Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa heri Mzee Samatta, utakumbukwa

Muktasari:

  • Nilimpigia simu kiungo wa zamani wa KMC, Prisons, Mbeya City, JKT Mgambo, African Lyon, Mohamed Samatta ambaye ni kijana wake, aliyekiri ni kweli mzee hatunaye tena.

Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kusema maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwengu, kwa sasa msemo huo unatumika kumsimulia maisha ya staa wa zamani wa Simba na Stars, Ally Pazi Samatta (marehemu).

Mzee Samatta alikutwa na umauti jana Jumapili asubuhi na nilipopokea ujumbe mfupi  katika simu yangu uliyoandikwa; 'Mzee wako Samatta hatunaye tena duniani'. Ilinichukua dakika kama tatu kuujibu kisha kuchukua hatua ya kupiga simu nikidhani pengine huenda kapoteza simu yake.

Nilimpigia simu kiungo wa zamani wa KMC, Prisons, Mbeya City, JKT Mgambo, African Lyon, Mohamed Samatta ambaye ni kijana wake, aliyekiri ni kweli mzee hatunaye tena.

Limekuwa jambo gumu kusimulia angalau kwa uchache  namna nilivyomfahamu Mzee Samatta aliyenichukulia kama binti yake na sio mwandishi wa michezo, alikuwa mtu mwenye busara, hekima, upendo mkubwa na hofu ya Mungu aliamini utu kuliko vitu alivyokuwa anasisitiza vinapita.

Siku tatu kabla ya kifo chake nilipokea simu kutoka kwa Mzee Samatta, akiniambia binti yangu naumwa utakapopata muda uje kuniona, ingawa sauti yake haikuonyesha kama mtu aliyezidiwa, nikamjibu pole baba 'Mzee Pele', nitajitahidi kuja kukujulia hali, kisha akampatia simu mkewe ambaye niliongea naye na kumpa pole ya kuuguza naye akasisitiza uje umuone mzee wako.

Kati ya vitu muhimu alivyoniambia siku hiyo vitakavyosalia kumbukumbu katika maisha yangu alisema unapopata changamoto  katika maisha yako silaha ya kwanza iwe ukimya, bidii, kumtegemea Mungu na vitendo vyako viwe na nguvu kuliko maneno na kifo pekee ndicho kije kikatize ndoto zako ni kitu alichokisisitiza sana bila kujua siku za usoni nitapokea taarifa za kifo chake.

Kisha akanigusia kuhusiana na binti yake anayeitwa Sophia ambaye alikuwa anatamani kusomea taaluma ya habari na sasa amechukua masomo ya utalii, akanisisitiza ikitokeaa akaja akasomea mambo ya habari uje kuwa msaada wa kumuelekeza maadili na kujituma kwa bidii.


Ninavyomfahamu

Ni miaka mingi iliyopita ambapo kwa mara ya kwanza nilifunga safari ya kwenda kufanya mahojiano na Mzee Samatta  nyumbani kwake, Mbagala Rangi Tatu, nilimkuta akiwa na watoto Said mchezaji wa zamani wa Polisi Tanzania, Mohamed na wajukuu zake.

Baada ya kujitambulisha akamwambia kijana wake Said akanichukulie soda, nilipogundua ni mzee mcheshi baada ya Said kuleta soda zilikuwa katika mfuko kama nne hivi, akaniuliza unakunywa soda gani nikajibu (jina kapuni)  kwa bahati mbaya haikuwepo, akamwambia kijana wake haya rudi tena dukani ukachukue, nikajikuta naingiwa na hofu kuona nasumbua watu.

Baada ya Said kurejea nayo akamwambia baba yake nimerudi afande kisha wakaanza kucheka, baadaye katika stori za hapa na pale nikagundua ni mzee msomi na alikuwa kamanda wa polisi na mchezaji mahiri enzi zake.

Tangu siku hiyo alinieleza alipenda nidhamu yangu akawa na ushirikiano mkubwa na magazeti ya Mwananchi pindi alipoulizwa kuhusiana na vipaji vya watoto wake na maoni mbalimbali.

Kati ya exclusive aliyowahi kuitoa katika magazeti ya Kampuni ya Mwananchi ilikuwa ni kuhusiana na ndoa ya kijana wake  Mbwana Samatta aliyofunga mwaka 2021 na mkewe Naima Mgange.

Siku mbili kabla ya harusi ya Mbwana, mzee huyo alinitumia ujumbe katika simu yangu ukisema ndani ya wiki hii nitakupa taarifa kubwa na kweli ilipofika siku ya tukio ilikuwa jioni akanitumia ujumbe mwingine akisema ndugu yako anaoa (Mbwana), lakini hataki vyombo vya habari ila njoo moja kwa moja hadi nyumbani Mbagala utapanda gari la familia.

