Kutojua sheria kigingi wanasoka wa kike

Muktasari:
- Sheria ya FIFA kuhusu uzazi ya mwaka 2020 iliyoanza kutekelezwa Januari 2021 inalenga kuimarisha usawa, heshima na ulinzi wa wanasoka wa kike.
Licha ya kutotekelezwa sheria ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuhusu haki za wachezaji wa kike wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kanuni hizo hazifahamiki kwa wachezaji wengi, makocha na hata uongozi wa vilabu.
Kati ya wachezaji wa timu zote za Ligi Kuu ya Wanawake waliozungumza na kufanyiwa utafiti kupitia dodoso zilizoandaliwa na Mwananchi, ni mmoja pekee ndio mwenye ufahamu kidogo kuhusu sheria hiyo, huku makocha na viongozi wa vilabu saba waliohojiwa, mmoja pekee ndiye aliyesema anaifahamu sheria hiyo, mmoja ana ufahamu kidogo na watano hawafahamu kabisa.
Sheria inasemaje
Sheria ya FIFA kuhusu uzazi ya mwaka 2020 iliyoanza kutekelezwa Januari 2021 inalenga kuimarisha usawa, heshima na ulinzi wa wanasoka wa kike.
Kupitia sheria hii, wachezaji wa kike wanapopata ujauzito wanapewa haki zikiwamo likizo ya uzazi yenye malipo, akitakiwa kulipwa theluthi mbili (2/3) ya mshahara wa kila mwezi, haki ya kurejea kazini baada ya kujifungua, huku klabu ikitakiwa kumsaidia kurejea taratibu kupitia mazoezi mepesi na baada ya kurejea atatakiwa kupewa muda maalumu kwa ajili ya kunyonyesha.
Sheria inazitaka timu kulinda mikataba ya wachezaji, haziruhusiwi kuvunja mkataba wa mchezaji kwa sababu ya ujauzito na iwapo hilo litafanyika, mchezaji atapaswa kufidiwa.
Timu zina nafasi ya usajili wa dharura, nje ya dirisha rasmi la usajili ili kufidia nafasi ya mchezaji aliye kwenye likizo ya uzazi na mchezaji anatakiwa kupumzika walau wiki 14, baada ya kujifungua kabla ya kurejea kiwanjani.
Shuhuda za wachezaji
Kwa upande wa wachezaji, Irene Kisisa anayeichezea Yanga Princess ndiye pekee kati ya waliohojiwa aliyesema anaifahamu sheria.
Anasema aliifahamu baada ya mchezaji wa Ulaya kushinda kesi dhidi ya timu yake. Hata hivyo anasema hakuifuatilia zaidi ili kuijua kwa undani.
Kipa wa zamani wa Yanga Princess, ambaye kwa sasa anaichezea Ceassia Queens ya Iringa, Tausi Abdallah anasema alijifungua kabla ya sheria hiyo kuwapo, lakini anaamini itawalinda wachezaji.

"Nilijifungua muda mrefu sheria hii haikuwapo, lakini hadi sasa wewe ndiye mtu wa kwanza kuniambia kwamba kuna sheria kama hii, sijawahi kuisikia popote," anasema Tausi ambaye alipojifungua alikuwa akichezea timu ya Mburahati.
"Nilifikiria muda unaenda na siwezi kucheza mpira muda wote, hivyo niliachana na soka na kuamua kuzaa, kipindi hicho hatukuwa hata na mishahara ilikuwa posho tu," anasema na kuongeza:
"Kwa miaka mitatu nilikuwa nje nikilea kabla ya kurudi kiwanjani. Hii ni kawaida kwa wachezaji wengi, wakitaka kuzaa hujitenga kabisa na timu, utasikia tu fulani kazaa, lakini kama wangekuwa wanafahamu sheria hii nafikiri wasingefanya hivyo.”
Mchezaji wa zamani wa Baobab Queens, Martha John anasema:
"Sijawahi kuisikia na wangewezaje kutimiza sheria hiyo kama pesa yangu ya usajili tu hawakunilipa. Nilijpanga kwa sababu niliamua kupata mtoto, hivyo haikunisumbua kwenye masuala ya kiuchumi."
