Bao la kipa lilivyoivusha Benfica Ligi ya Mabingwa Ulaya
Kipa wa Benfica, Anatoliy Trubin (Kulia mwenye nguo za njano), akitoka kuupiga mpira kwa kichwa na kufunga bao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Jumatano, Januari 28, 2026. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kipa, Anatoliy Trubin amefunga bao hilo katika dakika za majeruhi na kuisaidia Benfica kucheza hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lisbon, Ureno. Kipa wa Benfica, Anatoliy Trubin, ameingia kwenye historia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufunga bao lililoipa timu yake ushindi wa kusisimua wa mabao 4-2 dhidi ya Real Madrid, na kuinyakulia Benfica tiketi ya mwisho ya kufuzu hatua ya mtoano chini ya kocha Jose Mourinho.
Dakika tano za nyongeza zilikuwa tayari zimekwisha, lakini mashabiki walioufurika Uwanja wa Estadio da Luz hawakuwa na haraka ya kuondoka. Ndipo tukio la hilo likatokea.
Trubin, kipa mwenye kimo cha futi sita na inchi sita kutoka Ukraine aliruka juu katika lango la Madrid na kuupiga mpira kwa kichwa na kuzitikisa nyavu za kipa mwenzake, Thibaut Courtois.
Kocha Jose Mourinho, aliyekuwa akihitaji bao moja tu dhidi ya klabu aliyowahi kuinoa, alimkumbatia mvulana wa kuokota mipira kwa shangwe kubwa, ishara ya hisia kali zilizotawala uwanja huo katika dakika za mwisho.
Ushindi huo wa mabao 4-2 uliopatikana dakika ya 97 uliihakikishia Benfica nafasi ya mwisho ya kufuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Real Madrid wakijikuta wakiingia hatua hiyo kwa tabu baada ya kupoteza mchezo huo.
Kocha wa Benfica, Jose Mourinho akishangilia bao la Kipa wake, Anatoliy Trubin alilofunga usiku wa jana dhidi ya Real Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Januari 28, 2026. Picha na Mtandao
Akizungumza baada ya mechi, Mourinho amekiri ugumu wa hali iliyojitokeza:
“Nimeshawahi kushinda au kupoteza katika mpira wa mwisho, lakini hali kama hii ni ngumu kuelezea. Unashinda lakini haitoshi, unafikiri inatosha lakini bado haitoshi, kisha unalazimika kubadili mbinu na kuchukua maamuzi ya hatari.
“Kuwashinda Real Madrid daima kuna uzito wake, lakini katika wakati kama huu tulilazimika kwenda kushambulia kwa kila kitu. Sisi si timu imara kwenye mipira ya juu, lakini golikipa alienda mbele na kufunga bao la kipekee. Ushindi huu ni wa kihistoria,” amesema Mourinho.
Baadhi ya wachezaji wa Benfica wakimshangilia Kipa wao, Anatoliy Trubin mara baada ya kufunga bao muhimu dhidi ya Real Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Januari 28, 2026.. Picha na Mtandao
Mchezo huo ulikuwa tayari umejaa matukio kadhaa hata kabla ya bao la Trubin, huku Madrid wakimaliza wakiwa na wachezaji tisa pekee baada ya Raul Asencio na Rodrygo kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi.
Real Madrid walikuwa wameanza vyema mechi hiyo, wakitangulia kupata bao kupitia Kylian Mbappe katika dakika ya 30, bao lililowapa matumaini ya kumaliza ndani ya timu nane bora za juu katika mashindano hayo.
Baadhi ya wachezaji wa Benfica wakiwa wameungana na Kipa wao, Anatoliy Trubin, mara baada ya kufunga bao muhimu dhidi ya Real Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Januari 28, 2026.. Picha na Mtandao
Hata hivyo, Benfica walisawazisha kupitia mabao mawili ya Andreas Schjelderup pamoja na bao la penalti la Vangelis Pavlidis, kabla Mbappe hajapunguza tena tofauti ya mabao kisha baadae golikipa, Trubin akafunga bao lililowapeleka hatua ya mtoano.