16 Bora UEFA kila kitu hapa
London, England. Timu za England vinavyoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya zimefahamu wapinzani wao wanaowezekana katika hatua ya 16 bora baada ya vilabu vitano kati yao kumaliza ndani ya nane bora na kufuzu moja kwa moja.
Arsenal, Liverpool, Tottenham, Chelsea na Manchester City zote zimefuzu kwenda hatua ya 16 bora, huku Newcastle ikiwa ndiyo pekee inayolazimika kupita kwenye michezo ya mchujo (play-offs).
Katika mwisho wa kusisimua wa hatua ya ligi, Real Madrid na Paris Saint-Germain zililazimika kwenda kwenye mchujo, Napoli ilitolewa kabisa na kipa wa Benfica Anatoliy Trubin alifunga bao la kichwa dakika ya 98 ili kuiweka timu ya Jose Mourinho kwenye mashindano.
Mshambuliaji wa Newcastle, Anthony Elanga (Kushoto) Nick Woltemade (Kulia) wakijaribu kumpita beki wa PSG, Ashraf Hakimi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyomalizika kwa sare ya 1-1 jana Jumatano, Januari 28, 2026. Picha na Mtandao
Newcastle ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya PSG na sasa italazimika kucheza dhidi ya Monaco au Qarabag katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini mwezi Februari ili kujaribu kujiunga na wenzao wa Ligi Kuu ya England.
Iwapo watafuzu hatua ya 16 bora, watakutana na Barcelona au Chelsea. Arsenal itakutana na Atalanta, Bayer Leverkusen, Borussia Dortmund au Olympiacos katika hatua ya 16 bora baada ya kumaliza kileleni mwa hatua ya ligi.
Kikosi cha Mikel Arteta kiliibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Kairat ya Kazakhstan katika uwanja wa Emirates na kuwa klabu ya kwanza kushinda michezo yote minane ya hatua ya ligi tangu mfumo mpya ulipoanza msimu uliopita.
Liverpool na Tottenham zitacheza dhidi ya Juventus, Atletico Madrid, Club Brugge au Galatasaray baada ya kumaliza nafasi ya tatu na ya nne mtawalia.
Timu ya Arne Slot iliichapa Qarabag 6-0, huko Anfield kuendeleza kiwango kizuri kwenye Ligi ya Mabingwa, huku Tottenham ikipata ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Frankfurt.
Chelsea itakutana na PSG, Newcastle, Monaco au Qarabag katika hatua ya 16 bora baada ya kuibuka na ushindi wa kusisimua wa 3-2 dhidi ya Newcastle, shukrani kwa mabao mawili ya Joao Pedro kipindi cha pili.
Manchester City, ambayo ilifuzu kwa tabu kwa kumaliza nafasi ya nane, itakutana na Real Madrid, Inter Milan, Bodo/Glimt au Benfica baada ya kuifunga Galatasaray 2-0.
Kwa kuangalia mbele zaidi kwenye michuano, Arsenal na Manchester City ziko upande mmoja wa droo, hivyo zinaweza kukutana katika robo fainali.
Liverpool na Tottenham haziwezi kukutana katika hatua hiyo, lakini zinaweza kucheza dhidi ya Chelsea au Newcastle.
Mshambuliaji wa Arsenal, Viktor Gyökeres akishangilia bao lake katika ushindi wa 3-2 dhidi ya FC Kairat katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa jana Jumatano, Januari 28, 2026. Picha na Mtandao.
Arsenal, Liverpool na Tottenham zote zitacheza mechi ya marudiano ya hatua ya 16 bora na robo fainali nyumbani kutokana na kumaliza ndani ya nne bora.
Arsenal pia itacheza mechi ya marudiano ya nusu fainali nyumbani iwapo itafika huko, kutokana na kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu.
Timu nyingine zilizomaliza ndani ya nane bora ni Bayern Munich (ya pili), Barcelona (ya tano) na Sporting Lisbon (ya saba), ambayo ilifunga bao la ushindi dakika ya 94 dhidi ya Athletic Bilbao na kujihakikishia kufuzu moja kwa moja, huku ikiitupa Real Madrid kwenye mchujo.
Kuepuka michezo ya mchujo mwezi Februari ni faida kubwa kwa timu kwani huwapa muda wa kupumzika na kujiandaa. Kocha wa Chelsea, Liam Rosenior, alisema:
“Ni jambo kubwa sana. Linatupa nafasi ya kufanya kazi vizuri na wachezaji uwanjani. Nimefurahi sana tumefuzu kwa njia hii.” Kocha Eddie Howe wa Newcastle alisema:
“Bila shaka tulitaka kufuzu moja kwa moja, lakini hatutaona michezo hiyo kama hasi.
“Tuna ratiba ngumu na tumekuwa na mechi nyingi msimu huu, lakini tuna kundi la wachezaji wenye kujituma na huu ni mtihani mwingine wa kukabiliana nao.”
Kwa upande wa Newcastle, sasa italazimika kucheza mechi nane mwezi Februari, ikiwemo michezo minne ya Ligi Kuu, mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Manchester City, na mchezo wa raundi ya nne ya FA Cup ugenini dhidi ya Aston Villa.
Katika michezo mikubwa ya mchujo, Mourinho anaweza kukutana tena na Real Madrid akiwa na Benfica, baada ya kuifunga 4-2 huko Lisbon.
PSG nayo huenda ikakutana na mpinzani wa Ufaransa, Monaco. Droo ya michezo ya mchujo itafanyika Ijumaa.
Baadhi ya wachezaji wa Liverpool wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 6-0 walioupata dhidi ya Qarabag katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana Jumatano, Januari 28, 2026. Picha na Mtandao
Msimamo kamili wa hatua ya ligi
Arsenal – pointi 24
Bayern Munich – 21
Liverpool – 18
Tottenham – 17
Barcelona – 16
Chelsea – 16
Sporting Lisbon – 16
Manchester City – 16
Real Madrid – 15
Inter – 15
PSG – 14
Newcastle – 14
Juventus – 13
Atletico Madrid – 13
Atalanta – 13
Bayer Leverkusen – 12
Borussia Dortmund – 11
Olympiacos – 11
Club Brugge – 10
Galatasaray – 10
Monaco – 10
Qarabag – 10
Bodo/Glimt – 9
Benfica – 9.25
Marseille – 9
Pafos – 9
Union Saint-Gilloise – 9
PSV – 8
Athletic Bilbao – 8
Napoli – 8
Copenhagen – 8
Ajax – 6
Eintracht Frankfurt – 4
Slavia Prague – 3
Villarreal – 1
Kairat – 1