Prime
MZEE WA FACT: Wazo la Makonda na mikasa huko nyuma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Ilikuwa hivi, mwaka 1970, ligi ya Tanzania ilikumbwa na mtikisiko mkubwa sana uliosababisha ishindwe kufanyika kabisa.
Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini, Paul Makonda, ametoa kauli mbili ngumu ambazo historia inaonesha ziliwahi kuleta utata huko nyuma.
Akiongea Machi 28 mwaka huu jijini Arusha alipokuwa akifungua kikao cha maafisa wa michezo na utamaduni, Makonda alisema serikali ina mpango wa mambo mawili makubwa.
1. Kuanzisha ligi ya wazawa watupu.
2. Kuhamasisha mashirika kuanzisha timu.
Sitaki kujadili kwa undani kama ni jambo jema au si jema, bali nataka kutumia nafasi hii kukumbushia mikasa iliyowahi kutokea huko nyuma kwa mawazo kama haya.
LIGI YA WAZAWA WATUPU
Makonda alisema lengo la kuanzisha ligi ya wazawa watupu ni kusaidia kutoa fursa kwa idadi kubwa ya wachezaji wazawa ambayo wamekuwa hawaipati kwenye Ligi Kuu ya NBC.
Tafsiri ya hii ni kwamba serikali ina mpango wa kuanzisha ligi nyingine, tofauti na hii ya NBC.
Wazo kama hili lilikuwepo nchini katika miaka ya mwanzo kabisa ya ligi.
Mpira uliingia nchini baada ya Vita Kuu ya kwanza ya dunia pale Waingereza walipochukua nafasi ya wajerumani kama wakoloni.
Wakaanzisha Ligi ya Wilaya ya Dar es Salaam, mwaka 1921.
Lakini hata hivyo, ligi hii ilishirikisha timu za wageni na wachezaji wa kigeni.
Ni hadi mwaka 1935 pale timu ya kwanza ya wazawa iliporuhusiwa kushiriki.
Timu hiyo iliitwa New Young Sports Club. Ilianzia daraja la pili na mwaka uliofuata yaani 1936 ikishiriki ligi ya juu kabisa, daraja la kwanza.
Lakini ikashuka mwaka huo huo na kusababisha mpasuko ulioigawa na kuzaliwa timu mpya.
Timu ikawa ikawa Stanley FC na baadaye ikajiita Sunderland.
New Young SC nayo ikajibadili jina na kujiita Young Africans.
Hadi hapo kukawa na timu mbili za wazawa, Young Africans na Sunderland.
Lakini timu hizi zilikutana na upinzani mkali kwenye ligi kiasi kwamba zikaanza kufikiria kuanzisha ligi yao ya wazawa watupu.
Walianza na wazo la kuanzisha chama chao cha timu za Waafrika, African Football Association (AFA).
Chama hiki ndio kije kusimamia ligi yao.
Wazo hilo lilianza 1938 na kufika mapema 1939 likapata kasi zaidi.
Wakaitisha mkutano mkubwa wa vilabu vya wazawa uliofanyika ukumbi wa Kariakoo
United Club Hall ili kuanzisha chama chao cha African Football Association (AFA).
Wakamteua meya wa Dar es Salaam, Ahmed Bin Saleh, awe mwenyekiti, Mwinyi Tambwe kuwa katibu mkuu, na Yahya Hassan kuwa mweka hazina.
Viongozi wengine walikuwa Sheikh Ally bin Saleh, Masoud Mwinchande na Mohamed Ally.
AFA ikatangaza kwamba ligi yao wa wazawa ingeanza rasmi Februari 27, 1939.
Chama cha soka cha Dar es Salaam (DFA) ambacho ndio kilikuwa kikisimamia ligi iliyokuwepo, kikaingia hofu kwamba ligi ya wazawa itaiua ligi ya Dar es Salaam.
Ikabidi serikali ya kikoloni iingilie kati kuzima jitihada za wazawa kuanzisha ligi yao.
Ilianza kwa kumteua Meya wa Dar es Salaam ambaye alikuwa anawaunga mkono wazawa na wazo lao la ligi ya wazawa.
Meya huyu aliitwa Gulam Rassul, ndipo wakamleta meya mpya kutoka Tabora, Ahmed
Bin Saleh.
Hii ilifanyika Julai 15, 1938. Meya huyu akapewa kazi maalumu ya kuzuia ligi ya wazawa.
Hata hivyo, na yeye akajikuta kanaswa na harakati za wazawa, akaungana nao na ndiye aliyekuja kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha wazawa (AFA).
Serikali ikakerwa na kumuondoa, na kumleta meya mpya aliyeitwa Muksin.
