Medo afutwa kazi Kagera Sugar

Dar es Salaam. Klabu ya Kagera Sugar imefuta kazi kocha wake Mellis Medo baada ya matokeo mabaya ya timu hiyo msimu huu.
Kagera imechukua maamuzi hayo baada ya kocha huyo kuongoza timu hiyo kwenye mechi 14 za Ligi Kuu Bara tangu alipotangazwa kuwa kocha wa timu hiyo, Oktoba 17,2024.
Medo ambaye alitua Kagera akitokea kwa ndugu zao Mtubwa Sugar ndani ya mechi 14, amefanikiwa kushinda mechi mbili pekee akipoteza saba huku akitoa sare tano.
Awali timu hiyo ilikuwa chini ya Mganda Paul Nkata ambaye alitangulia kufukuzwa akiwa amewaongoza wakata miwa hao kwenye michezo saba ya kwanza, akishinda mmoja pekee.
Ingawa Kagera bado haijatangaza rasmi lakini Mwananchi linafahamu kwamba kocha huyo ameshaondolewa kwenye timu hiyo ambayo imerudi nyumbani kuanza maisha mapya bila ya Medo.
Mchezo wa mwisho ambao umehitimisha siku 129 za Medo ndani ya Kagera ni ule dhidi ya JKT Tanzania walipopokea kipigo cha mabao 2-0, ambapo baada ya mechi hiyo kocha huyo alibakizwa jijini Dar es Salaam kwa kumalizana na mabosi wake huku kikosi hicho kikirudi Bukoba.
Ndani ya mechi hizo 14 Kagera imeruhusu mabao 22, ikifunga 13 pekee ikiendelea kusalia nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi na pointi zao 15 ndani ya mechi 21 ilizocheza.