.
Sasa hivi hakuna tena yale matatizo ya timu kushindwa kufika kituo cha mechi. Na hata ile changamoto ya timu kusafiri usiku mmoja kabla ya mchezo ili wafikie uwanjani moja kwa moja kuepuka gharama za kulala hotelini, nayo imekuwa historia.
Japo changamoto haziishi, lakini kwa kiasi kikubwa zimepungua sana. Wadhamini wa jina, NBC, nao sio wa kuwaacha nyuma hata kidogo.
Tuzo za mchezaji bora wa kila mechi na kila mwezi zimeongeza thamani kubwa sana. Hakuna mchezaji ambaye hapendi kutajwa kama mchezaji bora wa mechi mwisho wa mchezo.
Watu wanapambania ile tuzo, ambayo pia ni nzuri sana hata kwa kuitazama. Haya yote yameongeza thamani ya ligi na kuifanya kuwa bora sana. Bado pia wadhamini binafsi wa vilabu...nao wanafanya kazi nzuri sana.
III. SERIKALI
Hawa ni wadau wakubwa sana wa mpira wetu na hata michezo kwa ujumla. Katika timu 16 za ligi kuu, timu zaidi ya nusu ni za taasisi za serikali.
Maana yake serikali ni wadau wakubwa sana. Lakini zaidi ya hapo, serikali inachangia kwa kiasi kikubwa sana katika uimarishaji wa miundombinu ya mpira.
Iwe serikali kuu kwa kumiliki viwanja kama Mkapa, au Halmashauri kwa kumiliii viwanja kama Tanzanite Kwaraa pale Babati mkoani Manyara.
Uwanja huu umekuwa kimbilio kwa timu mbalimbali baada ya kupata kadhia katika viwnaja vyao vya asili.
CHANGAMOTO
Licha ya ubora wote tulionao, bado kuna changamoto mbili kuu za kutatua. Changamoto hizi zimekuwa donda ndugu kwa mpira wetu, kila mwaka kila msimu.
Nazo ni waamuzi na miundombinu. Hili ndilo eneo ambalo kwa sasa tunatakiwa kuliwekea mkazo kweli kweli ili kuifanya oigi yetu iwe bora zaidi na zaidi.
Makosa ya kibinadamu kwa waamuzi wetu yamekitihiri...mbaya zaidi wanaofadika mara nyingi ni wale wale.
Na kuhusu miundombinu, nadhani mamlaka za soka zinatakiwa kuchukua hatua ngumu kidogo.
Kama ambavyo wametunga sheria ya makocha wa CAF tu kufundisha ligi yetu, basi pia watunge sheria kwamba viwanja vyenye hadhi ya CAF tu ndio vitapewa leseni ya kutumika ligi kuu.
Hii itamsaidia kocha wa CAF kufundisha kwenye viwanja vya hadhi yake.
Mungu ibariki Tanzania