Mameya wote hawa watatu waliotajwa hapa walikuwa waarabu.
Ni meya Muksin ndiye aliyekuja kufanikiwa kuzima ndoto za wazawa kuanzisha ligi yao.
Alikuja na wazo la wagawanye uwatawale, akaweka mtego wa kuwagawanya vinara wa harakati hizi, Young Africans na Stanley FC.
Alitaka timu mojawapo katika hizi aiunganishe na timu ya Waarabu ya Arab Sports ilishakuwa hivyo maana haitokuwa na wazo la kujitenga tena.
Mtego huo ukainasa Stanley FC na kukubali kuungana Arab Sports Club.
Muungano huu ulifanyika 1939, na kuanzia hapo timu mpya iliyozaliwa ikaitwa Sunderland SC ambayo sasa ni Simba.
Hapo ndipo wazo la kuanzishwa kwa ligi ya wazawa ikafia hapo hapo.
TIMU ZA MASHIRIKA
Makonda alisema kwamba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ameridhia kuyaandikia mashirika yote nchini yawe na timu.
Hadi sasa kwenye ligi kuu zaidi ya nusu ya timu zinamilikiwa na taasisi, idara au mashirika ya serikali.
JKT Tanzania - Jeshi la Kujenga Taifa.
KMC - Halmashauri ya Manispaa Kinondoni
Mbeya City - Halmashauri ya Jiji Mbeya.
Dodoma Jiji - Halmashauri ya Jiji Dodoma.
Pamba Jiji - Halmashauri ya Jiji Mwanza.
Mashujaa FC - Jeshi la Wananchi.
TRA United - Mamlaka ya Mapato.
Namungo - Halmashauri ya Manispaa Ruangwa.
Tanzania Prisons - Jeshi la Magereza.
Na timu zinaweza kuongezeka kutokana na agizo la Waziri Mkuu.
Wazo la timu za mashirika kuja kwa wingi kwenye ligi liliwahi kusababisha ligi kuvunjika.
Ilikuwa hivi, mwaka 1970, ligi ya Tanzania ilikumbwa na mtikisiko mkubwa sana uliosababisha ishindwe kufanyika kabisa.
Wakati huo, mpira wa Tanzania ulikuwa wa ridhaa kwa asilimia 100 kwa maana kwamba wachezaji hawakuwa wakiutegemea kuendesha maisha yao.
Wengi wa wachezaji, kama siyo wote, walikuwa wakifanya kazi kwenye makampuni, mashirika na taasisi mbalimbali huku mpira ambao ulikuwa ukichezwa zaidi na timu za mitaani, ukiwa kama sehemu ya kujifurahisha tu.
Vilabu kama Sunderland (sasa Simba) na Yanga vilikuwa vikiwasajili wachezaji kwa kuwashawishi kwamba vitawatafutia kazi kwenye mashirika kama bandari na kadhalika.
Mwaka huo, FAT ilifungua milango zaidi kwa timu za mashirika na taasisi mbalimbali kama TPDF (Jeshi), Polisi, Magereza, na Cargo (bandari) kushiriki ligi.
Kuruhusiwa kwa timu hizi kukawalazimu wachezaji wa timu za mitaani kama Yanga, Sunderland (Simba) na Cosmopolitan kuamua kuzitumikia timu za kazini kwao na kuziacha timu zao za mitaani.
Hali hiyo ikazifanya timu za mitaani zikose wachezaji na hivyo kujitoa kwenye ligi, zikisema hazina uwezo wa kuziba mapengo ya wachezaji hao.
Kutokana na hilo, FAT kwa kushauriana na chama cha ligi ya soka cha Dar Es Saaam (Dar Es Salaam Football League Association DFLA) na kile cha mkoa wa Pwani (Coastal Region Football Association CRFA) ikaivunja ligi.
Lakini ilikuwa lazima apatikane mwakilishi wa Tanzania kwenye klabu bingwa Afrika, ambayo ndiyo yalikuwa mashindano pekee ya Afrika wakati huo, kwa hiyo wakaiteua Yanga kwa kigezo kwamba ndiyo walikuwa mabingwa wa msimu uliopita, yaani 1969.
Wakati huo, DFLA na CRFA ndizo zilizokuwa na nguvu kuliko hata FAT licha ya kwamba FAT ndicho kilikuwa cha kitaifa.
Uamuzi huo ukapitishwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kuwa rasmi, Yanga wakashiriki klabu bingwa Afrika, 1971.
Kwa hiyo sasa, 2026, Paul Makonda anapotuambia kwamba waziri mkuu ameridhia kuandika barua kwa mashirika, anaturudisha nyuma hadi 1970 ambako hali kama hii ilitokea.