Prime
Mtibwa ilishuka kinyonge ikapanda kibabe

Muktasari:
- Kushuka kwa Mtibwa Sugar kulihitimisha miaka 28 ya ushiriki wake kwenye Ligi Kuu ambayo ilicheza tangu ilipopanda mwaka 1996.
Mei 25, 2024 haikuwa siku nzuri katika historia ya Mtibwa Sugar kwani timu hiyo ambayo iliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mbili, ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu hadi Ligi ya Championship.
Siku hiyo, Mtibwa Sugar ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-2 na Mashujaa FC katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, matokeo ambayo yaliifanya Mtibwa kusalia na pointi zake 21 ambazo zisingeweza kuiokoa na janga la kushuka daraja wakati huo ikibakia na mechi moja mkononi.
Kushuka kwa Mtibwa Sugar kulihitimisha miaka 28 ya ushiriki wake kwenye Ligi Kuu ambayo ilicheza tangu ilipopanda mwaka 1996.

Hata hivyo Mtibwa Sugar imedumu katika Ligi ya Championship kwa msimu mmoja tu baada ya juzi, Jumamosi Aprili 26, 2025 kufanikiwa kurejea katika Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Bigman, matokeo yaliyoifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi 67 ambazo zitaifanya imalize katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Championship ambazo kikanuni timu zinazomaliza hapo zinapanda Ligi Kuu.
Siri ya mafanikio
Ubora wa kikosi cha Mtibwa Sugar umeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo hadi ikaweza kurejea Ligi Kuu baada ya kucheza Championship kwa msimu mmoja tu.
Kwa kiasi kikubwa hilo limechangiwa na idadi kubwa ya wachezaji wazoefu na wa hadhi ya Ligi Kuu ambao Mtibwa Sugar iliamua kubaki nao na wengine iliwasajili ikiamini uzoefu wao ungekuwa chachu kwao kufanya vyema katika ligi.
Safu yake ya ulinzi msimu huu imeundwa na kipa Costantine Malimi ambaye msimu uliopita aliitumikia Geita Gold kwenye Ligi Kuu na mabeki wawili wa kati mara kwa mara wamekuwa wakicheza nahodha Oscar Masai aliyewahi kuzichezea Geita na Azam FC sambamba na Eric Kyaruzi aliyewahi kuzichezea Kagera Sugar na Mbeya City.

Katika safu ya kiungo wanaocheza mara kwa mara ni Abdul Hillary aliyewahi kuichezea KMC, Juma Nyangi aliyewahi kucheza Alliance, Anuary Jabir aliyezitumikia Kagera Sugar na Dodoma Jiji huku kwenye ushambuliaji wakiwepo Omary Marungu, Raidhin Hafidh aliyeichezeaga Coastal Union, George Makang'a (Namungo, KMC) na Juma Liuzio (Simba, Mbeya City).
Namba hazipingwi
Mtibwa Sugar haijapanda kwa bahati mbaya au kwa kubahatisha na hilo linathibitishwa na takwimu ambazo imeweka katika mechi 28 ilizocheza msimu huu hadi ilipojihakikishia kupanda katika Ligi Kuu msimu ujao.

Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma 'Maniche'.
Ukiondoa idadi ya pointi 67 ilizokusanya, Mtibwa Sugar ndio timu ambayo imepata ushindi katika idadi kubwa ya michezo kwenye Championship msimu huu ambapo imefanya hivyo katika michezo 21 na inayofuatia kwa kupata ushindi mara nyingi ni Stand United ambayo imepata ushindi katika michezo 18.
Mtibwa Sugar imetoka sare nne na imepoteza michezo mitatu.
Kwa kufumania nyavu, Mtibwa Sugar inashika nafasi ya pili katika Ligi ya Championship ambapo hado sasa imefunga idadi ya mabao 54 huku timu kinara ikiwa ni Mbeya City ambayo imeziona nyavu za timu pinzani mara 58.
ndio timu ambayo imeruhusu mabao machache zaidi katika Ligi ya Championship ambapo katika mechi 28, nyavu zake zimetikiswa mara 16 huku inayoshika nafasi ya pili ikiwepo Bigman ambayo katika mechi 28, imefungwa mabao 18.

Mshambuliaji wake Raidhin Hafidh anashika nafasi ya tatu katika orodha ya vinara wa kufunga mabao katika Ligi ya Championship akiwa amefumania nyavu mara 16 huku anayeongoza akiwa ni Andrew Simchimba wa Geita Gold mwenye mabao 18 na anayeshika nafasi ya pili ni Abdul Shahame wa TMA ambaye ana mabao 17.
Ushindi mkubwa zaidi ambao Mtibwa Sugar imepata katika Ligi ya Championship msimu huu ni wa mabao 5-0 ambao iliupata katika mechi ya nyumbani dhidi ya Geita Gold katika Uwanja wa Manungu Complex, Februari 26, mwaka huu.
Ni mechi nne tu msimu huu ambazo Mtibwa Sugar ilimaliza bila kufunga bao ambazo tatu ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Stand United, Geita Gold na Songea United na nyingine ni ile iliyotoka sare tasa na Mbeya City.
Mtibwa Sugar haijaruhusu nyavu zake kutikiswa katika michezo 14 ambayo ni nusu ya mechi zote ilizocheza hadi sasa kwenye ligi hiyo.
Vita iko hapa
Kwa Mtibwa Sugar kuwa ya kwanza kupanda Ligi Kuu, timu hiyo imeacha ushindani mkali wa nafasi moja iliyobaki ya kupanda moja kwa moja kwa timu mbili ambazo ni Mbeya Ciy iliyopo nafasi ya pili na Stand United iliyopo nafasi ya tatu.

Mbeya City yenye pointi 62 inahitaji pointi nne tu katika mechi mbili ilizobakiza ili iweze kujihakikishia kupanda lakini kama itayumba, inaweza kujikuta ikitoa fursa kwa Stand United inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 59.
Mechi mbili ambazo Mbeya City imebakiza kwa ajili ya kumalizia msimu zote zitakuwa za nyumbani dhidi ya Cosmopolitan na Green Warriors.
Stand United imebakiza mechi moja ugenini dhidi ya Polisi Tanzania na ya mwisho itamalizia katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Geita Gold.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar, mechi ijayo itacheza ugenini dhidi ya Transit Camp na mechi ya mwisho itakuwa nyumbani kucheza na Kiluvya United.
Kuna ushindani wa kuwania nafasi moja ya kupanda Ligi Kuu kupitia mechi za mchujo (play-off) ambao unahusisha timu za Geita Gold, Mbeya Kwanza na TMA.
Kocha, wachezaji furaha
Kocha wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma 'Maniche' amesema kuwa kupanda kwao Ligi Kuu ni juhudi za pamoja za timu na sapoti ya mashabiki.
"Namshukuru mwenyezi Mungu tumeweza kurejea Ligi Kuu. Kwa dhati naushukuru uongozi wa Mtibwa Sugar, wachezaji na mashabiki kwa namna ambavyo tumekuwa tukishirikiana kuanzia mwanzo wa msimu hadi hivi sasa," alisema Maniche.
Mshambuliaji wa timu hiyo, Omary Marungu amesema kuwa heshima ya Mtibwa Sugar katika soka la Tanzania ndio iliwapa ari ya kufanya vizuri.
"Mtibwa Sugar ni timu kubwa Tanzania ambayo imeshawahi kuchukua ubingwa hivyo kucheza Championship hakuendani nayo na ndio maana tumekuwa tukipambana kuhakikisha inarudi Ligi Kuu na jambo jema tumefanikiwa katika hilo," amesema Marungu.