Mazembe, Al Hilal zainufaisha Simba

Muktasari:
Kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mechi walizopata katika mashindano ya Simba Super Cup yamefanya wapate kipimo sahihi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mechi walizopata katika mashindano ya Simba Super Cup yamefanya wapate kipimo sahihi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza Dar es Salaamjana, Gomes alisema katika mashindano hayo mechi yao na TP Mazembe iliyomalizika kwa suluhu ilikuwa ni kipimo kikubwa zaidi kwao kuliko dhidi ya Al Hilal.
“Mechi yetu na Mazembe ilikuwa ngumu zaidi ya Al Hilal, ulikuwa mchezo wa kukaba na kushambulia sana, lakini wachezaji wangu wamecheza vizuri na hiki ni kipimo tosha kwa ajili ya mechi zetu zijazo.
“Tulikosa nafasi nyingi za kufunga, hasa kipindi cha kwanza, lakini tupo katika wakati mzuri wa kuanza mechi za ligi na kimataifa,” alisema.
Gomes alisema baada ya kutwaa Simba Super Cup, amegeuzia akili yake upande wa ligi ili kuhakikisha kwamba wanachukua ubingwa.
“Malengo yetu ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kila msimu ili kushiriki kimataifa mara kwa mara, najua tuna michezo miwili migumu ya ligi kati ya Dodoma na Azam, lakini tutahakikisha tunashinda.
“Simba ni timu kubwa sasa Afrika, hivyo wana kila sababu ya kufanya vizuri katika mashindano ambayo wanashiriki,” alisema kocha huyo raia wa Ufaransa
Kwa upande wao, nyota wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema kitendo cha Simba kucheza na TP Mazembe na Al Hilal kimewapa faida wachezaji pamoja na benchi la ufundi katika maandalizi yao kimataifa.
Malima alisema kutokana na ugeni wa wachezaji pamoja na kocha wao, walivyopata mechi hizo imekuwa na faida kwa wote katika kujiweka sawa.
“Mwalimu ni mpya na kuna wachezaji wapya, lakini tutambue kabisa kucheza na hizo timu ni faida kubwa kwao, pia mwalimu amejua yupi amtumie na yupi asimtumie,” alisema Malima.
Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema Simba wamefanikiwa kimawazo kwani kucheza mechi na timu mbili kubwa ni malengo ya muda mrefu hasa wakiangazia upande wa Ligi ya Mabingwa.
“Simba wanajua nini wanachokitaka katika Ligi ya Mabingwa na ndiyo maana wameamua kuandaa mashindano haya, wana mechi ngumu na wamepata kipimo kigumu, bila shaka wamefanikiwa kwa ujumla.
“Faida nyingine ambayo Simba wameipata ni kucheza hizi mechi, kwani hata wachezaji ambao walikuwa hawachezi na wao wamepata muda wa kucheza, kuna utofauti kati ya kucheza na kutocheza kabisa,” alisema kiuongo huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.