Mourinho arudishwa tena kwa Real Madrid
Muktasari:
- Timu 16 zinazocheza hatua ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Real Madrid, Monaco, PSG, Juventus, Benfica, Borussia Dortmund, Atalanta, Qarabag, Newcastle United, Club Brugge, Atletico Madrid, Bodo/Glimt, Inter Milan, Olympiacos na Bayer Leverkusen.
Droo ya hatua ya mchujo ya kuwania kucheza hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imechezeshwa leo huko Nyon, Switzerland huku ikiibua baadhi ya mechi zenye mvuto na ushindani.
Miongoni mwa mechi zinazotegemewa zitakuwa na ushindani na mvuto mkubwa ni mbili zitakazokutanisha timu mbili za Ufaransa, Monaco na PSG ambazo zimepangwa kukutana katika mchujo.
Droo hiyo pia itamkutanisha kwa mara nyingine Meneja wa Benfica, Jose Mourinho na timu yake ya zamani, Real Madrid.
Ikumbukwe Jumatano iliyopita, Mourinho aliiongoza Benfica kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Real Madrid katika mechi ya mwisho ya hatua ya ligi ya mashindano hayo.
Qarabag imepangwa kukutana na Newcastle United, Bodo/Glimt itaumana na Inter Milan na Galatasaray itacheza dhidi ya Juventus.
Borussia Dortmund itacheza na Atalanta, Club Brugge itakabiliana na Atletico Madrid na Olympiacos itacheza na Bayer Leverkusen.
Kwa mujibu wa utaratibu wa mashindano hayo, timu zilizomaliza katika nafasi ya tisa hadi ya 16 zitaanzia mechi zao za hatua ya mchujo ugenini na kumalizia nyumbani.
Mechi za kwanza za hatua ya mchujo zitachezwa Februari 17 na 18 mwaka huu na za marudiano zitakuwa Februari 24 na 25 mwaka huu pia.