Anasema baada ya kubaini ni mjamzito msimu ukielekea kumalizika, aliamua kutosaini mkataba mpya na timu yoyote ili alee mimba.
Hali hiyo anasema ilichangiwa na kutokuwa na uelewa kuhusu sheria hiyo.
Herieth Edward, mchezaji wa timu ya Ceassia Queens, sawa na wenzake haijui sheria ila anasema: "Kuna umuhimu wa kujua sheria hii, kuna wachezaji hawana wazazi, pengine wanafikiria ikiwa watazaa mtoto watamwacha na nani? nimepata bahati mwanangu analelewa na mama yangu.”
Anasema alibaini ana ujauzito ukiwa na takribani miezi mitano wakati huo akiwa na timu ya Taifa, hivyo alirudi nyumbani kulea mimba hadi alipojifungua.
"Kipindi hicho nilikuwa Marsh Queens, niliamua kuondoka ingawa niliwaambia uongozi kwamba naumwa," anasema.
Mbali ya wachezaji hao waliozungumza, pia Mwanachi ilifanya dodoso ya mtandao kwa wachezaji wawili kwa kila timu y Ligi Kuu ya Wanawake na kati ya hayo hakuna hata mmoja aliyekuwa anaifahamu sheria hii.
Ufahamu wa viongozi
Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya anasema anaifahamu sheria na amekuwa akiwakumbusha wachezaji kuhusu umuhimu wa kuanzisha familia.
"Naifahamu na hata mimi binafsi nimekuwa nikiwakumbusha wachezaji juu ya umuhimu wa familia na kuzaa," anasema.
Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema anasema anaifahamu sheria hiyo ingawa si kwa undani.
Anasema: "Wachezaji wanaopata mimba wakiwa na timu huwa wanaondoka wenyewe kwa sababu mchezaji anasajiliwa kwa ajili ya kucheza.”
Anatoa mfano akisema: “Mchezaji amesajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja, amepata mimba mwezi wa saba au wanane, au tuseme alikuja akiwa na mimba na mkataba amesaini mwezi wa saba unaisha wa tano mwaka unaofuatia, atahudumiwajwe wakati hakuna anachokitoa katika timu?"
Edna anasema sheria hiyo ni ngumu kutekelezwa Tanzania kutokana na mazingira, hivyo anaona labda mchezaji apewe muda wa kulea mimba na mtoto kisha akirejea ndipo aanze kulipwa.
Kocha wa Fountain Gate Princess, Mirambo Kamili anasema hana ufahamu kuhusu sheria hiyo lakini haoni ugumu wa kuitekeleza.
"Mimi siifahamu hii sheria lakini sioni kama kuna ugumu sana wa kuitekeleza, kwa sababu kama timu ilimsajili mchezaji ikiwa na nia ya kumlipa mshahara, inashindwaje kumpa mshahara nusu? ni kwa sababu tu, baadhi ya timu huwa zinataka kunufaika na mchezaji wakati huo hawataki wachezaji wanufaike na timu," anasema.
Kocha wa Mashujaa Queens, Ally Ally anasema hajawahi kusikia kuhusu sheria hiyo.
"Mara nyingi huwa wanamsajili kama mchezaji wa kiume ndiyo maana hata siku moja katika mikataba wanayowapa wachezaji sijaona kipengele kuhusu familia," anasema.
Kocha Ezakiel Chobanka, aliyefundisha timu za wanawake kwa zaidi ya miaka saba akiwa na timu za Alliance ya Mwanza, Tiger Queens na Ceassia Queens ya Iringa anasema haifahamu sheria ingawa anaamini ikifuatwa itasaidia wachezaji.
"Nina muda mrefu kwenye soka la wanawake, siifahamu sheria hii. Pia sijawahi kuwa na mchezaji mwenye ujauzito kwenye timu kuanzia Alliance na hapa nilipo sasa (Ceassia)" anasema.
