Kibano kipya wapotevu wa muda uwanjani, kuanzia Kombe la Dunia
Hatua hiyo ni mwendelezo wa sehemu ya kipengele cha sheria ya muda wa mchezo cha mwaka jana kilicholenga kuwazuia makipa kushikilia mpira kwa muda mrefu kupita kiasi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika Marekani, Canada na Marekani kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka huu zikishirikisha timu za taifa 48.
Chombo kinachosimamia sheria za soka duniani, kimetangaza mabadiliko kadhaa muhimu yatakayoanza kutumika rasmi wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2026, yakilenga kuongeza kasi ya mchezo na kuondoa mbinu za makusudi za kupoteza muda.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika Marekani, Canada na Marekani kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka huu.
Kwa mujibu wa maamuzi hayo, Refa atakuwa na mamlaka ya kuanza kuhesabu sekunde tano kwa ishara ya mkono endapo ataona kurusha mpira wa pembeni au mpira uliopo katika eneo la hatari kunacheleweshwa kimakusudi.
Iwapo muda huo utaisha kabla ya mpira kurejeshwa uwanjani, umiliki utahamia kwa timu pinzani. Mpira wa kurusha utatolewa kwa upande mwingine, huku kuchelewesha mpira uliopo langoni kutaadhibiwa kwa timu pinzani kupewa kona.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa sehemu ya kipengele cha sheria ya muda wa mchezo cha mwaka jana kilicholenga kuwazuia makipa kushikilia mpira kwa muda mrefu kupita kiasi.
Katika mabadiliko mengine, mchezaji anayefanyiwa mabadiliko atalazimika kuondoka uwanjani ndani ya sekunde 10 tangu ubao wa mabadiliko uonyeshwe au mwamuzi atoe ishara.
Akishindwa kufanya hivyo, mchezaji mbadala atalazimika kusubiri hadi mpira usimame tena baada ya dakika moja ya mchezo kupita kabla ya kuingia. Hata hivyo, mchezaji anayetolewa atalazimika kuondoka mara moja bila kuchelewa.
IFAB pia imeelekeza kuwa mchezaji anayepatiwa huduma ya kwanza uwanjani au ambaye jeraha lake limesababisha mchezo kusimama, atalazimika kutoka nje ya uwanja pindi mchezo unapoanza tena na kubaki nje kwa angalau dakika moja.
Sera hiyo inalenga kukomesha mbinu za kujifanya majeruhi ili kupunguza kasi ya mchezo au kuvunja presha ya timu pinzani.
Kuanzia sasa, VAR itaruhusiwa kuingilia maamuzi katika matukio matatu ya ziada pale ushahidi wa wazi utakapokuwepo. Matukio hayo ni;
Kadi nyekundu iliyotokana na kadi ya pili ya njano iliyotolewa kimakosa, tukio la utambulisho usio sahihi wa mchezaji na kona iliyotolewa kimakosa kwa uwazi.
Kumekuwa pia na ufafanuzi kuhusu mpira wa kudondoshwa, ambapo umiliki utapewa timu ambayo ingekuwa imeendelea kumiliki mpira kama mchezo usingesimama.