Baada ya kufika katika tukio la harusi yenye nikiwa na Wanahabari wenzangu ambao ni Bui na Elizabeth tukazuiwa na watu ni kama walikuwa mabaunsa ambao hawakutaka kiandikwe chochote, ndipo yule mzee akasimama kifua mbele na kunitetea kwamba yeye ni mzazi ana haki ya kufanya kile anachokitaka kwa kijana wake, ndipo tukaendelea na kazi zetu.

Exclusive nyingine ilikuwa ni kuhusiana na msikiti ambao Mbwana ameujenga Vikindu Wilaya Mkuranga uliyo na uwezo wa kuingiza waumini 500, jumba lake la kifahari  lilipo  maeneo ya Kibada Wilayani Kigamboni, ofisi zake za utalii, kuwakataza vijana wake kupiga penalti pamoja na usajili wa Mbwana ukiwemo ule wa kwenda Aston Villa mwaka 2020.

Pia alikuwa anasisitiza kwa nini anapenda kumzungumzia Mbwana ni kutokana na ukimya wa kijana wake huyo, ambao baadhi ya watu walikuwa wanatumia kama fimbo ya kumkandamiza na mazuri yake aliyokuwa anayafanya yashindwe kuonekana, hivyo hakutaka kukubali unyonge aliamua kukaa mbele ili kuhakikisha kijana wake anapata heshima inayotakiwa.

Ukiachana na hilo, aliwahi kunishangaza katika mambo kadha, moja ni kukataa kwenda kuishi katika mjengo ambao kijana wake aliujenga alitamani zaidi kuona anapopita mtaani kwake Mbagala anataniwa na watoto njiani ambao alikuwa ana kawaida ya kuwapa pesa za kununua pipi, kachori na kuamini hiyo ni baraka kwake.

Pia aliwahi kusema alitamani angekuwa hai mama yake Mbwana ili ayaone mafanikio ya kijana wake, lakini kitu alichokifanya kama kumbukumbu ni kumbukusha kwenda kuwasaidia ndugu wa mama yake.

Kiufupi nimeshindwa kuelezea kila kitu kumhusu mzee Samatta ambaye alijaa ukarimu, ushauri imekuwa vigumu mno kutokana na kifo chake, kubwa nitamuombea kwa Mwenyezi Mungu apumzike kwa amani na kuyafanyia kazi mambo aliyowahi kunishauri katika kazi yangu.

Na leo Mzee wetu huyu sitapata fursa ya kuzungumza naye tena, kwani mchana wa leo mwili wake unaenda kuhifadhiwa katika maskani yake ya milele huko Kibiti, mkoani Pwani. Inaumiza sana.


Huyu ndiye Mzee Pazi

Mzee Ally Pazi Samatta alizaliwa mwaka 1943 mkoani Pwani na enzi za uahi wake aliwahi kuwa muajiriwa wa Jeshi la Polisi na aliktamba katika soka akicheza kama mshambuliaji namba 10.

Baadhi ya timu alizozitumikia enzi za ujana wake alipokuwa akikiwasha na kutupia sana kambani ni Polisi Moro aliyocheza mwaka 1962- 1963 kisha kukipiga Canada Dry (1963-1964) kabla ya kusajiliwa na Simba enzi ikifahamika kama Sundeland aliyoitumikia kuanzia mwaka 1964-1965. Amekipiga pia timu za West Lake (iliyokuja kubadilishwa majina kadhaa hadi kuwa Kagera Sugar), Polisi Dar es Salaam na timu ya Mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima United).

Pia amewahi kukipiga kwa mabingwa wa zamani wa Ligi ya Bara, Cosmopolitan kati ya 1968-1969 na kuzitumikia pia timu za taifa kuanzia ile ya Tanzania Bara hadi Taifa Stars na mbali na kucheza timu ya Mkoa wa Dar na kushiriki michuano ya Kombe la Taifa, kabla ya kugeukia ukocha akizinoa baadhi ya timu kama Polisi Mara na kuzinoa timu za mikoa ya Morogoro na Mbeya.

Kipaji chake cha soka alikirithisha kwa wanawe Mohammed Samatta anayemudu kucheza kama kiungo mshambuliaji akikipiga timu kadhaa ikiwamo African Lyon, KMC na nyinginezo wakati Mbwana Samatta akitamba kuanzia Mbagala Market, African Lyon, Simba, TP Mazembe ya DR Congo,  KRC Genk ya Ubelgiji, Aston Villa ya England, Fenerbahce ya Uturuki na PAOK ya Ugiriki.

Hata hivyo, katika mahojiano maalum na Mwananchi enzi za uhai wake, Mzee Samatta alisema licha ya Mohammed na Mbwana kufahamika zaidi, lakini ana watoto wake wengine wa kiume wanakipiga kama kawaida sambamba na binti yake aitwae Sophia mbali na wajukuu zake watano wanaocheza pia.