Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City hali tete ikichapwa nyumbani na Fountain Gate

Muktasari:

  • Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea keshokutwa kwa uwepo wa mechi mbili zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti nchini.

Dar es Salaam. Kichapo cha bao 1-0 nyumbani kutoka kwa Fountain Gate, leo Jumanne, Machi 3, 2026, kimeishusha Mbeya City kwa nafasi moja kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbeya City ambayo awali ilikuwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 13, imeshuka kwa nafasi moja hadi ya 14 ikipishana na Fountain Gate ambayo imepanda kwa nafasi moja hadi ya 13.

Bao pekee la Fountain Gate katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya limepachikwa na Sadick Ramadhan katika dakika ya 79 akiunganisha krosi ya Henry David.

Kabla ya kuingia kwa bao hilo, timu hizo zilishambuliana kwa zamu katika nyakati tofauti lakini safu zao za ulinzi zilikuwa imara kuondosha hatari ambazo zilielekezwa kwao.

Ushindi huo umeifanya Fountain Gate kulipa kisasi kwa Mbeya City kwani katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Tanzanite Kwaraa, Babati ilipoteza kwa kichapo kama cha leo.

Kwa upande mwingine kichapo cha leo kimeifanya Mbeya City kuendeleza historia yake mbaya ambayo imekuwa nayo msimu huu katika Uwanja wake wa nyumbani ambapo hadi sasa haijawahi kushinda ikiwa mwenyeji.

Timu hiyo katika mechi sita ilizocheza nyumbani msimu huu, imetoka sare nne na kupoteza michezo miwili, ikifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa Fountain Gate baada ya kucheza mechi sita mfululizo za Ligi Kuu bila kupata ushindi ambapo imetoka sare mbili na kupoteza michezo minne.

Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea keshokutwa kwa uwepo wa mechi mbili zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti nchini.

Katika Uwanja wa Airtel Singida, wenyeji Singida Black Stars wataikaribisha Yanga na Tanzania Prisons itakuwa katika Uwanja wake wa Sokoine kucheza na Azam FC.