Morocco yabanwa, Twiga mzigoni

Muktasari:
- Zambia ni moja kati ya timu kubwa kwenye michuano hii ikiwa imemaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2022 hii ikiwa ni mara yao ya nne wanashiriki michuano hii.
Rabat, Morocco. Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wanawake (WAFCON) imeanza jana kwa wenyeji Morocco kubanwa nyumbani na Zambia, huku Twiga Stars ikiingia uwanjani kesho.
Hii ni michuano mikubwa kwa upande wa wanawake Afrika ikishirikisha timu kubwa za bara la Afrika.
Twiga itaanza kampeni zake kesho wakati itakapovaana na Mali kwenye mchezo unasubiriwa kwa hamu kubwa ukianza majira ya saa 4:00 usiku.
Mali ni moja ya timu tishio kwenye michuano hii ikiwa imeshatwaa ubingwa huo mara moja, lakini itakutana na kigingi cha Twiga ambayo kwa sasa ina mastaa wenye uzoefu wa kutosha.
Mechi nyingine kali ya kesho, Afrika Kusini itavaana na Ghana kwenye mchezo wa mapema.
Katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi jana, Morocco ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Zambia kwenye mechi iliyokuwa na mvuto wa hali ya juu ikipigwa kwenye Uwanja wa Rabat Olympic.
Staa wa Zambia Barbara Banda, alikuwa wa kwanza kuifungia timu yake katika dakika ya kwanza tu ya mchezo huo.
Morocco iliamka na kusawazisha katika dakika ya 12 tu ya mchezo kwa mkwaju wa penalti, lakini Zambia ilijipatia bao la pili kupitia kwa Kundananji katika dakika ya 27.
Ghizlan Chebbak alifanikiwa kuifungia Morocco katika dakika za mwisho kabisa za mchezo huo na kufanya mchezo huo umalizike kwa sare ya mabao 2-2, lakini mashabiki wa Morocco walilalamikia safu yao ya ulinzi kuwa mbovu.
Morocco, ambao ndiyo nchi mwenyeji inatakiwa kufanya kazi kubwa ili kupata mafanikio makubwa zaidi ya yale ya mwaka 2022 ambao ilimaliza katika nafasi ya pili ambapo ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Afrika Kusini.
Zambia ni moja kati ya timu kubwa kwenye michuano hii ikiwa imemaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2022 hii ikiwa ni mara yao ya nne wanashiriki michuano hii.