Mlezi wa zamani wa Baobab, Inocencia James anasema hajawahi kuisikia sheria hiyo licha ya kuwa kiongozi wa timu ya wanawake kwa zaidi ya miaka sita.
Sawa na wenzake, Meneja wa Bunda Queens, Aley Ibrahim anasema haifahamu sheria hiyo ingawa ina umuhimu kwa ustawi wa wachezaji na soka la wanawake nchini.
Kauli ya Wizara, TFF
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa linatekeleza suala la usalama kwa wachezaji kwa timu za wanawake kwa kushirikiana na FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Amesema TFF wapo katika mchakato wa kuandaa mapitio ya sera mpya ya Safe Guarding kwenye mpira wa miguu kwa Tanzania ambayo itahusisha maeneo mbalimbali ya haki za wanawake wanaocheza mpira.
"Serikali kwa kushirikiana na TFF tupo katika mchakato wa kuhakikisha sera ya usalama kwa wachezaji inaanza kutumika kwa timu zote za wanawake ili kuweka mazingira mazuri kwa wachezaji wa kike ambao ni wajawazito au wanaonyonyesha waweze kuendelea kushiriki katika shughuli za michezo kwa usalama," amesema.
Mkurugenzi wa sheria, masoko na hadhi za wachezaji, Boniface Wambura amesema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa viongozi wa timu mbalimbali kuhusu sera hiyo.
"Bado tunatoa mafunzo, lakini hili ni suala la sheria ni haki ya mtu, hivyo yule ambaye anaona amenyimwa haki kuna vyombo vinasimamia aende. Shida kubwa iliyopo hatupendi kusoma na kujifunza, muda mwingine hata tukiwa tunatoa elimu ya bure watu wanaona tabu kushiriki," anasema
Mwansheria Simon Patrick anasema: "Changamoto kubwa ipo Afrika, timu nyingi za wanawake zimekuwa zikiwapa wachezaji mikataba ya mwaka mmoja mmoja kwa sababu zinahofia zikiwapa mikataba ya muda mrefu wanaweza kupata mimba wakiwa ndani ya mkataba."
Anasema kuwapa mikataba ya mwaka mmoja ni njia mojawapo ya kuepuka kuwatimizia wachezaji mahitaji yanayotakiwa kwa mujibu wa sheria.
"Lakini sasa naona timu nyingi zimeelewa kwa sababu kuna mikataba ya miaka miwili na kuendelea," anasema.
Athari kiafya
Daktari bingwa wa masuala ya uzazi kwa kina mama, Abdul Mkeyenge anasema kwa kawaida mchezaji wa kike anatakiwa kupumzika anapopata ujauzito kwa sababu mazoezi wanayofanya yatamweka katika hatari kubwa ya kuharibu mimba.
"Anasema mjamzito anashauriwa vitu vya kufanya na vingine hashauriwi. Katika mazoezi, hashauriwi kufanya magumu kwa sababu yana asilimia kubwa ya kusababisha mimba kuharibika,” anasema.
Anasema: "Kwenye mpira wa miguu tunatumia nguvu, tunakimbia huku na kule na kuna mazoezi mengine ya kunyoosha viungo, mtu anaweza akainama kushoto au kulia, sasa ile si nzuri sana kwa mjamzito, hivyo kimsingi mwanamke akiwa na mimba hatakiwi kufanya mzoezi magumu au kunyanyua vitu vizito na kujikunja kupita kiasi."
Anasema kitaalamu na kiusalama akipata ujauzito ni vyema akakaa nyumbani.
"Mwanamke akipata mimba kibaiolojia mwili huwa na mabadiliko, wengine huwa hawapendi kufanya kitu fulani au wanakuwa na hasira, sasa unakuta mchezaji mwenye hali hiyo akipewa hata maelekezo na mwalimu wake, anaweza asifanye kile anachoambiwa," anasema.
Ujauzito anasema unaweza kuchangia kiwango cha mchezaji kushuka kwa kuwa naweza asifuate maelekezo.
Imeandikwa kwa udhamini wa Taasisi ya Gates Foundation.