Prime
Mwalimu afichua ugumu wa kutua Simba
Muktasari:
- Nyota huyo wa Tanzania atakuwa na mtihani mwingine wa kupambania nafasi ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na kocha Fadlu Davids.
Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Simba Seleman Mwalimu ameeleza sababu zilizomfanya ajiunge na Wekundu hao wa Msimbazi katika dirisha hili la usajili. Mwalimu maarufu kama Gomez alitambulishwa kujiunga rasmi na Simba Agosti 28, kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Wydad Casablanca ya Morocco.
Akizungumzia kuhusu usajili wake ndani ya klabu ya Simba, Mwalimu alisema amekuja kwa kazi maalumu huku malengo yake sio kurudi tena nyuma bali ni kwenda mbele zaidi.
“Nimekuja kama mwanajeshi aliyeko vitani nina kazi maalumu ambayo nimekuja kuifanya kwa sababu malengo yangu siyo kurudi tena nyuma nataka niende mbele na njia ambayo nimechagua ni kuja hapa, kisha niondoke tena,” alisema.
Sababu kutua Simba
Mwalimu alielezea jinsi usajili wake kuja Simba ulivyokuwa licha ya uongozi wa Wydad kuonesha ugumu wa kumwachia aondoke.
“Wakati nimeenda Wydad nilitoka timu ya daraja la chini ambayo ni Fountain Gate lakini nilivyofika kule niliaminika nikawa nacheza na nilifanya vizuri kila mechi niliyopewa nafasi.
“Kipindi Simba wanatuma ofa ya kunihitaji kocha alikuwa hataki na viongozi walikuwa hawataki. Simba walituma ofa mara mbili na zote zilikataliwa lakini kocha Fadlu aliongea na uongozi wangu na akaonyesha nia ya kunitaka.
“Niliongea na kocha wangu wa Wydad kuhusu kutaka kuondoka, lakini alinikatalia akaniambia bado ananihitaji, nilimwambia nahitaji nafasi ya kutosha kucheza zaidi na ninayopata hapa, alinikubalia kwakuwa bado nina miaka minne ya kucheza Wydad, kwa hiyo mimi ndiyo nilifanya mambo yakawa rahisi,” alisema Mwalimu.
Kinachomsubiri Simba
Akielezea kuhusu nafasi yake ndani ya Simba, Mwalimu alisema amekuja ili kupambana kufikia malengo ya timu iliyojiwekea pamoja na malengo yake binafsi.
“Nimekuja Simba kwa majukumu maalumu, nimekuja kupambana msimu huu kuhakikisha Simba inafikia malengo yake na mimi mwenyewe kufikia malengo ambayo nimejiwekea, kwa hiyo nina kazi mbili ambazo natakiwa kuzifanya kwa weledi na ustadi.”
Kuhusu wanaosema amefeli
Mwalimu akukaa kimya kuhusu watu wanaomsema kuwa amefeli kucheza Wydad;
“Huo ni mtazamo wao lakini mimi najua ni kitu gani ambacho kimenifanya nimekuja Tanzania na malengo ambayo nimejiwekea mimi mwenyewe katika msimu huu wa 2025/2026. Nimekuja kwa mkopo wa mwaka mmoja lakini huwezi jua kama Wydad pengine wakanihitaji tena kwenye dilisha dogo hata kabla ya mwaka kumalizika.
“Kwa hiyo mimi najua kitu ambacho kimenileta Tanzania na najua kazi iliyonileta. Binafsi sina presha yoyote kutokana na maneno ya watu kwenye mitandao, huwa nachukulia kama changamoto ambayo inanipa motisha kwenda kuwaonyesha ubora wangu uwanjani.
“Mimi nitawaonyesha na watajua kweli kijana amekuja kwa malengo gani, kwa hiyo nitapambana kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha naisaidia timu kwa asilimia mia moja kwani kwa sasa Simba ndiyo timu yangu na nina furaha pia kuwa Tanzania."
Kwa sasa Mwalimu ameshajumuika na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kilichotokea Misri kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2025/2026.
Nyota huyo wa Tanzania atakuwa na mtihani mwingine wa kupambania nafasi ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na kocha Fadlu Davids kwani anaungana na washambuliaji wengine kama Jonathan Sowah na Steven Mukwala ambao walionyesha makali msimu uliopita ambapo kila mmoja alifunga jumla ya mabao 13 kwenye Ligi Kuu.